NCCR MAGEUZI YAWEKA KAMBI KIGOMA KUSINI ILI KUKABILIANA NA DAVID KAFULILA


BAADA ya kumtimua uanachama Mbunge wa Kigoma Kusini David Kafulila, NCCR-Mageuzi kimelivamia jimbo lake na kuanza kufanya mikutano ya hadhara kueleza sababu za kumtimua.

Kwa takriban wiki mbili sasa, Kafulila amekuwa mkoani Kigoma ambako pamoja na mambo mengine, amekuwa akifanya mikutano katika jimbo lake na akiwatoa hofu wapiga kura wake kuhusu uamuzi wa chama chake wa Desemba 17, mwaka jana wa kumvua  uanachama.

Baada ya Kafulila kufanya mikutano hiyo ambayo ilionekana kukibomoa chama chake na kujijengea ngome binafsi kisiasa, viongozi wa NCCR-Mageuzi wakiongozwa na Katibu Mkuu, Samwel Ruhuza wamelazimika kuweka kambi Kigoma tangu Januari Mosi.

Akizungumza kutoka Kigoma, Ruhuza alisema chama hicho kilifanya mikutano katika Jimbo la Kasulu Vijijini jana na leo kitakuwa katika Jimbo la Kasulu Mjini.

“Mikutano yetu tulikuwa tunaifanya kwa lengo la kuangalia utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na wabunge wetu pamoja na madiwani,” alisema Ruhuza.

Alisema licha ya kupokewa vizuri katika mikutano hiyo, hata uamuzi wa chama hicho kumvua uanachama Kafulila na wenzake watatu akiwemo aliyekuwa mgombea urais wake katika Uchaguzi Mkuu wa 2010 Hashim Rungwe, ulieleweka kwa wananchi wa Kigoma Kusini.

“Hatuna wasiwasi na hata ukifanyika uchaguzi mwingine Kigoma Kusini tunashinda bila wasiwasi wowote… mambo ni mazuri,” alisema Ruhuza.

Akizungumzia ziara ya viongozi hao, Kafulila alidai kwamba hawakupata mapokezi mazuri kama wanavyosema... “Mbona hawasemi walivyozomewa na wananchi wilayani Kasulu na kushushwa jukwaani walipokuwa Nguruka?.”

Kuhusu ziara zake, Kafulila alisema kikubwa alichokuwa akitaka kuwaeleza wananchi wa jimbo lake ni maendeleo aliyowaletea kwa kipindi cha mwaka mmoja wa ubunge wake.

Kafulila ambaye alitokea Chadema na kujiunga NCCR- Mageuzi  mwishoni mwa mwaka 2009, alivuliwa wadhifa wa Katibu Mwenezi wa chama hicho Desemba 8 mwaka jana na siku 10 baadaye alivuliwa uanachama kwa kosa la kuzungumza mambo ya chama katika vyombo vya habari

Posted by Bigie on 8:44 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.