DEWJI ASHAURI WABUNGE WA DAR WAACHE KUJITAFUTIA UMAARUFU KUPITIA MGONGO WA "WAZIRI MAGUFULI"....ADAI KUWA "MBONA WAO WAMEJIPANDISHIA POSHO NA WAKO KIMYA?"

SAKATA la nauli mpya ya kivuko cha mv Magogoni limechukua sura mpya baada ya mfanyabiashara maarufu nchini, Azim Dewji (pichani) kuwajia juu wabunge wa mkoa wa Dar es Salaam, akiwataka kuacha kumshambuliaji Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli na badala yake wahangaike kutatua matatizo ya msingi ya wananchi katika majimbo yao.

Wabunge hao wakiongozwa na Mbunge wa Temeke, Abbas Mtemvu, juzi walizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa, kitendo cha Magufuli kutangaza ongezeko nauli ya kivuko hicho kwa asilimia 100 bila kushirikisha wananchi, hakina tofauti na udikteta.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Dewji alisema wabunge hawapaswi kupinga kila jambo kwa lengo la kujijenga kisiasa na kusisitiza kuwa Magufuli ana hoja za msingi, hivyo aungwe mkono kwa lengo la kuboresha usafiri wa majini katika eneo hilo na jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi.

“Jamani, ongezeko la sh 100 linaleta chokochoko za nini? Leo hii hata ombaomba ukimpa sh 100 anaweza kukurushia usoni. Wanalalamikia shilingi 100 wakati wao walijiongezea posho za laki mbili hawakuona ubaya wowote…nadhani wabunge wa Dar es Salaam walipaswa kumuunga mkono Magufuli ili kivuko kijiendeshe na kutoa huduma bora na za kudumu, badala ya kila kitu kutegemea kitoke serikali kuu.

Hivi kila kitu kikitoka serikalini, fedha nyingine za maendeleo zitatoka wapi, kama si kuishia kuziba mapungufu kama yanayojitokeza kwenye vivuko vyetu vinapoharibika?” alihoji na kusema kama fedha zisipokusanywa, na vivuko vikapata hitilafu na kushindwa kutoa huduma, watakuwa wa kwanza kudai serikali imewasahau wana-Kigamboni.

Alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa, pesa zitakazokusanywa kutokana na nauli mpya zitachangia pia kulipa ongezeko la posho za wabunge, kwa kuwa ni fedha za wananchi na wabunge wanalipwa kutokana na fedha za walipakodi.

“Daladala zinapanda kila kukicha, hatusikii kelele, sasa angalia, Waziri Magufuli amesema kwa mara ya mwisho bei ya kuvuka kwenda na kutoka Kigamboni ilipandishwa miaka 14 iliyopita, hawaoni kuwa bei hiyo imepitwa sana na wakati?

Na mbaya zaidi nasikia wanataka wakabidhiwe kazi ya kuendesha kivuko, mbona baadhi yao majimbaoni mwao tayari mambo yameanza kuwa ya shingo, hayaendi kabisa. Nadhani wangejikita katika kustawisha majimbo kwanza, wakishamaliza ndipo waombe kusaidia kazi za wengine, huu kwao si wakati sahihi wa kutoa msaada,” alisema na kuhoji kwanini wasizungumze kumaliza kero nyingine za jijini, ikiwemo foleni.

Kauli ya Dewji, aliyekuwa anazungumza kwa hisia kauli, huku akisisitiza wabunge kuacha kudandia mambo kwa lengo la kupata umaarufu aliouita wenye kuwajenga zaidi kisiasa badala ya kuwanufaisha wananchi wa kawaida, imeibuka huku kukiwa na mjadala mkali tangu kupandishwa kwa nauli za kivuko cha Magogoni.

Jumapili iliyopita, Dk. Magufuli alitangaza kuwa, serikali imeamua kupandisha nauli hiyo kutoka kati ya sh 50 na Sh 100 hadi sh 200 kwa safari moja ya kivuko hicho, kutokana na gharama za uendeshaji kuwa juu. Alisema nauli iliyokuwapo ni ya tangu mwaka 1997, huku nauli ya vivuko vingine zaidi ya 30 nchini imekuwa ikipanda mara kwa mara.

Magufuli alisema kivuko cha Magogoni kimekuwa kikitoza nauli za chini ikilinganishwa na Chato, kinachotoza sh 300, Pangani Sh 200, Kisorya Sh 300, Lugolora Sh 500, Nyakarilo Sh 300, Chato-Bukombo Sh 2,000, Kirambo sh 500 na Utete Sh 300, huku wanafunzi wakisafiri bure.

Sambamba na upandishaji nauli kwa watu, pia nauli ya magari imepanda ambapo madogo yatatozwa Sh 800 na Sh 1,500, pick up sh 1,000 na Sh 2,000 na yale ya kuanzia tani tatu na nusu Sh 5,000 hadi Sh 7,500.
 

Posted by Bigie on 3:33 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.