SERIKALI YAREJESHA TENA MITIHANI YA KIDATO CHA PILI

   WAKATI jana wanafunzi wa kidato cha nne wakianza mitihani yao ya kuhitimu elimu ya sekondari, hatimaye serikali imerejesha tena mtihani wa kidato cha pili.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mullugo, alitangaza urejeshaji huo mbele ya wananchi wa jimbo lake la Songwe lililoko wilayani Chunya, mkoani Mbeya.

Mullugo alisema kuwa ili kupunguza kushuka viwango vya ufaulu hapa nchini hasa kwa kidato cha nne, serikali imeamua kurejesha mtihani huo wa kidato cha pili na wanafunzi wote watatakiwa kufikisha wastani wa alama 25 ili kuendelea na masomo ya kidato cha tatu.
“Kuanzia mwaka huu hakuna mwanafunzi atakayeruhusiwa kuendelea na kidadto cha tatu bila kufanya mtihani wa kidato cha pili na kufikisha wastani wa 25,” alisema Mullugo.
Wakati huohuo, Naibu Waziri huyo wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi alitoa msaada wa zaidi ya shilingi mil. 277 kwa ajili ya kusaidia elimu jimboni humo.

Msaada huo aliutoa mwishoni mwa wiki katika mkutano wa hadhara uliokutanisha wananchi wa jimbo hilo eneo la Mkwajuni wilayani humo ambapo walimu wakuu, walimu wa masomo ya sayansi na waratibu wa elimu wa kata wote walipatiwa komyuta za mikononi (laptops) 40 ambazo kiasi chake ni shilingi mil. 48.

Mbali na kompyuta hizo, alitoa vitabu vya ziada na kiada 6,000 kwa shule za sekondari zilizo katika jimbo hilo; madawati 80 ya kisasa yenye thamani ya shilingi 40,000 kwa kila moja na fedha taslimu shilingi milioni 10 kwa shule saba za sekondari za jimbo hilo; huku kituo cha polisi cha Mkwajuni kikipatiwa karatasi (rimu 10) kwa ajili ya kuandikia kesi.
Aidha Mullugo alisema kuwa kuanzia Novemba visima 17 vya maji vitachimbwa katika vijiji 15 vilivyomo ndani ya jimbo hilo ambavyo alisema alipata msaada wake kutoka  Sabodo Foundation.

“Ndugu zangu, kila kitu ambacho nilikiahidi kwenye kampeni licha ya kupita bila kupingwa na kila nitakachoahidi kuanzia sasa mradi nimetamka kwa mdomo wangu lazima nitekeleze kwa sababu mimi naitwa Mullugo Ahadi Umepata,’’ alisema Naibu Waziri huyo huku akishangiliwa na umati mkubwa uliofika kumsikiliza.
Akishukuru kwa misaada hiyo, mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari Maweni, Annety Robert, alisema kuwa haijawahi kutokea mbunge kuwajali walimu kama alivyofanya mbunge huyo.

“Kwanza hatuamini maana haijawahi kutokea walimu kuwa karibu na wabunge kama Mullugo na hii ni historia haiji kufutika maana hata ambao hatukujua kutumia kompyuta tunaenda kujifunza na hivi vitabu amatusaidia sana,’’ alisema Mwalimu Annety Robert.
Alitoa Shilingi 500,000 papo hapo kwa ajili ya kuwaendeleza wanawake wa eneo la Majengo fedha ambazo zilipokelewa na Malikiana Jonas na hundi ya shilingi milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa soko la wananchi wa Mwambani ambayo ilipokelewa na Erick Mwashambwa.

Mbali na zawadi hizo na nyingine nyingi, alitoa ahadi ya kuwalipia karo ya kidato cha tano wanafunzi wote wa kidato cha nne watakaofaulu kwa daraja la kwanza hadi la tatu kutoka katika shule za sekondari za kata zilizoko jimboni kwake huku akiahidi kutoa shilingi milioni moja kwa shule za msingi zitakazoshika nafasi ya kwanza hadi tano katika kufaulisha.
Mullugo aliweka wazi kuwa jumla ya gharama za misaada hiyo aliyoitoa ni shilingi 277, 200,000 na ataendelea kulikomboa jimbo hilo katika masuala yote ya maendeleo.

Aliendelea kuahidi kuwa kuanzia mwaka 2012 mbali na kuhamasisha na kuchangia maendeleo ya jimbo hilo alisema kuwa ataimarisha chama chake cha CCM kwa kuanza kuwalipa shilingi 10,000 kila mmoja makatibu na wenyeviti wa chama chake.

Posted by Bigie on 10:43 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.