DR.KIKWETE AKATISHA MAPUMZIKO NA KUREJEA DAR ILI KUWAFARIIJI MAMIA YA WAATHIRIKA WA MAFURIKO


 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akiongoza maombolezo ya wananchi 20 waliopoteza maisha kwenye mafuriko jijini Dar es salaam baada ya kukatisha  mapumziko yake ya sikukuu na kurejea Dar es Salaam kujionea mwenyewe madhara na uharibifu wa mafuriko pamoja na kutoa mkono wa pole kwa waliopoteza ndugu zao, kuumia ama kuharibiwa nyumba zao na mafuriko hayo.
 
Mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius K Nyerere akitokea kwenye Mbuga ya Wanyama ya Serengeti, mkoani Mara, ambako alikuwa anapumzika, Rais alilakiwa na mawaziri na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Said Mecky Sadiq.

Mheshimiwa Sadiq amemweleza Mheshimiwa Rais kuhusu hali halisi ya mafuriko katika Mkoa wa Dar es Salaam na madhara yake akisema kuwa mpaka sasa watu 20 wamethibitishwa kupoteza maisha na watu wengine 68, wakiwamo wakazi 66 wa Wilaya ya Ilala, wamejeruhiwa kutokana na mafuriko hayo.

Mkuu huyo wa Mkoa pia amemweleza Rais Kikwete kuwa watu 4,909 wamepatiwa hifadhi ya muda katika sehemu mbalimbali, hasa katika shule za msingi na sekondari, baada ya nyumba zao kuharibiwa katika mafuriko hayo yaliyotokana na mvua zilizoanza kunyesha tokea usiku wa kuamkia Jumatatu, Desemba 19,mwaka huu hadi leo.

Amemwambia Rais Kikwete kuwa kata zote 30 katika wilaya zote tatu za Mkoa wa Dar es Salaam zimeathiriwa na mafuriko hayo na kuwa wengi wa watu ambao nyumba zao zimeharibiwa na kubomolewa katika mafuriko hayo wamehifadhiwa na wanapatiwa huduma na Serikali.

Mara baada ya kupatiwa maelezo hayo, Rais Kikwete amepanda helikopta kukagua maeneo yote yaliyoathiriwa na mafuriko hayo hasa yale yaliyoko katika Bonde la Mto Msimbazi na baada ya ukaguzi huo alikwenda kuwapa mkono wa pole na kuwajulia hali wananchi waliopewa hifadhi katika Shule ya Msingiya Mchikichini katika Wilaya ya Ilala.

Kuna kiasi cha watu 1,900 katika shule hiyo na akizungumza nao, Rais Kikwete amesema kuwa alikuwa amefika kuwapa pole kwa matatizo yaliyowafika.

“Nimekuja kuwapeni pole na maafa yaliyowafika. Nimekuja kuwahakikishenikuwa tupo, tuko nanyi na tutahakikisha kuwa mnapata huduma zote za msingiza chakula, za afya, za usafi kwa maana ya kila aliyeko hapa kupatiwa godoro, blanketi na chakula.”

Rais Kikwete pia ametumia nafasi hiyo kuwaagiza wote wanaohusika na mipango ya miji na usalama wa wananchi kuhakikisha kuwa wanatafuta na kupata majawabu ya kudumu ya watu kuathiriwa mara kwa mara na mafuriko kwa sababu ya kujenga na kuishi katika maeneo ya mabonde.

“Fanyeni uamuzi wa kutokujenga tena ama kutokurejea tena katika maeneo ya mabonde. Fanyeni uamuzi wa kutokuishi katika mazingira ya mashaka ya usalama wenu na wa familia zenu kila mvua inaponyesha. Hasara mnaijua zaidi nyie, hasara za kujenga upya, hasara za kusafisha tope, hasara za kununua samani mpya kila mvua inaponyesha,” Rais Kikwete amewaambia wananchi hao.

Rais amewaagiza maofisa wanaohusika kuwasaidia watu wanaoishi mabondenikuhamia sehemu nyingine. “Napenda kuwahakikishieni kuwa tutawapatia maeneo ya kuishi nje ya mabonde na maofisa wote wanaohusika wako hapa wamenisikia.”

