SAMWEL SITTA AKIRI KUWA CHADEMA INAKUBALIKA KWA KUPINGA UFISADI


WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samwel Sitta, amesema nguvu ya Chama cha Demokrasia (CHADEMA) inatishia uhai na utawala wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Akizungumza katika kipindi cha dakika 45 kinachorushwa na kituo cha televisheni cha ITV, waziri huyo ambaye pia aliwahi kuwa Spika alisema:  
“Mambo kama haya nasema hata kule Igunga CHADEMA walituhangaisha na kujipatia umaarufu wa kukubalika kwa wananchi kutokana na udhaifu wetu na hasa tabia hii ya kuendelea kuwabeba watu wasio waadilifu wenye tuhuma za ufisadi.

“…CHADEMA katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana hawakuwa na mgombea lakini kwenye uchaguzi mdogo wameibuka na kura zaidi ya asilimia 43, wanatumia udhaifu wetu wa tuhuma za ufisadi na ugumu wa maisha halafu wanazijengea hoja wananchi wanawakubali wao. Hapa lazima tujibadilishe na kujipanga upya.”

Alisema nguvu iliyoonyeshwa na CHADEMA katika uchaguzi huo, ilitokana na udhaifu wa CCM ambayo inaendelea kuwakumbatia mafisadi.
Alisema CHADEMA wameweza kutumia udhaifu huo na ugumu wa maisha wa wananchi kuushawishi umma.

Katika uchaguzi huo uliofanyika kujaza nafasi ya Rostam Aziz aliyejiuzulu kwa madai kwamba amechoshwa na siasa uchwara ndani ya CCM, mgombea wa chama hicho, Dk. Peter Kafumu, alishinda kwa kura 26,484 akifuatiwa na wa CHADEMA, Joseph Kashindye, aliyepata kura 23,260 na Leopold Mahona, wa CUF, kura 2,104.

Sitta alisema katika uchaguzi ujao ndani ya CCM, chama chake kinapaswa kujipanga na kupata safu mpya ya uongozi wenye maadili ili watue mzigo wa mafisadi ambao wanafanya vitendo hata vya kulitia hasara taifa bila kujali, kwani lengo lao ni utajiri.

Alisema mambo si shwari ndani ya CCM, akaonya kwamba endapo chama hicho hakitabadili mfumo na utendaji wake, kitakumbwa na ushindani mkubwa wa kisiasa huko mbele.

“Nadhani unaona hali ya kisiasa inavyozidi kuwa ngumu, wenzetu wa CHADEMA wanatumia mbinu ya umaskini walionao wananchi na hoja ya mafisadi ambayo inazidi kuwajengea umaarufu. Kielelezo tosha ni matokeo ya uchaguzi Igunga ambao CHADEMA walipata aslimia 43. Kumbuka ni mwaka jana tu tumefanya uchaguzi mkuu lakini wananchi wamegeuka,” alisema Sitta.


Waziri Sitta alitumia kipindi hicho kusisitiza kauli yake ya mara kwa mara kwamba hahusiki na uanzishwaji wa chama cha siasa cha CCJ na kudai kuwa yeye ni mwanasiasa na amekuwa akikutana na wanasiasa wenzake wakiwemo wale wa kambi ya upinzani na kujadili mambo mengi, hivyo haoni kuwa huo ni usaliti.

“Unajua ukishakuwa mwanasiasa utakutana na wenzako, wapo wanaokuja tunazungumza na wananiambia huko uliko hakufai njoo upande huu, naomba kukujulisha au kuujulisha umma kuwa mimi ni mwana CCM na nitabaki CCM, lakini ujue kuwa CCM si baba yangu au mama yangu nikiona yamenishinda nitajua cha kufanya,” alisema Sitta.


Hata hivyo, zipo kumbukumbu nyingi zinazoonyesha kuwa Sitta alikuwa miongoni mwa wanasiasa waandamizi ndani ya CCM walioasisi CCJ kwa malengo ya kushindana na CCM na CHADEMA katika uchaguzi mkuu wa 2010.

Mbali na Sitta, makada wengine wa CCM walioasisi CCJ kwa madai kwamba wanakerwa na mwenendo wa CCM, ni Nape Nnauye, Dk. Harrison Mwakyembe na Fred Mpendazoe.
Miongoni mwao, Mpendazoe ndiye alijitoa mhanga kwa kuondoka CCM na kupoteza ubunge wa Jimbo la Kishapu; lakini CCJ kilipokosa usajili wa kudumu akajiunga na CHADEMA. Baadaye aliandika kitabu na kuwataja aliokuwa nao, ingawa wamekuwa wanakanusha kuhusika na harakati hizo.

Sitta ndiye amekuwa kinara wa kundi lililojipachika jina la “wapambanaji wa ufisadi” ambalo wachambuzi wa siasa wanasema lilijitokeza ili kuuza nguvu ya CHADEMA katika mapambano ya ufisadi.

CHADEMA ndiyo iliyoasisi hoja na mapambano ya ufisadi na kwa mara ya kwanza ilianika hadharani orodha ya watuhumiwa ufisadi 11, Septemba 2007, Mwembeyanga, Dar es Salaam.
Orodha hiyo iliwasilishwa na aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Dk. Willibrod Slaa, baada ya Sitta, akiwa Spika wa Bunge, kukataa hoja ya Dk. Slaa kuhusu ufisadi na kutishia kumshtaki kwa maelezo kuwa alikuwa ameghushi vielelezo alivyokuwa navyo.

Hata hivyo, baada ya kuona kasi ya vita ya ufisadi imeshika moto, Sitta na kundi lake, wakiwamo pia Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango, na Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka, waliibuka na kuanza kushambuliana na makundi mengine ndani ya CCM waliotajwa na Dk. Slaa.

Hata hivyo, wachambuzi wanasema kwamba nia ya kina Sitta haikuwa kupigana na ufisadi, bali kuendeleza vita ya makundi ndani ya chama chao, na kuipiku CHADEMA katika vita ya ufisadi, ili wananchi waone kwamba hata ndani ya CCM kuna wanaochukia ufisadi.
Baadaye, Rais Jakaya Kikwete amekuja kuitumia hoja ya ufisadi kuwachukulia hatua za kisiasa na kisheria baadhi ya waliotajwa katika orodha hiyo, ingawa naye ni miongoni mwa waliotajwa.

Wachambuzi wa kisiasa wanasema hatua hiyo ya Rais Kikwete ni propaganda za kisiasa za kutaka kujikosha mbele ya Watanzania, kwani sehemu ya ufisadi unaowahusu hao wanaotuhumiwa ilimhusisha au kumhusu pia yeye, kwani baadhi ya pesa zilizotumika kumwingiza madarakani zilitokana na ufisadi.

Baadhi ya makada ndani ya CCM wamekuwa wanahusisha kauli za Sitta na uchaguzi mkuu ujao, ingawa yeye amesema juzi kwamba hana nia ya urais.

Hata hivyo, inajulikana kwamba Sitta ana kundi lake, na kauli zake zinalenga kuwadhoofisha baadhi ya wanaofikiriwa kuusaka urais ndani ya chama chake, ambao wanadhaniwa kuwa washindani wake au wa kundi lake.

Posted by Bigie on 10:50 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.