NAHODHA AMKABIDHI NCHIMBI OFISI
JAMII 2:44 AM

ALIYEKUWA Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai Nahodha, jana amekabidhi ofisi ya wizara hiyo kwa Dk. Emmanuel Nchimbi, huku akimweleza changamoto za kuzifanyia kazi, zikiwamo ya msongamano wa mahabusu magerezani na vitambulisho vya taifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Nahodha ambaye amehamia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alisema mrundikano wa mahabusu magerezani bado ni tatizo, hivyo kuna haja ya kulitazama suala hilo kwa umakini.
Alibainisha kuwa kutokana na kuliona tatizo waliunda kamati ya kushughulikia ili pamoja na mambo mengine isaidie mahabusu walio na kesi zisizokuwa na msingi kutokaa magerezani kama njia mojawapo ya kupunguza msongamano.
Kuhusu vitambulisho vya taifa, Nahodha alisema zoezi hilo limekwama kidogo kutokana na kufanyiwa marekebisho na kwamba hali hiyo imechangiwa na uundwaji wa mikoa na wilaya mpya.
Alisema walitazamia kuzindua rasmi mradi huo Mei 8 mwaka huu lakini ilishindikana kutokana na sababu hiyo, hivyo mamlaka husika ndio waratibu wa zoezi hilo na wameahidi ndani ya miezi miwili kulikamilisha.
Kwa upande wake, Waziri Nchimbi aliahidi kufanya kazi kwa uadilifu ili kutimiza malengo ya Watanzania na Rais Jakaya Kikwete.





