JE, NI SAHIHI KWA WABUNGE KUJIONGEZEA POSHO PEKE YAO KWA KISINGIZIO CHA UGUMU WA MAISHA?


Hivi karibuni kumeibuka mjadala juu ya ongezeko la posho za wabunge kwa karibu ya asilimia 200, kutoka sh. 70,000 hadi sh. 200,000.

Mtandao huu umefuatilia kwa makini suala hilo la nyongeza ya posho hiyo ya wabunge kama lilivyoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari na baadae kutolewa maelezo na Katibu wa Bunge Dk. Thomas Kashilila na Spika wa Bunge Anne Makinda.


Kwa kuzingatia maoni yao pamoja na tamko la chama cha Mapinduzi ,CCM,lililotolewa jana na katibu wa halmashauri kuu ya Taifa,itikadi na uenezi,mtandao huu umeona ni bora ukumbushe mambo yafuatayo:

Ugumu wa  maisha au kupanda kwa gharama za maisha, ni suala linalowakabili wananchi wote wa Tanzania.


Tunawaomba waheshimiwa Wabunge na Serikali yetu wakumbuke kuwa  mkoa wa Dodoma  una wakazi  wengi,tena kutoka sehemu mbali mbali za nchi.

Hii ni pamoja na WANAFUNZI WA VYUO VIKUU,ambao wengi wao wanatoka mikoani,WAFANYAKAZI WA SERIKALI NA TAASISI BINAFSI,pamoja na WANANCHI WENYEWE WA MKOA WA DODOMA.Kwa hali kama hii,ingekuwa ni busara zaidi   kama jambo hili  lingelenga  kutatua ugumu huo wa maisha kwa makundi yote katika jamii na si kwa makundi machache (WENYE UWEZO) ndani ya jamii.
 
 Kwa kuongeza kiwango hicho cha posho kwa wabunge ni kuongeza tofauti ya mapato kati ya wenye nacho na wasionacho katika jamii yetu hasa kwa kuegemea baadhi ya makundi.


Hapa nina maanisha kuwa,kama ni kweli maisha ya Dodoma  yamepanda,serikali ilitakiwa kuchukua hatua za makusudi za kuwanusuru  wananchi wa mkoa huo na sehemu mbalimbali.JE SERIKALI INADHANI WANANCHI WA DODOMA,TENA WENYE KIPATO CHA CHINI,WANAISHIJE?  NI ASILIMIA NGAPI YA WAKAZI WA DODOMA NI WAAJIRIWA?
 
 Mwanzoni mwa mwaka tulishuhudia MIGOMO isiyokuwa na ukomo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma ambao madai yao yalikuwa ni pesa za kujikimu,pesa za mafunzo ya vitendo (industrial training) na pesa za vitivo maalum (special fulculty requirements).Hatujui undani wa maamuzi yaliyochukuliwa ,lakini taarifa tulizo nazo mpaka sasa ni kuwa walio dai special fulculty requirements hawakupewa  na walioomba kwenda  field hawakuenda.JE,WAHESHIMIWA WALISHIRIKI VIPI KUWASAIDIA VIJANA HAWA NA HALI WAKIWA WANAJUA HALI HALISI YA MAISHA YA DODOMA KUWA NI MAGUMU?


 Bunge ni chombo muhimu cha kutunga sheria, kinapoibuka na madai kwamba sababu za kuongezeka kwa posho hizo kunatokana na kupanda kwa gharama za maisha mjini Dodoma kama alivyoainisha Spika wa Bunge, ndiyo inasababisha hofu na mashaka miongoni mwa Watanzania.

 Swali kubwa ambalo  Watanzania wengi wanajiuliza ni je, maisha yanapanda Dodoma peke yake na kwa wabunge tu?

 Mtandao huu unatoa ombi kwa waheshimiwa wabunge wetu na mamlaka zingine zinazohusika na swala hili, kulitafakari upya jambo hili.
 
Tunaamini busara itatumika kulitatua jambo hili, kwani kuendelea nalo kunaweza kutafisiriwa ni kuwasaliti watendaji katika sekta nyingine wakiwemo Walimu, askari, Madaktari na wengineo.

 
Ni muhimu ifahamike kuwa kuongoza ni kuonesha njia, hivyo si sahihi kwa wabunge kuonesha njia kwa kujiongezea posho peke yao kwa kisingizio cha ugumu wa maisha huku wakiwaacha wananchi ambao ndiyo wanaowawakilisha bungeni wakikosa nafasi ya kupunguza ugumu wa maisha unaowakabili, jambo ambalo ni hatari.

 

Posted by Bigie on 7:36 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.