MAKAMU WA RAIS ATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA MKUU WA JESHI LA POLISI NCHINI NA MKUU WA MKOA WA TANGA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerari Said Mwema na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Chiku Galawa, kufuatia ajali ya gari la Polisi lililopata ajali na kusababisha kifo cha askari sambamba na kujeruhi wengine, ajali iliyotokea jana katika barabara itokayo Lushoto kuingia mji mdogo wa Mombo. Gari hilo lilikuwa mwishoni mwa msafara wa Makamu wa Rais uliokuwa ukitokea wilayani Lushoto.

Makamu wa Rais alikuwa akimalizia ziara yake mkoani Tanga, ziara aliyoianza Januari 24 na kuikamilisha jana Januari 27 wilayani Lushoto. Msafara wa Makamu wa Rais ulikuwa unatoka Lushoto ukielekea Hale, ambako huko Makamu wa Rais amefika salama.

 Makamu wa Rais amesikitishwa sana na tukio hilo na amewapa pole Mkuu wa Jeshi sambamba na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, na anabainisha kuwa tukio hilo limemgusa sana na anawatakia moyo wa ujasiri na uvumilivu kufuatia tukio hili ambalo limekuja katika kipindi ambacho hakikutarajiwa.

Makamu wa Rais anatarajiwa kuondoka mjini Tanga leo kufuatia kuhitajika kusimamia mkutano wa Kamati ya Muungano unaofanyika leo asubuhi jijini Dar es Salaam, sambamba na kusimamia majukumu mengine ya serikali kufuatia Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Kikwete kuwa nje ya nchi kikazi kwa sasa.

“Naamini mkoa wa Tanga na Jeshi la Polisi watatoa huduma zote zinazohitajika kwa wafiwa sambamba na majeruhi, nami binafsi nitafatilia kwa ukaribu,” anasema Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Bilal.

Imetolewa na: Boniphace Makene
Mwandishi wa Habari wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania

Posted by Bigie on 7:06 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.