DIAMOND AZOMEWA AKIWA JUKWAANI NCHINI UINGEREZA.....ULIMBUKENI WAMPONZA
JAMII 12:17 AM
Ushamba wa mapenzi alionao Naseeb Abdul ‘DIAMOND’ , umekwenda hatua mbaya zaidi, alichokifanya Uingereza hivi karibuni, kimeshusha thamani yake hadi sifuri.
Akiwa Uingereza, Diamond aliropoka maneno ambayo siyo tu kwamba yalimfanya azomewe jukwaani, bali pia yaliwadhalilisha warembo wenye majina makubwa Bongo, Wema Sepetu na Jokate Mwegelo.
Inadaiwa kuwa Diamond akiwa katikati ya shoo kwenye ukumbi mmoja jijini London, alisimamisha muziki halafu akawaambia mashabiki waliohudhuria, wamchagulie mpenzi wa maisha yake, kati ya Wema na Jokate.
Madai yanaanikwa kwamba kitendo hicho, kiliwakera mashabiki ambao walilipuka na kumzomea, huku wengi wakimponda kwa kumwita limbukeni wa mapenzi, anayetumia umaarufu wake vibaya kuwachezea warembo.
Mashabiki mbalimbali wametoa maoni kwamba kauli ya Diamond kuwa hamjui mpenzi wake kati ya Wema na Jokate, inatosha kuchangamsha ubongo wa warembo hao ili wajivue gamba mapema na endapo wataendelea naye, basi nao wataonekana ni limbukeni.
Kwa upande mwingine, kauli ya Diamond imeibua mjadala mkubwa kwenye mitandao mbalimbali, huku kipande cha video, kinachomuonesha ‘dogo huyo mpenda sifa’ akibwabwaja jukwaani kikisambazwa kwa fujo kupitia intaneti na kuchangiwa maoni ya kufuru.
Kuweka pamoja maelfu ya maoni yaliyotumwa, wachangiaji wamemwita Diamond ni mchafuzi wa watoto wa kike, hana mapenzi ya kweli, gusa unate, mkuki popote na mengineyo ambayo hayana tafsiri nzuri kwa ‘dogo huyo’ aliyekulia Tandale, Dar.
Promota mmoja wa Uingereza , alimwambia mpekuzi wetu kuwa alipanga kumpa shoo tatu Diamond katika majiji ya Leads, Swansea na Leiceste lakini aliahirisha baada ya kuona amewachafua mashabiki na hakubaliki tena.
Oktoba 2, 2011, Diamond kwa utashi wake, bila kulazimishwa, alijishaua kumvisha pete ya uchumba, Wema ambaye ni staa wa filamu mwenye taji la Miss Tanzania 2006-07.
Diamond, alimvalisha pete Wema na kuahidi kufunga naye ndoa katika tukio kubwa la shoo ya siku yake ya kuzaliwa, iliyochukua nafasi ndani ya New Maisha Club, Masaki, Dar es Salaam.
Wakati Diamond anautangazia ulimwengu kuwa Wema ndiye mke wake mtarajiwa, Jokate ambaye ni Miss Tanzania namba mbili 2006-07, alikuwepo.
Kwa mujibu wa watoa maoni, tusi kwa Wema ni kuwa kumbe alivishwa pete kanyaboya isiyo na mapenzi ya moyoni, kama ni mpira, basi alipangwa kikosi cha kwanza kwa ajili ya kumshikia nafasi mchezaji mwenye namba yake.
Jokate anaendelea kusisitiza kwamba hajawahi kukwea kitandani na Diamond, isipokuwa yupo karibu na ‘bwa mdogo’ huyo mpenda wamama kwa ajili ya kazi tu.
Wema anadai anao ushahidi kuwa Jokate kaanguka dhambini, wakati huo huo Diamond naye anajichetua ili aonekane kidume cha mbegu kwa kuomba mashabiki wamchagulie anayefaa.
Kabla ya tukio hilo, Jokate ni mrembo maarufu ambaye heshima yake kwenye jamii ilikuwa juu kutokana na jinsi alivyoendesha mtindo wa maisha yake.
Tathmini inaonesha kuwa tangu alivyoanza kuhusishwa kutoka kimapenzi na Diamond, heshima yake imepungua, huku watu wengi wanaompenda wakisema kwamba mrembo huyo ameingia chaka.
Kitendo cha Diamond kumuweka mezani na Wema, kisha kumchezesha bahati nasibu kama atashinda au la, kimezidi kuporomosha heshima ya Jokate.