CCM YATAZAMIWA KUWASHUKURU WANANCHI KWA USHINDI WA UBUNGE NA VITI 17 KATI YA 22 VYA UDIWANI
JAMII 5:03 PM
Chama Cha Mapinduzi-CCM-Mkoa wa Dar es Salaam kesho kinafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika Viwanja vya Bakharesa, Manzese ili kuwashukuru wananchi wa Igunga kwa kukipa ridhaa tena Chama hicho kuendelea kuongoza Jimbo hilo.
Kufuatia mkutano huo Wana-CCM kutoka maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam wametakiwa kujitokea kwa wingi katika mkutano huo ambao pia utahudhuriwa na Mbunge Mteule wa Jimbo la Igunga Dokta PETER KAFUMU.
Katibu wa Itikadi na Uenezi CCM Mkoa wa Dar es Salaam JUMA SIMBA katika mkutano na waandishi wa habari amesema wameamua kufanya mkutano huo ili kuwashukuru pia wananchi katika Kata 17 kati ya 22 zilizofanya Uchaguzi Mdogo wa Udiwani ambao CCM ilishinda kwa kishindo.
Kabla ya kuanza mkutano huo wanatarajia kuwapokea viongozi wa Sekretarieti ambao waliongoza Kampeni katika Jimbo hilo la Igunga na kuwezesha kupatikana kwa ushindi huo.
Ushindi uliopatikana katika Jimbo la Igunga amesisitiza kuwa umeonesha kwamba bado wananchi wana imani kubwa na Chama Cha Mapinduzi-CCM.
Mgeni rasmi katika mkutano huo anatarajiwa kuwa ni Katibu wa NEC wa CCM Uchumi na Fedha Mheshimiwa MWIGULU NCHEMBA.






