SERIKALI KUIPA HADHI YA WILAYA HOSPITALI YA SINZA
JAMII 10:38 AM
WAKATI serikali ikiwa mbioni kuipatia hadhi Hospitali ya Sinza kuwa ya wilaya,kumebainika kwamba hospitali hiyo inakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo ya ukosefu wa wodi za kulaza wagonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo wakati wa kukabidhiwa msaada wa mashuka 69 yenye thamani zaidi ya sh. 600,000 kwa ajili ya wagonjwa kutoka kwa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mtaa (TALGWU).
Mratibu wa Huduma Saidizi Dk Hugolin Mselle alisema kuwa, licha ya serikali kuwa katika mkakati wa kuzindua rasmi hospitali hiyo kuwa ya wilaya lakini bado imeshindwa kuangalia matatizo mbalimbali yanayoikabili.
Akichanganua, Mselle alisema kwamba mbali na hospitali hiyo kutokuwa na wodi za kulaza wagonjwa kama wanaume, watoto na wakinamama bado hospitali hiyo inakabiliwa na ufinyu wa eneo, bajeti, pamoja na rasilimali watu kuwa chache.
“Hatuna wodi za kulaza wagonjwa wakiume,watoto wadogo, zaidi ya wakinamama wanaosubiria kujifungua watoto, na bajeti tunayotengewa na serikali kweli ni ndogo sana haikidhi ongezeko la wagonjwa” alisema Mselle.
Naye Katibu Mkuu wa TALGWU Taifa Sudi Madega alisema msaada huo umekuja baada ya chama hicho kubaini changamoto zinazoikabili hospitali hiyo bila kupatiwa ufumbuzi wa kina na serikali.
“Lengo la chama si kuishia hapa bali tuna mkakati endelevu ambao tunaendelea kujadili jambo jingine mbadala la kuisaidia hospitali hii kutokana na kuwa miongoni mwa hospitali za serikali zinazokabiliwa na changamoto mbalimbali.” Alisema Madega.
Hospitali hiyo inakabiliwa na uhaba wa vitanda vya kulaza wagonjwa, dawa, vitendea kazi, magodoro,vifaatiba vya upasuaji, ultrasound pamoja na jenereta.






