TUCTA:: SHIRIKISHO LA WAFANYAKAZI LATAKA KIMA CHA CHINI CHA MSHAHARA KIWE Tsh. 500,000

    SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), linafanya utafiti kubaini chanzo cha hali ngumu ya maisha inayowakabili wafanyakazi kwa lengo la kudai nyongeza mpya ya mishahara.
Utafiti huo utasaidia kudai nyongeza mpya ya kima cha chini cha mishahara kutoka sh 310,000 walichodai mwaka jana hadi kufikia sh 500,000.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo, Nicholas Mgaya, alisema kuna ulazima wa kufanya hivyo kutokana na hali ya maisha kuzidi kuwa ngumu.
Alisema utafiti huo, utaelekezwa kwenye vipaumbele vitatu ambavyo ndivyo vinavyogusa maisha ya mfanyakazi katika maisha ya kila siku.
Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na pato la taifa, ongezeko la bei za bidhaa na kuporomoka kwa kasi kwa thamani ya shilingi.

Alisema baada ya kukamilika kwa utafiti huo, watatangaza kiwango kipya cha mshahara wa mfanyakazi.
“Sisi tunataka mshahara ambao utamuwezesha mfanyakazi aishi bila matatizo, hivyo tunatarajia kiwango cha chini kiongezwe hadi kufikia sh 500,000 toka kiasi cha sh 315,000 tulichokuwa tukikipigania kiongezwe mwaka jana,” alisema Mgaya.

Aidha Mgaya alisema shirikisho hilo limejiwekea mikakati ya miaka mitano yenye lengo la kuongeza wanachama ukilinganisha na wanachama 600,000 waliopo sasa.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Hezbron Kaaya, aliwataka wanachama kutambuwa kuwa hawako pale kutekeleza matakwa ya mtu binafsi.

Alisema huu ni wakati wa kuliletea shirikisho hilo mabadiliko ambayo yataweza kuwajengea imani kwani wengi wao wameonekana kupoteza imani kwa shirikisho hilo.

Posted by Bigie on 10:59 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.