NDUGAI: WABUNGE HAWALALI HOVYO

NAIBU Spika wa Bunge la Muungano, Job Ndugai, amekiri kuwa idadi ya wabunge wanaolala wakati wa vikao vya Bunge imepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na kazi nzito iliyofanywa na vyombo vya habari kuwaweka hadharani wawakilishi wenye tabia hiyo.

Ndugai, pamoja na kutetea kulala huko alikokuita ni ‘kutafakari’, alisema ukali wa mijadala ya Bunge umetokana na wabunge wengi kutambua kuwa wanafuatiliwa kwa makini na wapiga kura wao kutokana na kumulikwa na kutangazwa kikamilifu na vyombo vya habari.

Akifungua mkutano wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyomba vya Habari Duniani uliofanyika jijini Dar es Salaam jana, Ndugai alisema kuwa wabunge wamekuwa makini katika kazi zao wawapo ndani ya Bunge hasa kutokana na vipindi vyake kurushwa moja kwa moja hewani, jambo ambalo limewafanya wapunguze hata kusisinzia.

Pamoja na pongezi hizo, Naibu Spika alivitaka vyomba vya habari kujikita kuandika habari za kuwakosoa wanaotaka kuingia madarakani ili jamii iweze kuelewa udhaifu na uzuri wao.

Alisema kwa kuwa vyombo vya habari ndio mhimili unaoaminiwa na jamii, ambao pia unaweza kujenga au kubomoa haraka, vina haki pia ya kuwajenga na kuwakosoa viongozi watarajiwa ili jamii iweze kuelewa sifa zao kabla ya kuingia madarakani.

“Limekuwa jambo la kawaida kuwakosoa viongozi walioko madarakani tu, pengine umefika wakati sasa kwa vyombo vya habari kuanza utaratibu wa kuandika habari za kuwakosoa watu ambao wanatarajia kuwa viongozi, badala ya kusubiri waingie ndio muanze kuwapiga kama mnavyofanya sasa,” alifafanua.

Kuhusu Bunge na uhuru wa vyombo vya habari, Ndugai alisema kuwa kutokana na mgawanyo wa madaraka, kwenye utawala wa kidekorasia kwa maana ya dola (utawala, Bunge na mahakama), Bunge ndio mhimili pekee ambao unahitaji waandishi wa habari na vyombo vya habari kuliko mihimili mingine.

Kwa upande wa haki za binadamu, alielezea kuwa vyomba vya habari ni sehemu muhimu sana kwenye mapambano dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu na kwamba vyombo vya habari huru ni silaha muhimu sana hususan katika jamii yoyote ya kidemokrasia.

Naibu Spika huyo alieleza kuwa vyombo vya habari vinapashwa kutumika kama jukwaa ambalo wananchi watalitumia kutoa maoni yao kwa uhuru na kuhakikisha kuwa mchakato unaendeshwa kwa uhuru na haki.

Awali Mwenyekiti wa Misa Tanzania, Mohamed Tibanyendere, aliielezea Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Dunia, kuwa ni ya kutafakari na kujieleza kama haki ya msingi ya binadamu na kichocheo cha kuweza kupata haki nyingine za msingi.

Chanzo: Tanzania Daima

Posted by Bigie on 1:27 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.