MTOTO WA MIAKA 12 AUGUZA WADOGO ZAKE USIKU KUCHA...BABA YAKE ALIFARIKI NA MAMA YAKE NI MGONJWA MAHUTUTI


Hakuna mtu anayejutia kuzaliwa, wengi wamekuwa wakifurahia huku wakitegemea  maisha mazuri lakini  kwa mtoto Mustapha Ali (12) (pichani)  imekuwa ni tofauti.

Mtoto huyo ambaye ni mkazi wa Mtoni Mtongani Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam anayesoma darasa la sita ni wa kwanza kuzaliwa katika familia yao na kwa sasa anakabiliwa na mzigo wa kuwauguza wadogo zake  mapacha, Swaumu na Ramadhani  wenye umri wa miezi nane.

Watoto hao wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na mtoto Mustapha  ameahidi  kuwa atawauguza wadogo zake hadi wapone.

Mustapha, amebaki na jukumu  hilo  baada ya mama yao aliyekuwa akiwauguza wadogo zake kuugua na kwa sasa yupo mahututi, wakati baba yao alishafariki dunia.

Mtoto huyo anayewauguza wadogo zake katika wadi ya watoto, Makuti B, wiki iliyopita alizungumza na mwandishi wetu na alikuwa na haya ya kusema:

“Maisha yamebadilika ghafla na kuwa mabaya hasa baada ya baba kufariki dunia nikiwa na miaka minne.

“Baba alikuwa akijishughulisha na kazi  za vibarua na mama kazi yake ni kuuza mboga mitaani. Kazi hizo zilituwezesha kupata mahitaji ya kila siku na kulipa kodi  ya nyumba.

“Mwaka 2007 baba alifariki dunia tukabaki na mama ambaye aliendelea na shughuli na biashara yake. Alikuwa akifanya  kazi hiyo bila kupumzika, mzigo wa maisha ulimlemea, nikakatisha kwenda shule nikawa nabaki nyumbani kumsaidia.

“Kufuatia kifo cha baba, muda mwingi mama alionekana mnyonge na aliyejaa mawazo mengi  kutokana na kazi ngumu, wakati  mwingine alikuwa akitokwa machozi.

“Mwaka juzi mama alipigiwa simu na kuambiwa kuwa bibi anaumwa huko Kigoma na hana mtu wa kumuuguza, ilimbidi aende hata hivyo, hakupona alifia mikononi mwake na baada ya mazishi alirejea Dar na kukuta kodi ya nyumba imeisha.

“Licha ya kusumbuliwa na maradhi, aliendelea na biashara yake kwani hakukuwa na mtu wa kumtegemea, alikuwa akiniambia bila kwenda kwenye shughuli hizo, tungekufa na njaa.

“Mama alianza kuchanganyikiwa kimawazo pale Swaumu  na Ramadhan walipoanza kuumwa, alikuwa haendi  kuuza mboga. “Maisha yalikuwa ni magumu, tulikuwa tukisaidiwa chakula na wasamaria wema wakati mwingne tulishindia uji.

“Hali za kiafya za wadogo zangu hawa (akiwaonyesha kwa mwandishi), zilianza kuwa mbaya na mama akawa hana fedha za kuwapeleka hospitali.

“Novemba 11, mwaka jana aliamua kuwaleta hapa Muhimbili akiwa hana fedha.

“Alimweleza daktari matatizo  yaliyokuwa yakitukabili kiafya na kiuchumi ndipo wadogo zangu walipokelewa na kuanzishiwa matibabu.

“Wadogo zangu walilazwa hapa mimi nilirudi nyumbani  na majirani wakawa wanapika  huko kwao na kunipa mimi nikawa namletea mama hapa hospitali.

“Niliendelea na zoezi hilo kila siku, nikashindwa kwenda shule lakini niliamini kuwa ipo siku wadogo  zangu wangepona nami ningeendelea na masomo.

“Hali ya mama ilizidi kuwa mbaya  kuliko hata wadogo zangu akawa anapatiwa, afya yake ilizidi kudhoofu daktari akashauri apewe dawa za kutumia akiwa  nyumbani, akarudi nyumbani.

“Hakukuwa na ndugu wa kubaki na wadogo zangu hospitalini, hivyo nikaamua niwauguze, nimekuwa nikilala nao kitanda kimoja.

“Kinachonihuzunisha ni kwamba, sielewi mama anaendeleaje na jambo lingine linaloniumiza kichwa ni kwamba kodi ya nyumba  imekwisha mwezi uliopita, sijui tutapata wapi fedha katika hali hii!.

“Mama hana nguvu tena ya kujishughulisha, hatuna ndugu wa kumwangalia ningekuwa na uwezo  ningempeleka kwetu Kigoma.

 “Nina mawazo  mengi kwani hata  kama akipatikana mtu wa kubaki na wadogo zangu hapa hospitalini nitaendaje shule? Sina viatu, nguo  na madaftari nitaishi wapi na nitakula nini?  

“Hata wadogo zangu hawana nguo na mahitaji  mengine muhimu.Tunaomba mtu yeyote mwenye huruma atusaidie kutulipia kodi ya nyumba, chakula na nguo ili tuweze kujinusuru na hali ngumu inayotukabili,” alisema  mtoto Mustapha  huku akitokwa machozi.

 Mtu yeyote aliyeguswa na kilio cha mtoto huyo amtembelee Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Kama una uwezo, itapendeza  ukimsaidia, kwani anahitaji msaada wa hali na mali.

Posted by Bigie on 3:05 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.