BABA "CHA POMBE" AMUUA MWANAE


MKAZI wa Kijiji cha Bugenika Kata ya Farkwa wilayani Kondoa, katika Mkoa wa Dodoma, Kingula Mdaki (56) anadaiwa kumuua mwanawe kwa mkuki huku chanzo kikidaiwa kuwa ni ulevi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Zelothe Stephen alisema aliyeuawa ni Kamuya Kingula (33) na kwamba mauaji hayo yalifanyika kijijini hapo Mei 6 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Kamanda, Mdaki ambaye ni baba alimjeruhi mwanawe kisogoni kwa kutumia mkuki kabla ya kupelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kondoa alikofia.

Kamanda Zelothe alisema, uchunguzi wa awali unaonesha kuwa chanzo cha mauaji hayo ni ulevi kwani baba na mtoto walikuwa wakinywa pombe ndipo wakaanza kurushiana maneno na hatimaye kupigana.

Mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili.

Katika hatua nyingine, mkazi wa Kijiji cha Leganga wilayani Kongwa, Lemanya Njimus (70) amejeruhiwa na kitu chenye ncha kali na alifariki wakati akipelekwa hospitalini.

Tukio hilo ni la Mei 7 mwaka huu kijijini hapo. Alijeruhiwa na watu wasiofahamika. Chanzo cha mauaji hakijafahamika na uchunguzi unaendelea.

Chanzo: Habarileo

Posted by Bigie on 2:47 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.