CHADEMA : JK NI KIINI CHA UOZO. SASA WATISHIA KUANDAMANA NCHI NZIMA


WAKATI Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikidai kuwa kiini cha hali ya nchi kuwa tete kimetokana na tabia ya Rais Jakaya Kikwete kukumbatia watendaji wabovu, baadhi ya mawaziri wanaotakiwa kujiuzulu wameanza kuhaha kujaribu kujinasua.

Miongoni mwa mawaziri hao ni Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami, ambaye ametuhumiwa kumlinda Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Charles Ekelege, amekanusha akidai kuwa hakupata ushauri kutoka kwa wasaidizi wake na hana maslahi yoyote na mtendaji mkuu huyo wa shirika hilo.

Hata hivyo, uchunguzi  umebaini kuwa waziri huyo sio tu alikaidi ushauri wa wataalamu wa wizara yake, bali pia alidiriki hata kumpuuza naibu wake, Lazaro Nyalandu.

Naye Waziri wa Uchukuzi Omar Nundu, katika staili ileile ya kukwepa kuwajibishwa, amemtwisha zigo Naibu Waziri wake, Athuman Mfutakamba, kuwa ndiye aliyeshinikiza kampuni ya China Communication Construction (CCC) kujenga gati namba 13 na 14 baada ya kugharamiwa safari nje ya nchi bila idhini yake.

Ni katika hali tete hiyo, CHADEMA imesema itachukua maamuzi magumu dhidi ya serikali ikiwa Rais Kikwete leo atashindwa kuwachukulia hatua na kuwalazimisha kujizulu mawaziri wake wanaotuhumiwa kufuja malioni ya fedha.

Akihutubia maelfu ya wakazi wa jiji la Mwanza katika viwanja vya Sahara jana, Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa alisema watachukua maamuzi magumu yatakayoitikisa nchi, ikiwa ni pamoja na kuongoza maandamano mazito na makubwa ya umma kushinikiza mabadiliko ya utawala.

Dk. Slaa, amedai kuwa hali ya nchi sasa ni mbaya na njia pekee ya kuiwajibisha serikali bila kumwaga damu ni kwa wananchi kuungana na kuandamana nchi nzima.

Alimshambulia Rais Kikwete akidai kuwa chanzo cha matatizo yanayolikumba taifa ni tabia ya kuwakumbatia watu waovu badala ya kuwachukulia hatua za kisheria na kiutawala.

Amesema kuwa CHADEMA imebaini kuwa kuna kila dalili kwamba Rais Kikwete hatachukua hatua kali dhidi ya wasaidizi wake baada ya kuwepo kwa kigugumizi kingi katika suala hilo.

Dk. Slaa aliongeza kuwa hali tete ya nchi isingefika hapa ilipo kama Rais Kikwete angekuwa makini na mkali kwa mambo ya taifa na kama angezingatia ushauri wake (Slaa) wa kumtaka avunje Baraza la Mawaziri mapema mwaka huu.

“Uozo uliofanywa na mawaziri umekuwa ukipata baraka zake kama Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri, na amekuwa na kawaida ya kulinda ubovu wa mawaziri wake kutokana na udhaifu wake mwenyewe wa kiuongozi."

Slaa alisema katika hali ya kawaida, Rais ndiye alitakiwa avunje Baraza la Mawaziri badala ya kusubiri kufanyiwa kazi hiyo na wabunge, hali ambayo inadhihirisha udhaifu wake katika kuongoza nchi.

“Kikwete ndiye chanzo cha udhaifu wote serikalini unaosababisha matatizo makubwa kwa taifa na wananchi. Ni kiongozi anayekwepa lawama na kubebesha mzigo wa uzembe wake kwa watu wengine,” alisema.

Alisema kuwa CHADEMA itapeleka hoja ya kutokuwa na imani na Rais Kikwete kwa wananchi kwa mujibu wa Ibara ya 8 ya Katiba kupitia mikutano na maandamano kama alivyoahidi Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

Aidha, Dk. Slaa ametoa siku saba kwa Jeshi la Polisi, mkoani Mwanza, kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watu waliohusika kuwakata mapanga wabunge wa CHADEMA wiki kadhaa zilizopita.

Sakata la TBS
Katika sakata la TBS, Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma kwa kutotekeleza pendekezo lake la kumtaka amsimamishe kazi mkurugenzi mkuu wa shirika hilo ili achunguzwe kuhusiana na kashfa ya kutoa mikataba kwa kampuni hewa ya kukagua magari na Singapore na Hong Kong, katika utetezi wake, Chami alisema kuwa hakumsimamisha Ekelege kwa vile anafuata utaratibu ulioainishwa mwaka 2004 ambao unaitaka wizara kusimamia mashirika yaliyo chini yake lakini si kuyaingilia katika utendaji wake wa kazi.

“Mkurugenzi akituhumiwa na yeyote, kanuni zinaelekeza kuwa waziri anapaswa kupata ushauri wa bodi ya wakurugenzi juu ya tuhuma zilizotolewa kisha kuwasilisha kwa mamlaka ya uteuzi yaani Rais,” alijitetea Chami.

Imedaiwa kuwa uzembe huo ulichangiwa pia na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu, anayetajwa kuwa alizembea kwa kutomshauri waziri na hivyo anapaswa pia kuachia ngazi.

Hata hivyo, uchunguzi uliofanya  kupitia nyaraka kadhaa, unaonyesha kuwa Nyalandu alitaka Mkurugenzi Mkuu wa TBS asimamishwe kazi, kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.

Nyalandu ambaye pia uchunguzi umebaini kuwa sio miongoni mwa mawaziri walioshinikizwa kuandika barua ya kuachia ngazi, alimshauri Waziri Chami, kutumia mamlaka yake kumsimamisha Ekerege.

