Watu Wawili Watiwa Mbaroni kwa kukutwa na Meno ya Tembo
news 6:07 PM
WATU wawili wametiwa mbaroni na Polisi mjini Mpanda kwa kukutwa na meno ya tembo waliokamatwa yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 157 ndani ya basi la Adventure.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Katavi, Dhahiri Kidavashari alisema vipande
vilivyokamatwa ni 22 vyenye uzito wa kilo 46.3 sawa na tembo saba
waliouawa.
Aliwataja
watuhumiwa hao kuwa ni Justine Baruti (39) mkazi wa kijiji cha Ivungwe –
Katumba katika Kambi ya Wakimbizi kutoka nchi jirani ya Burundi iliyoko
wilayani Mlele mkoani Katavi.
Mtuhumiwa
mwingine ni Boniface Hoza (40) mkazi wa kijiji cha Kalela wilayani
Kasulu mkoani Kigoma. Akisimulia mkasa huo Kidavashari alisema Desemba
24 mwaka huu saa 12:00 alfajiri, askari polisi wakiwa doria katika Kituo
Kikuu cha mabasi kilichopo eneo la Mji wa Zamani mjini Mpanda
walimtilia shaka mmoja wa watuhumiwa Jusitine Baruti ambaye akiwa na
kifurushi tayari kupanda basi la abiria la Kampuni la Adventure.
Inadaiwa
kuwa basi hilo la Adventure lenye nambari za usajili T992 DDT lilikuwa
limepaki katika Kituo Kikuu cha mabasi mjini Mpanda tayari kwa safari ya
kuelekea mjini Kigoma.
“Mtuhumiwa
huyu alijaribu kuwatoroka askari hao wa doria lakini walifanikiwa
kumkamata na kumweka chini ya ulinzi. Walipopekua mabegi mawili
aliyokuwa nayo walikuta vipande 15 vya meno ya tembo vyenye uzito wa
kilo 33. Vipande hivi kwa pamoja vikiwa na thamani ya Sh 90,000,000 ni
sawa na tembo wanne waliouawa,” alieleza.
Kwa mujibu wa Kamanda Kidavashari, basi hilo la abiria liliamriwa kwenda Kituo Kikuu cha Polisi kilichopo mjini Mpanda ambapo baada ya upekuzi wa kina, mtuhumiwa mwingine Boniface Hoza alikamatwa akiwa ameficha begi kwenye uvungu wa kiti alichokalia chenye namba K3.