MSANII AFIKISHWA MAHAKAMANI KWA KOSA LA "KUFANYA BIASHARA HARAMU YA UKAHABA"


MREMBO mwenye mvuto wa kimahaba, Evonia William, juzi Jumatano alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, Dar es Salaam kwa kosa la kufanya biashara haramu ya ukahaba.

Awali, mrembo huyo aliwahi kutupa karata yake kwenye ulingo wa filamu za Kibongo kwa kushiriki sinema tatu (scene chache) lakini "hakuweza kuwika".

Mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo, Richard Magodi alimsomea Evonia shitaka lake mbele ya Hakimu Mkazi, William Mutaki na kumwambia kuwa kosa alilokutwa nalo ni la kukaa eneo la wazi na kufanya ukahaba.

Mwendesha mashitaka huyo aliiambia mahakama kuwa, Januari 17, mwaka huu, saa 2:00 usiku, mshitakiwa huyo alinaswa eneo la Buguruni karibu na Baa ya Kimboka akifanya kosa hilo.

Evonia alikana shitaka hilo na kumwambia hakimu kuwa alikamatwa eneo hilo kwa kosa la kupigana na changudoa aliyekuwa akijiuza, lakini yeye hakuwa na lengo la kufanya biashara hiyo.

Baada ya mrembo huyo kukana shitaka, mheshimiwa hakimu alimwambia kuwa, dhamana ipo wazi, lakini alikosa mdhamini hivyo alipelekwa rumande.

Mshitakiwa huyo akiwa mahakamani hapo, alimlalamikia baba yake mzazi aliyemtaja kwa jina la William Molo, kuwa ndiye chanzo cha yeye kuteseka na kuzurura hovyo.
Alisema, baba yake pamoja na uwezo wake mkubwa kifedha, alikataa kumsomesha, ndiyo sababu anahangaika mitaani.

“Kama baba yangu angenisomesha, nisingekuwa hivi. Ningekuwa na maisha mazuri kama mabinti wengine. Nimembembeleza sana anisomeshe lakini hataki. Akitokea msamaria yeyote kunisomesha au hata kufanya kazi za ndani, nipo tayari kutulia,” alisema msichana huyo huku akiangua kilio.

Kesi hiyo itatajwa tena Januari 31, mwaka huu mahakamani hapo huku Evonia akiendelea kula msoto rumande.

Posted by Bigie on 6:32 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.