JESHI LA CONGO LASAMBAZA VIFARU KATIKA JIJI LA KINSHASA IKIWA NI MAANDALI YA KUAPISHWA KWA JOSEPH KABILA
JAMII 4:28 AM
Jeshi la Congo limesambaza vifaru kote jijini Kinshasa kama hatua ya kujiandaa kuapishwa kwa Rais Joseph Kabila kufuatia Uchaguzi wenye utata uliofanywa mwezi uliopita.
Ni viongozi wachache tu wa mataifa ya Afrika wameahidi kuhudhuria; na waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ubelgiji aliyekuwa amepanga kuhudhuria sherehe hizo amefutilia mbali ziara hiyo.
Ameahidi kuwa huenda akafika nchini humo baada ya matangazo ya uchaguzi wa Bunge kutangazwa katika mazingira yaliyo bora zaidi.
Wachunguzi wa nchini na wa kimataifa wameshutumu ukiukaji mkubwa wa utaratibu wa upigaji kura katika uchaguzi wa Urais na Bunge uliofanywa Novemba 28; tayari kiongozi mkuu wa upinzani Etienne Tshisekedi amejitangaza kuwa Rais baada ya kukataa kukubali matokeo.
Tshisekedi alisema Jumamosi kuwa atajiapisha mwenyewe kuwa Rais baadaye juma hili katika uwanja mkuu wa michezo jijini Kinshasa. Kiongozi huyo wa upinzani pia alitoa wito kwa vikosi vya usalama viheshimu amri yake badala ya Rais Kabila, ambaye alisema amevunja Serikali yake.
Upande wa Rais Kabila umetaja matamshi ya Tshisekedi kama ya uhaini.