Rais Kikwete pia amesimama kwa muda kwenye Barabara ya Morogoro na kuwajulia hali walioathiriwa na mafuriko katika eneo hilo ambao wameweka makazi yao kwenye miti iliyoko barabarani hapo baada ya nyumba zao kuzingirwa na kuharibiwa na maji katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam eneo la ekari 200 na lenye uwezo wa kutoa viwanja 2,800 limeainishwa katika eneo la Mbopo, Wilaya ya Kinondoni, kwa ajili ya kutoa viwanja kwa walioathiriwa na mafuriko hayo baada ya wenye viwanja hivyo kulipwa fidia.


 Rais Kikwete akiongea na waathirika wa mafuriko hayo waliohifadhiwa kwenye shule ya Msingi ya Mchikichini
 Baadhi ya walioathirika na mafuriko wakimsikiliza Rais Kikwete
 Waathirika wa mafuriko wakimsikiliza Rais Kikwete
 Rais Kikwete akiendelea kuongea na waathirika wa mafuriko
 Rais Kikwete akitembelea madarasa walikohifadhiwa baadhi ya waathirika katika shule ya msingi ya Mchikichini. Mbele yake ni Mbunge wa Ubungo Mh John Mnyika
 Rais Kikwete akikagua chakula kilichoandaliwa waathirika hao
 Rais Kikwete akioneshwa chakula hicho
 Rais Kikwete akisalimiana na kinamama waliohifadhiwa shule ya msingi Mchikichini
 Rais Kikwete akiangalia athari za mafuriko hayo katika bonde la mtomMsimbazi maeneo ya Jangwani
 Baadhi ya wakaazi walioko katika bonde la mto wa Msimbazi maeneo ya Jangwani wakiwa bado kwenye paa
 Rais Kikwete akiwa ameongozana na viongozi wa mkoa wa Dar es salaam
 Rais Kikwete akisalimiana na baadhi ya viongozi wa serikali za mitaa  wa mkoa wa Dar es salaam
 Rais Jakaya Kikwete akisalimiana na Mbunge wa Ubungo Mh John Mnyika. Kulia ni Meya wa Kinondoni Mstahiki Mwenda
 Rais Kikwete akiongea na walioathirika na mafuriko eneo la Jangwani
 Rais Kikwete akisalimiana na waathirika eneo la Jangwani
 Rais Kikwete na mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh Saidi Mecky Sadiq wakiangalia athari Jangwani
 Wakaazi wa eneo la Jangwani wakimshangilia Rais Kikwete baada ya kuhakikishiwa misaada pamoja na kuhamishiwa sehemu zingine
 Wakaazi wakipiga makofi baada ya kuahidiwa misaada pamoja na maeneo mapya ya makaazi
 Rais Kikwete akiongea na wakaazi wa Jangwani
 Rais Kikwete akiwafariji wakaazi wa Jangwani
 Rais Kikwete akisalimiana na waathirika wa mafuriko Jangwani
 "....Poleni jamani"
 Rais Kikwete akiwafariji wakaazi wa Jangwani
 Baadhi ya waathirika wa mafuriko wakiwa katika hifadhi ya muda Shule ya msingi ya Mchikichini
 Mbunge wa Ilala Mh Zungu na Mbunge wa Ubungo Mh John Mnyika wakitafakari kwa masikitiko
 Baadhi ya wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu wakimsikiliza Rais Kikwete
 Baadhi ya waathirika wakiwa katika darasa la Shule ya msingi ya Mchikichini
 Ni wakati wa kufua
 Mtoto akiwa shule ya msingi Mchikichini
 Sehemu ya madarasa yanayohifadhi waathirika
 Mwananchi akijipumzisha baada ya dhahama ya siku mbili ya mafuriko

 Rais Kikwete na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mh Sadiq wakirejea baada ya kuzunguka kwa helikopta kujionea madhara hayo ya mafuriko
 Rais Kikwete akiwa ndani ya Heikopta ya JWTZ kukagua madhara ya mafuriko
 Rais Jakaya Kikwete akipata maelezo ya madhara ya mafuriko Dar
 Rais Kikwete akiwasili kutoka mkoani Mara ambako amekatisha mapumziko yake ya mwaka kujionea madhara ya mafuriko

Posted by Bigie on 10:03 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.