UCHAGUZI WA SHIRIKISHO LA MUZIKI WASOGEZWA MBELE ,SABABU IKIWA NI KUKOSEKANA KWA WAGOMBEA WENYE SIFA


Uchaguzi wa Shirikisho la Muziki Tanzania (TMF) uliokuwa ufanyike wiki hii umesogezwa mbele baada ya kukosekana kwa wagombea wenye sifa wa kutosha kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za kusimamia uchaguzi.

Akitoa taarifa kwa wajumbe wa vyama vinne wa shirikisho hilo waliokuwa wamekusanyika ukumbi wa BASATA mwishoni mwa wiki hii kwa ajili ya uchaguzi, Mwenyekiti wa Kamati ya kusimamia uchaguzi, Angelo Luhala alisema kuwa, baada ya kamati yake kupitia fomu za wagombea kwa makini ilibainika kuwa ni wagombea wawili tu ambao walionekana wana sifa kati ya wagombea 22 wa nafasi mbalimbali.

“Ndugu wajumbe, kamati imepitia kwa makini fomu zote za wagombea 22 wa nafasi mbalimbali. Imebaini kuwa, ni wagombea wawili tu walionekana wana sifa za kugombea kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi wa shirikisho la muziki” alisema Luhala.

Alizitaja nafasi zilizopata wagombea kuwa ni ile ya Rais ambapo mgombea Fredrick Mariki maarufu kwa jina la Mkoloni kutoka chama cha muziki wa kizazi kipya (TUMA) ndiye pekee  alionekana anasifa huku wenzake watatu ambao ni Francis Kaswahili, Salim Omary Mwinyi na Samwel Semkuruto wakikosa.

Mbali na nafasi ya urais, Luhala alimtaja mgombea mwingine aliyekuwa na sifa kuwa, ni Che Mundugwao kutoka chama cha muziki wa asili (TAFOMA) aliyekuwa akigombea nafasi ya Makamu wa kwanza wa rais huku akisisitiza kuwa wagombea wengine waliosalia hawakuwa na sifa kwa mujibu wa katiba yao.

“Kinachotuongoza katika hili ni katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi ambazo mmeziweka nyinyi wenyewe. Lazima tutende haki na tulisimamie hili vinginevyo tutaonekana hatufai
” alisisitiza Luhala.

Sifa zilizokuwa zinahitajika kwa wagombea kwa mujibu wa katiba, kanuni na taratibu  ni pamoja na kuwa na elimu inayoanzia kidato cha nne au inayolingana na hiyo, kuwa raia wa Tanzania, kutokuwa na rekodi ya kufungwa na vingine vingi ambavyo kwa wagombea walikosa kabisa viambatanisho vyake.

Luhala alitoa wito kwa wagombea  wapya wenye sifa na vyama vingine vinavyounda shirikisho hilo ambavyo haviko hai kuwa hai sasa na kujitokeza pale uchaguzi utakapotangazwa tena baada ya mwezi mmoja.

Aidha, aliwakumbusha wale ambao waliomba kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na hawakuteuliwa kutokana na kutoambatanisha nyaraka hitajika kuleta kumbukumbu zilizokosekana ili kamati iridhie uteule wao.

Vyama vilivyotarajia kushiriki uchaguzi kutokana na kuwa hai ni pamoja na kile cha muziki wa kizazi kipya (TUMA, Muziki wa asili (TAFOMA), Muziki wa Injili (CHAMWITA) na kile cha Muziki wa Disco (TDMA) huku vyama  vya Taarab, Muziki wa Dansi na Mtandao wa wanamuziki Tanzania havikukushiriki kwa kutokuwa hai.

Posted by Bigie on 11:40 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.