HALI BADO NI TETE BUNGENI


Sakata la hoja ya kutokuwa na imani na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, limeshika kasi mpya.

Wakati orodha ya wabunge wanaotaka kuwasilishwa kwa hoja hiyo ikiwasilishwa kwa Spika Anne Makinda leo, Kambi ya Upinzani Bungeni imetangaza kuwa endapo Spika, atakataa kuitisha Bunge maalum baada ya siku 14 akishapokea hoja hiyo, wataipeleka kwa wananchi.

Hayo yalisemwa jana na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, akiwa ameongozana na Kiongozi wa wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya na kiongozi wa wabunge wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Moses Machali.

Alisema wanatarajia kuwa Spika Makinda ataitisha Bunge mapema ili kujadiliwa kwa hoja hiyo na iwapo hatawasilisha wataipeleka kwa wananchi ili kuongeza sahihi zaidi na kushinikiza kuitishwa kwa Bunge.

Zitto ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu ya Mashirika ya Umma (POAC), alisema jumla ya wabunge 73 kutoka vyama mbalimbali wamesaini katika hoja hiyo ambayo atawasilisha leo kwa Spika.

Alisema wabunge hao ambao amewatambulisha kama wazalendo ni kutoka Chadema, CCM, NCCR-Mageuzi, CUF na TLP.

Hata hivyo, hadi kufikia jana mbunge pekee wa chama cha upinzani wa UDP, John Cheyo, alikuwa hajasaini. Cheyo pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
“Anaweza kusaini maana bado leo (jana), na kesho (leo), anaweza kusaini hatuwezi kusema sasa amekataa kusaini,” alisema Zitto.

Alisema hoja hiyo inalenga katika kutimiza matakwa ya kikatiba na Kanuni za Bunge.

“Tutawasilisha rasmi kwa Spika taarifa ya maandishi kwa mujibu wa kanuni 133 (1) na (3) ya hoja kutokuwea na imani Waziri Mkuu kwa kushindwa kusimamia uwajibikaji wa serikali bungeni kwa mujibu wa ibara ya 52 na hivyo kulinda mawaziri wenye kusababisha matumizi mabaya ya fedha za umma na kulisababishia hasara taifa,” alisema na kuongeza:

“Tunatarajia kwamba siku 14 baada ya kuwasilisha hoja hiyo Bunge litakutana kwa haraka kujadili hoja hiyo ili kuwawezesha uwajibikaji na hatua kuchukuliwa za kuhakikisha mapendekezo ya ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na maazimio ya Bunge yanatekelezwa.”

Alisema hoja hii ni mwendelezo wa operesheni uwajibikaji hivyo anaowamba wabunge wazalendo na Watanzania wote waiunge mkono ili kuimarisha uwajibikaji wa viongozi, kupambana na ubadhirifu na kunusuru uchumi wa nchi na kuchangia katika ustawi wa wananch.

Kwa upande wake, Sakaya ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum, alisema CUF kinaungana na chama chochote katika hoja ambayo ina maslahi ya umma.

“Hiyo ndiyo sera yetu tunapokuwa katika mikutano ya hadhara, hata Lipumba (Mwenyekiti wa CUF), akiwa nchini na hata nje ya nchi amekuwa akizungumzia kuhusiana na ubadhirifu unaoendelea nchini,” alisema.

Alisema kwa miaka saba akiwa bungeni wamekuwa wakijadili kuhusiana na ripoti za CAG na kamati mbalimbali, lakini hakuna anayewajibika na kuongeza kuwa umefikia wakati sasa wawajibike.

Naye Machali ambaye ni Mbunge wa Kasulu Mjini, aliwapongeza wabunge wawili wa CCM, ambao ni Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe na Mbunge wa Mwibara, Aphaxard Lugola, ambao wamejitokeza waziwazi kusaini hoja hiyo bila kuogopa.

“Woga hautatusaidia kujenga uwajibikaji katika nchi yetu, tujitokeze kusaini, tuache woga ili tuweze kuisimamia serikali katika uwajibikaji…Nawapongeza sana wabunge waliosaini hoja hii wanaonyesha kuwa wanasimamia maneno yao,” alisema Machali.

Akizungumzia kuhusu idadi ya wabunge waliojitikeza kusaini hoja hiyo, Zitto alisema wabunge wengine watatu wa CCM waliosaini hoja hiyo wameomba majina yao kuhifadhiwa hadi leo watakapowasilisha hoja yao kwa Spika.

Zitto alielezea kusudio lake la kuwasilisha hoja hiyo muda mfupi baada ya kuhitimisha taarifa ya kamati yake Alhamisi usiku, akitaka wabunge kumuunga mkono kwa kuweka sahihi kwenye hoja hiyo.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, hoja hiyo inatakiwa iungwe mkono na wabunge wasiopungua asilimia 20 ambayo ni sawa na wabunge 70.

Ijumaa Spika Makinda wakati wabunge wakichangia taarifa za kamati za Bunge, alitamka kuwa hoja hiyo ni batili kwa kuwa kanuni zinataka kuwasilishwa kwa taarifa siku 14 kabla kujadiliwa, na kueleza kuwa mkutano wa sasa wa Bunge unamalizika Jumanne, siku nne tu zijazo.

CHANZO: NIPASHE

Posted by Bigie on 2:29 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.