JARADA LA UCHUNGUZI DHIDI YA NASSARI LATUA KWA DDP

JALADA la uchunguzi dhidi ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na wenzake, waliokuwa wakihojiwa na polisi kuhusu kauli walizotoa katika mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Arusha Jumamosi iliyopita, limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) kwa uamuzi zaidi.
 
Mkuu wa Kitengo cha Polisi cha Ufuatiliaji n a Tathmini, katika Makao Makuu ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Issaya Mngulu alisema jana kuwa tayari jeshi limekamilisha uchunguzi na mahojiano na viongozi hao wanaokabiliwa na tuhuma zinazoangukia katika kifungu cha 63 B cha kanuni ya adhabu sura ya 16.

Kwa mujibu wa sheria, kifungu hicho kinahusiana na makosa ya kuhamasisha chuki miongoni mwa jamii kwa kuibua tofauti za matabaka kidini, kikabila, rangi au maeneo na anayekutwa na tuhuma hizo anaweza kushtakiwa kwa makosa ya uchochezi.Mngulu alisema wakati polisi wakisubiri maelekezo kutoka kwa DPP,Nassari na wenzake wameruhusiwa kuendelea na shughuli zao baada ya kuwekewa dhamana kwa ahadi kuwa wataitwa wakati wowote kama watahitajika.

Pamoja na Nassari, kiongozi mwingine wa Chadema aliyehojiwa kwa zaidi ya saa tisa juu ya maneno hayo ni, Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha), John Heche na mwanachama Ally Bananga.

Hata hivyo Katibu Mwenezi wa Chadema wilaya ya Arusha, Emmanuel Kileo ambaye alikuwa miongoni mwa walioitwa na polisi kwa mahojiano ameenguliwa kwenye orodha ya majina yaliyopelekwa kwa DPP kwa kile kinachodaiwa kuwa ushahidi wa kumuunganisha na makosa hayo haupo.

Kileo ndiye aliyeandika barua ya kutoa taarifa ya mkutano kwa Kamanda wa Polisi  wa Wilaya ya Arusha kabla ya siku ya mkutano kama sheria ya vyama vya siasa inavyoelekeza.

Ufafanuzi wa kisheria kutoka kwa mmoja wa mawakili aliyeomba jina lake lihifadhiwe, Nassari na wenzake wanaweza kufunguliwa mashtaka ya uchochezi kwa kigezo cha kuchochea chuki ya wananchi dhidi ya Serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari Jumatatu iliyopita, DCP Mngulu alitangaza kusakwa kwa Nassari ili ahojiwe kuhusu kauli anazodaiwa kutoa kwenye mkutano wa Chadema.

Chanzo: Mwananchi

Posted by Bigie on 12:08 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.