Mwandishi wetu amebaini kuwa Nyalandu alitimiza wajibu wake ipasavyo kwa kumwandikia waziri wake dokezo Februari 10, mwaka huu, akimshauri aangalie uwezekano wa kumsimamisha kazi kwa muda mkurugenzi wa TBS ili apishe uchunguzi.

Katika dokezo hilo ambalo Tanzania Daima imepata nakala yake, Nyalandu anaeleza jinsi wabunge walivyoishutumu TBS wakati wa kikao cha pamoja cha kamati tatu za Bunge, kuhusiana na ukaguzi wa magari nje ya nchi na mchakato wote.

Wabunge walioshiriki ziara ya Hong Kong na Singapore walitoa madai kuwa Ekelege aliwadanganya juu ya kampuni zinazokagua magari na bidhaa zingine nje ya nchi na kwamba TBS ilitoa taarifa tofauti ya yale yaliyojiri wakati wa ziara hiyo.

“Ofisi ya CAG na wabunge wametoa mapendekezo ya kuiomba wizara imsimamishe kazi kwa muda Mkurugenzi Mkuu wa TBS ili kupisha uchunguzi wa CAG juu ya tuhuma hizo.

“Kutokana na unyeti wa shutuma zilizotolewa, nakushauri uangalie uwezekano wa kumsimamisha kwa muda na endapo hatakuwa na tuhuma za kujibu, basi arudishwe kazini mara moja,” alishuri Nyalandu.

Alipotafutwa kwa simu mwishoni mwa wiki ili kupata msimamo wake, Nyalandu alijibu yuko nchini Afrika Kusini, hakutaka kuingia kwa undani juu ya sakata la TBS, lakini akapinga kuandika barua ya kujiuzulu, kwa madai kuwa hana sababu ya kufanya hivyo kwa vile alitimiza wajibu wake katika sakata hilo.

Nundu aibua mapya
Kwa upande wake, Waziri Nundu jana aliwaambia waandishi wa habari kuwa aliyeshinikiza kupewa tenda kampuni ya China Merchant kujenga gati hizo ni naibu wake, Athuman Mfutakamba, hivyo ndiye anayepaswa kujiuzulu.

Waziri huyo alisema tangu alipoingia wizarani hapo alikuwa akilipinga suala hilo na kutaka kampuni mbalimbali 11 zishindanishwe, lakini hakusikilziwa.

“Mimi nilitaka kampuni zishindanishwe, lakini halikufanyika na mbaya zaidi CCC ilinipa mwaliko nikaangalie miradi yao nikakataa, wakamfuata Naibu Waziri wangu wakampeleka China, wakamlipia gharama zote yeye na msaidizi wake tu bila kibali changu, sijui alikwendaje. Anasema nilikuwa sipo alienda kuchukua kibali ofisi nyingine.

“Aliporudi na sio kwamba nilikuwa sipo, wakaenda tena Mauritania, sikujua amekwendaje na wakampeleka Equtorial Guine aliporudu akaandika ripoti na kupeleka kwingine akishinikiza CCC ipewe huo mradi,” alisema Nundu na kusisitiza kutoona sababu ya yeye kujiuzulu katika suala hilo.

Alisema tangu mwaka 2008 hadi Novemba mwaka jana alikuwa hajatimiza ahadi ya kupatikana kwa mkopo kutoka benki ya Exim ya China na kusema kutokana hali hiyo, kampuni hiyo imechelewesha mradi huo.

Alisema jambo la kushangaza sasa mambo yanageuzwa na kudaiwa kuwa na kampuni ya mfukoni, China Merchant.
“Hatari sasa mambo haya yameletwa bungeni, tena yameletwa na kamati yakisema mambo makubwa tena.”

Akionekana kuchukia, Nundu alikwenda mbali zaidi na kudai kama angekuwa na madaraka ningempiga mtu risasi kwa kusemwa vibaya.

Alisema hana njaa ya kuiba fedha za umma, kwani kwa nafasi ambazo amewahi kushika tangu awe mtumishi sehemu mbalimbali nchini na nje ya nchi ana pesa za kutosha za kuishi vizuri yeye na familia yake.

Alisema ana machungu na taifa lake na anafanya kazi ya uwaziri kama kulipa fadhili kwa taifa ambalo lilimsomesha ndiyo maana anapigwa vita kila kona kwa sababu amebana ulaji wa baadhi ya watu ndani ya wizara yake na ndani ya Mamlaka ya Bandari (TPA).
Nundu alisema sio kwamba yuko kwenye nafasi ya uwaziri kwa ajili ya kusaka fedha bali anataka kulisadia taifa lake na amekuwa anajitahidi kufanya kazi kwa maadili makubwa.

“Mimi ni kama niko porini na nimevamiwa na majambazi napiga kelele lakini hakuna mtu wa kunisaidia,” alisema Nundu akimaanisha kuwa wanaompiga vita ni wale wanaotaka kufuja fedha kwa kutumia miradi ambayo yeye anaona kuna mianya ya rushwa.

Sakata la kutaka mawaziri takriban nane wajiuzulu, liliibuka bungeni juzi ambapo wabunge walianza mchakato wa kutia saini za kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, hali iliyoifanya kamati ya wabunge wa CCM kulazimika kukutana kwa dharura na kuwaamuru mawaziri hao kuandika barua za kujiuzulu wenyewe.

Waliotajwa katika orodha hiyo, ni pamoja na Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo; Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Prof. Jumanne Maghembe; Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Haji Mponda; na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami.

Wengine ni Waziri wa Uchukuzi, Omar Nundu; Waziri wa Nishati na Madini, William Ngereja; Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige; na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Mkuchika.

Chanzo: Tanzania Daima

Posted by Bigie on 11:04 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.