IGP SAID MWEMA APANGA KUTOA TAARIFA YA MIPANGO YA KU UAWA KWA DR. MWAKYEMBE
JAMII 4:44 AM
MKUU wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema, leo anatarajiwa kutoa taarifa juu ya hatua zilizochukuliwa na jeshi hilo, kuhusiana na tuhuma za kuwepo kwa njama za kuua baadhi ya viongozi wa serikali na wa vyama vya siasa.
Tuhuma hizo nzito ni zile zilizowahi kutolewa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe, na kurejewa tena juzi na Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Mwema alisema hayo jana alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake ambao pamoja na mambo mengine, walimtaka aeleze ni hatua gani zilizochukuliwa na jeshi hilo mpaka sasa tangu Mwakyembe atangaze orodha ya baadhi ya wanasiasa na viongozi wa serikali walio katika hatari ya kuuawa.
Tuhuma hizo zimezidi kupata uzito wake hivi sasa kutokana na kuwepo kwa utata wa chanzo cha maradhi yanayomsibu Mwakyembe ambaye yuko nchini India kwa matibabu.
“Maswali yote haya yaliyosalia, nitayajibu kesho saa tano na niseme ni maswali mazito kwa hiyo nitayajibu kwa uzito wake maana nisingeweza mambo yote haya kuyatolea majibu leo leo. Kwa hiyo naomba tukubaliane hivyo kwamba kesho tutaendeleza mkutano huu tena,” alisema Mwema.
Taarifa kuhusu maradhi yanayomsibu Mwakyembe zimeibua utata mwingi, hasa ikikumbukwa kuwa mwezi Machi, mwaka huu, alikaririwa akidai kuwepo kwa njama za kuuawa kwake na baadhi ya viongozi na wanasiasa wengine wanaoonekana kuwa mstari wa mbele kupinga ufisadi.
Ndani ya tuhuma hizo, naibu waziri huyo alieleza hatua kwa hatua kuhusu kile alichokiita mpango wa utekelezaji wa mkakati huo wa mauaji, akiwahusisha baadhi ya maafisa wa polisi, usalama wa taifa na mganga mmoja wa jadi.
Aidha alisema njia zilizopangwa na watu hao kutekeleza mpango huo wa mauaji ni pamoja na kutumia ajali ya gari, ushirikina na sumu.
Miongoni mwa wanasiasa na viongozi aliowataja kuwa katika orodha ya kuuawa ni pamoja na Waziri wa Maji, Profesa Mark Mwandosya, ambaye naye yuko India hivi sasa akipata matibabu na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.
Wengine ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; na Mbunge wa Same Mashariki Anne Kilango.
Kutokana na uzito wa tuhuma hizo, jeshi la polisi lilimtaka Mwakyembe atoe tuhuma hizo kwa maandishi, hatua ambayo aliitekeleza, lakini tangu wakati huo hakuna hatua yoyote iliyoelezwa kuchukuliwa na jeshi hilo.
Tishio la ugaidi
Mapema akizungumza na waandishi wa habari, IGP Mwema alisema jeshi hilo limechukua tahadhari zote dhidi ya tishio la mashambulizi ya kigaidi kutoka kundi la al-Shabaab, kama yalivyotokea hivi majuzi katika nchi jirani ya Kenya.
Alisema polisi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya usalama, likiwemo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wameimarisha ulinzi katika mipaka yote na hali ni shwari.
Alitoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari na kutoa taarifa polisi pindi watakapoona dalili zozote za kufanyika kwa tukio lisilokuwa la kawaida.
Mwema alisema chanzo cha ugaidi kinatokana na kuwepo kwa ushabiki wa kidini, kisiasa, mila na utamaduni; kukosa hoja na uvumilivu; kuwa na migogoro ya kijamii isiyopatiwa ufumbuzi mapema; pamoja na kushamiri kwa shughuli za magendo ya silaha haramu na dawa za kulevya.
Pia alikiri kuwepo kwa wahamiaji haramu wanaoendesha maisha yao bila mamlaka zilizopo kuwa na taarifa na kwamba matokeo yake ni kuwepo kwa matukio mengi ya uharamia katika ukanda wa Bahari ya Hindi.
Hata hivyo, alibainisha kuwa tayari Jeshi la Polisi limewakamata maharamia 13 na wameshafikishwa mahakamani.