DEREVA WA AJALI ILIYOUA WATU 14 MKOANI MBEYA AFIKISHWA MAHAKAMANI NA KUSOMEWA MASHTAKA 44 AKIWA AMELAZWA
JAMII 11:06 PM
DEREVA Moses Kapusi (55), aliyekuwa akiendesha gari aina ya Fuso lililosababisha ajali na kuua watu 14 hivi karibuni eneo la Msangamwelu, wilaya ya Mbeya Vijijini wakati likitokea Mbuyuni, wilayani Chunya, jana amefikishwa kortini na alisomewa mashtaka 44.
Mashtaka hayo yaliendeshwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, ambako mtuhumiwa amelazwa akipatiwa matibabu tangu kutokea kwa ajali hiyo.
Akisoma mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mbeya, Michael Mteite, wakili wa serikali, Griffin Mwakapeje, alisema mshtakiwa alisababisha ajali akiwa na gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T 532 AJF, katika barabara kuu itokayo Mbeya kwenda Chunya eneo la Msangamwelu ikitokea mnadani Mbuyuni.
Kapusi, alisomewa mashtaka hayo akiwa chini ya ulinzi wa polisi kwenye wodi namba moja ya hospitalini hapo na kuyakana yote.
Mahakama iliahirisha kesi hiyo baada ya kumpatia dhamana mshtakiwa ili aendelee na matibabu chini ya ulinzi huku upande wa mashtaka ukiomba muda zaidi kwa ajili ya upelelezi. Kesi hiyo atatajwa tena Oktoba 17.






