Membe: Nikiwa Rais Wasanii Wataenda Kujifunza Nje
siasa 8:43 PM
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
amesema kama atachaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, atahakikisha anasimamia haki za wasanii ipasavyo.
Membe alitoa kauli hiyo mkoani Lindi wakati akitangaza nia ya kuwania
urais kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
“Nitahakikisha naweka mipango imara katika kusimamia kazi za wasanii wote kunufaika na hakimiliki zao,” alisema.
Pia alisema atahakikisha wasanii wanakwenda kujifunza nje ya nchi
masuala ya sanaa ili sekta hiyo ipate mabadiliko ya kimaendeleo kwa
wasanii na Serikali kwa ujumla.
“Nikichaguliwa kuwa rais, nimejiwekea mikakati mingi kuhakikisha sekta
ya sanaa inapiga hatua kutoka hapa tulipo sasa,” alisema Membe.
Katika mkutano huo, waliohudhuria ni baadhi ya wasanii akiwemo
mchekeshaji, Adam Melele ‘Swebe’, Hemed Malyaga ‘Mkwere Orijino’ na
Kulwa Kikumba ‘Dude’.
Gazeti la Mtanzania