TANZANIA IPO HATARINI KUIGIA GIZANI


SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limesema hali ya umeme si ya kuridhisha na kwamba kuna hatari ifikapo Agosti mwaka huu taifa linaweza kuingia gizani.

Hatua hiyo, inatokana na kupungua kwa kina cha maji katika Bwawa la Mtera ambako sasa limefikia mita 1.36.


Kiwango hicho, ni kidogo ikiliganishwa na ujazo wa kawaida wa bwawa hilo ambao ni mita 698.5 chini usawa wa bahari.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, William Mhando alisema zaidi ya mita 690.0 za ujazo wa maji zinahitajika kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

Alisema kutokana na hali hiyo, shirika linafanya jitahada mbalimbali kuinusuru hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kutumia vyanzo vingine vya uzalishaji kama vile gesi na mafuta.

Hali si nzuri kabisa, maji yamepungua kwa kiasi kikubwa, ili kuinusuru hali hii tutajitahidi kutumia mtambo wa IPTL, na tunatarajia Juni kupitia mtambo wa Jackbsen kuzalisha megawati 100 hadi 350… kadri hali itakavyokuwa inaendelea, huku tukiendelea kujipanga,” alisema Mhando.

Licha ya Mhando kusema kuwa watatumia mtambo huo, alibainisha hali ni mbaya zaidi, kwani mtambo huo unaligharimu shirika Sh bilioni 26 kwa mwezi, kuuendesha kwa kutumia mafuta mazito.

“Watanzania wanapaswa kuelewa hali halisi tuliyonayo sasa, tunajitahidi sana.. sidhani kama mtu binafsi angeweza, kwa sababu licha ya kutumia kiasi hicho cha pesa kwa wastani tunapata umeme kwa senti 32 Dola za Marekani kwa yuniti, lakini tunawauzia wananchi kwa senti 11.9 tu ,”

“Vivyo hivyo, kwa upande wa Aggreko ni senti 42 kwa kutumia mafuta ya diseli…biashara tunayoifanya ni ngumu sana ni sawa na tunatoa huduma tu, wananchi wanapoomba vitu vingi waelewe tumeelemewa,” alisisitiza Mhando.

Akizungumzia mahitaji ya umeme Mhando alisema jumla ya megawati 833, zinahitajika na mahitaji halisi hadi kufikia Desemba, mwaka huu.

“Mahitaji ya sasa ni megawati 1000-1200 na ili hali yetu iwe nzuri, shirika linahitaji Sh trilioni 1.3,” alisema.

Katika hatua nyingine , Mhando alisema shirika hilo linapata hasara kubwa kupitia upotevu wa umma na kufikia asilimia 21 na kubainisha kuwa, upotevu unaotokana na watu ni asilimia 11 wakati kwenye mfumo ni asilimia 10.

“Tumeandaa mpango kabambe kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, kuwakamata wale wote wanaoliibia shirika, na hata wafanyakazi wetu tutawabana, pia tumeshabaini watu wakubwa ambao ni wezi hasa wale wenye viwanda…endeleeni kusubiri tu tutawafichua.” alisema.

Alisema, operesheni kata umeme iliyofanyika hivi karibuni imefanikiwa kwa kiasi kikubwa, kwani awali shirika hilo lilikuwa likikusanya asilimia 96, lakini kupitia operesheni hiyo ukusanyaji umepanda na kufikia asilimia 98 na Sh bilioni 60 zilikusanya kupitia madeni kutoka serikalini.

Akizungumzia kukatikakatika mara kwa mara kwa umeme katika eneo kubwa la jiji la Dar es Salaam, Mhando alisema hali hiyo inasababishwa na kuwepo kwa mahitaji makubwa ya umeme inayosababisha mitambo kuzidiwa, baada ya kuwepo kwa ongezeko kubwa la majengo.

“Mradi huu, utaanza hivi karibuni na tutashirikiana na wakandarasi kutoka nchini Finland na vituo vingine vitajumuisha maeneo ya Kurasini, Mbagala na Gongolamboto na vitafanyakazi kulingana na hali ya umeme,”

Chanzo: Mtanzania

Posted by Bigie on 2:31 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.