WEMA, WOLPER NA UWOYA WAPATANA....

MASTAA Wema Sepetu na Irene Uwoya ambao walitangaza bifu dhidi ya staa mwenzao  Jacqueline Wolper Massawe wamepatana.
 
 Husna Posh ‘Dotnata’ ndiye aliyefanikisha mastaa hao kumaliza bifu katika kikao kilichochukua nafasi hadi usiku wa manane.

Tukio la upatanishi, lilifanyika kwenye sherehe ya kuzaliwa ya Uwoya, iliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye bustani iliyopo Tangi Bovu, Mbezi Beach, Dar es Salaam.
Kikao cha usuluhishi kilikuwa sapraizi, kwani waalikwa wote, walifika eneo hilo kwa ajili ya kufurahi na Uwoya na kumpongeza kwa kutimiza miaka kadhaa ya kuzaliwa kwake .

Sherehe ilianza saa 6:00 usiku kwa kufungua shampeni kisha ikakatwa ndafu, iliyoliwa na kila aliyehudhuria.
MC wa shughuli hiyo, Steve Nyerere, alitangaza tukio la Uwoya kumlisha ndafu Wolper, jambo ambalo liliwashtua wote waliohudhuria.

Baada ya tangazo hilo, Wolper alisogea mbele, akalishwa ndafu na Uwoya kisha mastaa hao, wakatazamana, wakatabasamu mwisho wakakumbatiana.
Hali ya Uwoya na Wolper kukumbatiana, iliamsha shamrashamra kemkem kwa ukumbi mzima kulipuka kwa mayowe.
Kutokana na mafanikio ya tukio hilo, Dotnata aliwaita Wolper na Wema ili nao wamalize tofauti zao, jambo ambalo lilizua utata.
Wema aliweka ngumu kumaliza bifu lake na Wolper kwa maelezo kuwa anahitaji muda zaidi kutafakari na kufanya uamuzi.

Hata hivyo, busara za Dotnata, zilimtuliza Wema ambaye naye alifungua kifundo chake moyoni na kukubali kumaliza tofauti zake na Wema.

Baadaye ukumbi mzima ulitaarifiwa kuhusu suluhu ya Wema na Wolper kisha wote wakashuhudia mastaa hao wakikumbatiana.

Katika kuonesha kwamba kweli wameamua kusameheana na kuwa kitu kimoja, kwa nyakati tofauti wasanii hao walikumbatiana na kupeana mabusu, jambo lililoamsha shangwe zaidi ukumbini humo.


Habari zinaeleza kuwa Wolper na Uwoya ilikuwa rahisi kupata suluhu kwa sababu waliketishwa usiku wa manane, siku moja kabla ya sherehe hiyo.

Ilielezwa kuwa Uwoya alipopeleka mwaliko wa sherehe yake kwenye Klabu ya Bongo Movie, alikutana na Dotnata ambaye alitoa rai ya kuwepo kwa suluhu na mwenzake Wolper.


Inaelezwa kuwa kutokana na wazo hilo kuafikiwa na kila upande, Dotnata aliwaketisha Wolper na Uwoya kisha wakamaliza tofauti zao, hivyo wao waliingia kwenye sherehe wakiwa hawana tofauti.


Wema alisema baada ya kupatanishwa kuwa yeye hana bifu na anapenda kumaliza mwaka vizuri.

“Napenda mwaka ujao niuanze vizuri, sitaki tena mambo hayo kwa kuwa jina langu lina maana ya upendo na furaha na siyo kuwekeana vinyongo,” alisema Wema.


Uwoya alipopata nafasi ya kuzungumza, alisema anachosisitiza ni upendo.

“Mengi ameongea Wema mimi kwangu  one love sina tatizo na mtu yeyote yule,” alisema Uwoya.

Wolper yeye alimshukuru Wema kwa kuzungumza maneno mazuri kutoka moyoni na siyo ya udanganyifu.


Alisema: “Wema ameongea kitu ambacho amekitoa moyoni mwake na si cha kudanganya, nimefurahi sana kumaliza hili bifu na Mungu asaidie tuendelee hivi.”


Maneno ya mastaa hao, yalifuatiwa na makofi, miruzi na aina mbalimbali za maneno ya kuwashangilia kutoka kwa wahudhuriaji wengine.

Posted by Bigie on 6:11 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.