LOWASA AVUNJA UKIMYA......APOKELEWA KAMA MFALME HUKO ARUMERU


HATIMAYE Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa amepanda jukwaani kumpigia debe mgombea ubunge wa CCM katika uchaguzi mdogo Jimbo la Arumeru Mashariki, Sioi Sumari, akiwaambia wananchi wa jimbo hilo kuwa Sioi ni mchapakazi na siyo mtu wa blah blah.

Kupanda jukwaani na kumnadi Sioi kumemaliza mjadala wa kama Mbunge huyo wa Monduli (CCM), angepata fursa hiyo kutokana na kile kilichokuwa kimeelezwa kuwa ni mgawanyiko mkubwa uliopo ndani chama hicho.

Awali, kulikuwa na taarifa kuwa Lowassa alikuwa hatakiwi kupanda jukwaani kumnadi mgombea huyo kwa maelezo kuwa kufanya hivyo kungekiharibia zaidi chama hicho.

Jana Lowassa alitengua kitendawili hicho saa 7:07 mchana alipowasili kwenye Viwanja vya Kikatiti akiwa na msafara wa magari yasiyopungua 20 yakiongozwa na pikipiki.

Baada ya kufika alipanda jukwaani kwa staili ya kukimbia na baadaye kucheza muziki jukwaani na kushangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo ambapo alipohutubia alisema wakazi wa jimbo hilo wanamfahamu kwamba yeye si mtu wa maneno, bali vitendo, hivyo kwa kumchagua Sioi ajenda ya maji itafungwa baada ya mgombea huyo kuapishwa.

Lowassa pia alimmwagia sifa Rais Jakaya Kikwete kwa uamuzi wake wa kuwapatia wakazi wa Kata ya Nduruma, Arumeru eneo la ekari 5,000 akisema ni mchapakazi hodari anayestahili heshima lakini pia Lowassa alikipiga vijembe Chadema akisema kilisababisha maandamano na vurugu katika Jimbo la Arusha Mjini na kuufanya mji huo kutokalika na kuwataka wakazi wa Arumeru wasikichague.

Alisema endapo watamchagua mgombea wa Chadema watakuwa wamefungulia fujo katika jimbo hilo kuanzia Mto Nduruma kuingia wilayani mwao, pia aliipongeza Kamati Kuu ya CCM kwa kupitisha jina la Sioi kuwania ubunge wa jimbo hilo akisema chama hicho kimeonyesha ukomavu wa demokrasia.

Akizungumza katika kampeni hizo, Sioi ambaye alimsifu Lowassa akiwaambia wakazi hao kuwa wanapaswa kuzingatia maneno aliyosema ili wapige hatua kimaendeleo, alisema endapo atapewa ridhaa ya kuwa mbunge, atahakikisha anawapa kipaumbele wanawake katika kujiajiri kwa kuwapatia mikopo ya biashara.

Alisema atashirikiana na Serikali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf), katika kufanikisha lengo hilo.
Awali, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole alisema wakazi wa jimbo hilo wanakabiliwa na kero za ardhi, maji na umeme hivyo kumchagua Sioi watakuwa wamechagua dawa ya matatizo yao.

Rais na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM, Benjamin Mkapa akimdai kwa mara ya pili Sioi jana, alitumia muda mrefu kufanya kile alichosema ni kutoa elimu ya uraia kwa vijana waliozaliwa baada ya uhuru akisema wale wanaodai chama hicho hakijafanya lolote ni wehu.

Akionekana kukwepa kujibu mashambulizi kutoka kambi ya upinzani yaliyotokana na hotuba yake kufungua kampeni za CCM wiki chache zilizopita, Mkapa alisema mbele ya CCM vyama vya upinzani ni sawa na vifaranga na chama hicho ni nambari moja.

Akihutubia mkutano uliofanyikia katika Kijiji cha Patandi Tengeru, Mkapa alisema: “Baada ya kuzindua kampeni za CCM yamesemwa maneno mengi dhidi yangu, chama changu na mgombea wetu lakini huu si wakati wangu wa kuyajibu.”

Posted by Bigie on 7:13 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.