25 WAFIKISHWA MAHAKAMANI KWA UKAHABA
JAMII 2:29 AM
WAKAZI 25 wa maeneo tofauti jijini Dar es Salaam jana wamefikishwa katika Mahakama ya Jiji kwa kosa la kufanya ukahaba maeneo ya wazi. Akiwasomea shitaka hilo, Mwendesha Mashitaka, John Kijumbe mbele ya Hakimu Mkazi, Tymoth Lyon, alisema Mei 8, mwaka huu, saa tatu usiku maeneo ya Corner Bar Sinza, washitakiwa kwa makusudi walitenda kosa hilo kinyume na sheria ya makosa ya jinai ya mwaka 2002.
Alidai ni kawaida kwa wanawake hao kufanya vitendo vya ukahaba maeneo tofauti ya Dar es Salaam kwa lengo la kujipatia fedha kwa ajili ya kukidhi mahitaji yao.
Kwa upande wa Jamhuri, imeomba mahakama itoe adhabu kali kwa washtakiwa hao kwa kuwa vitendo vya ukahaba vimekuwa vikiendelea siku hadi siku.
Mwendesha mashataka huyo aliwataja wanawake hao kuwa ni Fatma Mohamed (20), Hadja Yusuph (25), Upendo Michael (20), Jackline Peter (20), Latifa Said (19), Fatma Omar (23), Zulfa Mussa (19), Asha Ramadhani (18), Lulu Gerald (19), Carline Aloyce (24), Queen Shabani (29), Mariam William (23) na Maria Mhando(20).
Wengine ni Nasra Ali (23), Asha Salum (19), Stela John (24), Sharifa Athumani (29), Angel Aloyce (22), Mariam Athuman (19), Amina Hassan (16), Zainab Shabani (23), Jacline Nelson (18), Happy Khamis (28), Doris Aloyce (29) na Hajula Issa (22).
Kati ya washitakiwa hao, watano walikubali kosa na wengine 20 walikana kosa hilo na upande ya dhamana ilikuwa wazi na kutakiwa kila mshtakiwa awe na wadhamini wawili, wawe ni watumishi wa Serikali na wasaini hati ya dhamana ya Sh 100,000.
Washitakiwa wote walishindwa kutimiza masharti ya dhamana na ndipo Hakimu Lyon alipowaamuru kurejeshwa Gereza la Segerea hadi Mei 25, mwaka huu kwa ajili ya kujibu tena shitaka hilo.
Chanzo: Mtanzania





