HUKUMU YA KESI DHIDI YA UBUNGE WA MKOSAMALI NI LEO


MAHAKAMA Kuu Kanda ya Magharibi, leo inatarajia kutoa hukumu ya kesi ya kupinga matokeo ya ubunge wa jimbo la Muhambwe yaliyompa ushindi mbunge wa sasa kupitia NCCR- Mageuzi, Felix Mkosamali.

Kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2010, ilifunguliwa na aliyekuwa mpinzani wake wa karibu katika uchaguzi huo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jamal Abdallah Thamim.

 
Katika madai yake ya msingi, Thamim aliiomba Mahakama itengue matokeo hayo kwa madai kuwa Mkosamali alitumia lugha za kashfa na uchochezi dhidi yake wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Alitaja baadhi ya matamko ya Mkosamali aliyoyaita kuwa ni kashfa dhidi yake kuwa ni pamoja na kumwita jambazi, muuzaji wa viungo vya albino na hatakiwi kuchaguliwa kuwa mbunge kwa kuwa anakata vichwa vya watu.

Katika kesi hiyo, Thamim anatetewa na wakili George Obuya Hezron na Mkosamali anatetewa na mawakili Method R G Kabuguzi Dk Chacha Bhoke.

Mlalamikaji aliiomba Mahakama kuu itengue ushindi wa Mkosamali kwa madai kwamba alitumia mbinu chafu kama vile kutoa kashfa na matusi katika mikutano yake ya kampeni katika maeneo mbalimbali ya Jimbo hilo .

Mbele ya Jaji wa Mahakama Kuu, Aishiel Sumari anayesikiliza kesi hiyo mjini Kibondo, imedaiwa kwamba tuhuma nyingine anazotuhumiwa nazo mbunge huyo ni pamoja na kutumia udini katika nyumba za Ibada kumchafua mlalamikaji, jambo lililosababisha akose kura za kutosha kuwa mbunge wa Muhambwe.

Aidha alitaja kutumia ubaguzi kama sababu nyingine iliyomsababishia kutochaguliwa kwa vile mshindi aliwajenga wapiga kura kumuona mlalamikaji ni mtu asiyestahili kuongoza Jimbo hilo la Muhambwe, jambo ambalo anadai halikubaliki kwa mujibu wa sheria na kanuni za Uchaguzi mkuu.

Wadaiwa wengine katika kesi hiyo ni msimamizi wa uchaguzi katika jimbo hilo pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao kwa pamoja wanalalamikiwa kuendesha uchaguzi kinyume cha utaratibu.

Hiyo ni mojawapo ya kesi tatu za kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2010, ambapo katika kesi ya kupinga matokeo ya ushindi katika Jimbo la Kigoma mjini dhidi ya Peter Serukamba, kesi hiyo namba 3 ya 2010 ilitupiliwa mbali na Jaji Stella Mugasha aliyekuwa akiisikiliza kutokana na mlalamikaji katika kesi hiyo, Ally Mleh wa Chadema kudaiwa kushindwa kutoa ushahidi wa kutosha.

Aidha Mbunge wa Kasulu vijijini, Agripina Zaitun Buyogela naye ushindi wake unapingwa Mahakamani na aliyekuwa Mgombea wa CCM katika jimbo hilo, Daniel Nsanzugwanko kwa madai ya kutumia mbinu chafu katika ushindi wake.

Kesi hiyo inasikilizwa na Jaji wa Mahakama Kuu kutoka Kanda ya Mwanza, Aishiel Sumari.  Awali kesi hiyo ilikuwa inasikilizwa wilayani Kibondo lakini iliahirishwa Aprili 13 na leo kupangwa kutolewa hukumu hapa hapa jimboni.

Jaji Sumari alisema aliiahirisha kesi hiyo na kuipangia hukumu yake baada ya mawakili wa pande zote kuwasilisha hoja za majumuishho.

Hukumu hiyo inasubiriwa kwa shauku kwa wakazi wa jimbo la muhambwe ambapo kila kundi la wafuasi wa mlalamikaji na mlalalamikiwa hawajui nini kitakachotokea.

Wakati wa kesi hiyo, kila upande ulikuwa na mashahidi 32, lakini kadiri muda ulivyosonga upande wa  mlalamikaji ulipunguza mashahidi wake na kubakiza 15 na upande wa utetezi kubakiza 21.

Chanzo: Mwananchi

Posted by Bigie on 11:35 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.