HAMAD RASHID MOHAMMED AGOMA KUHOJIWA NA KAMATI YA NIDHAM NA MAADILI YA CUF
JAMII 10:20 PM
MBUNGE  wa Wawi, Hamad Rashid Mohammed (CUF) ameigomea Kamati ya Nidhamu na  Maadili ya chama hicho kumhoji na kumjadili kuhusu tuhuma zinazomkabili  za kukiuka Katiba, akidai hana imani na wajumbe wake. 
Pia ameigomea kwa kudai kuwa tayari alishafahamu kwamba Kamati hiyo ilikuwa na maamuzi 
ya  kumfukuza uanachama, kupitia barua pepe aliyoinasa ikitoka kwa Katibu  wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad kwenda kwa Mwenyekiti Profesa  Ibrahim Lipumba. 
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mh Hamad ambaye pia ni Mjumbe wa 
Baraza  Kuu la CUF alisema alipokea barua ya kuitwa kuhojiwa kwa tuhuma za  kwenda kinyume cha Katiba ya CUF, Desemba 23, mwaka huu na kikao hicho  kilifanyika rasmi jana. 
Alisema  baada ya kuhudhuria kikao hicho, alilazimika kukigomea kuendelea  kumjadili kutokana na kutokuwakubali wajumbe watano kati ya wanane  akiwemo Mwenyekiti wa Kamati 
hiyo ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CUF, Machano Khamis Ali na Katibu wake Hamis Hassan. 
Alisema viongozi hao wawili amewakataa kutokana na ushiriki wao katika kumtuhumu. 
Alisema hana imani na Machano baada ya kiongozi huyo kuahidi kumshughulikia katika 
kikao kilichofanyika hivi karibuni bila ya kumpa nafasi ya kusikiliza upande wake. 
Aidha, kwa upande wa Hassan, Hamad alisema Katibu huyo alimtuhumu kwa kumuandikia 
Lipumba barua na kumtuhumu kuwa (yeye) ni chachu ya kuchafuka kwa hali ya kisiasa ndani 
ya chama na kwamba pamoja na washirika wake, wamekuwa wakifanya mbinu za chini 
kwa chini kumuondoa Lipumba kwenye nafasi yake. 
Alisema pia katika Katiba ya CUF hakuna kipengele chochote kinachozungumzia Kamati 
ya Nidhamu na maadili hivyo alikuwa na sababu ya kuikataa Kamati hiyo. 
Pamoja na hayo, pia alisema sababu iliyomfanya aigomee Kamati hiyo ni baada ya kufahamu 
kuwa tayari wajumbe wake walikuwa na uamuzi wa kumfukuza uanachama kupitia barua pepe ya Maalim Seif kwenda kwa Lipumba. 
Aliinukuu  barua pepe hiyo ambayo ilisema “Nimeshauriana na Makamu tumeona kuna  ahadi ya jamaa yako (Hamad) na genge lake kuitwa kwenye Kamati ya  Nidhamu kuhojiwa, ushahidi wa kutosha umekusanywa dhidi yake…Kamati hiyo  italeta taarifa kwa Kamati Kuu ya Taifa. 
“Kamati Kuu ya Taifa ifanye uamuzi mgumu wa kuwasimamisha uongozi vinara wao na 
wengine  kupewa karipio, Kamati hiyo ifikishe taarifa yake katika kikao  kitakachofanyika Februari mwakani... muono wetu tumfukuze kwenye chama  na akienda mahakamani, ikitoa 
uamuzi wa kumpendelea, mwache awe Mbunge wa Mahakama kama akina Asha Ngede na Naila 
Majid,” Hamad alinukuu barua pepe hiyo. 
Aidha, alisema katika barua pepe hiyo, Maalim Seif alimshauri Lipumba kuwa ikiwezekana 
na Hamad Rashid aachwe hata akienda Chadema, CCM au aendelee na urafiki wake na 
Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa. 
“Jamani  hii ni dhambi kubwa anayoifanya Maalim Seif, mimi namheshimu sana na  ndio maana nataka ajipime mwenyewe kwani haya ndio yaliyomfanya Jumbe  ajiuzulu,” alidai mwanasiasa huyo mkongwe. 
Alisema hana ukaribu wowote na Lowassa zaidi ya kusalimiana kawaida kama watu wengine. 
Alisema amezushiwa mambo mengi, ameitwa muasi na anataka kukibomoa chama, wakati 
amekuwa kiungo muhimu baina ya Wazanzibari na Wabara ndani ya CUF. 
Aidha,  alisema amesaidia kampeni hadi ya Lipumba wakati wa uchaguzi na  kufadhili baadhi ya wabunge tofauti na Maalim Seif, aliyedai hajawahi  hata kufungua mkutano mmoja wa chama Bara. 
“Namuomba Maalim Seif kwa hali iliyofikia kama anataka kujisafisha na kuheshimika, basi 
afuate nyendo za aliyekuwa Rais wa Afrika Kusini Nelson Mandela na Baba wa Taifa hayati 
Mwalimu Julius Nyerere,” alisema. 
Alisema  hali ya chama hicho ni tete kwa kuwa hakiendeshwi kwa haki na mambo  mengi ya kusingiziana na kuzushiana huku fedha nyingi zikitumika bila  maelezo na iwapo watu 
wakihoji wanaitwa waasi. 
Alihoji inakuwaje chama hicho kimekaa zaidi ya miaka mitatu na CCM kujadili muafaka wa 
Zanzibar na kushindwa kukaa hata kikao kimoja kujadili na kufikia muafaka kuhusu mgogoro 
unaoendelea. 
Naye  mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho, Doyo Hassan Doyo, alisema  wanachokitaka kwa sasa ni kukirejesha chama hicho katika hali  inayokubalika kwa pande zote Bara na Visiwani ikiwemo kuhakikisha fedha  za ruzuku za chama zinafikia maeneo yote. 
“Sisi tunapata kwa mwezi Sh milioni 124 na michango ya fedha za wabunge takribani Sh 
milioni 60, jumla ni Sh milioni 190 hadi 200 lakini fedha hizi zinaishia makao makuu, huko 
wilayani watu wanazisikia tu, tukihoji tunaitwa waasi,” alidai Doyo. 
Kwa  sasa sakata hilo, baada ya Hamad Rashid kuigomea Kamati ya Nidhamu na  Maadili linasubiri kuwasilishwa wakati wowote mbele ya Baraza Kuu la CUF  kwa majadiliano zaidi.





