JOHN SHIBUDA NA HOJA YAKE YA UKABILA (MAKALA, MWANANCHI JUMAPILI)

Ndugu zangu,

Kuna wakati nilitua uwanja wa ndege wa Nairobi na kupanda teksi.  Nilishangaa sana pale dereva wa teksi alipojitambulisha kwangu kwa kutamka; “ I am Peter, and a Kikuyu”


Kwamba anaitwa Peter na kabila lake ni Mkikuyu. Kwa mimi Mtanzania hilo lilikuwa jambo la ajabu sana. Sijapata kujitambulisha kwa  jina na kabila langu katika maisha yangu yote. Si kawaida yetu Watanzania.

Katika nchi za wenzetu kuna tatizo la ukabila. Watanzania tuna bahati kubwa; hatuna ukabila. Labda ukabila wetu upo kwenye lugha ya Kiswahili. Udugu wetu  Watanzania umejenga sana kwenye lugha ya Kiswahili. Anayezungumza lugha ya Kiswahili ni mwenzako huyo, huulizi tena kabila lake.

Ndio, Watanzania hatuna ukabila wala udini. Wenye kutaka kupandikiza mbegu za chuki za ukabila na udini miongoni mwetu ni wachache sana, na hususan wanasiasa kwa malengo ya kisiasa. Tuwe makini sana.

Ona majuzi hapa, Mtanzania mwenzetu John Shibuda ameibua hoja ya ukabila. Nakubaliana na Shibuda kwenye hoja ya kutaka haki yake ya kutangaza nia ya kuwania Urais wa nchi hii iheshimiwe.

Shibuda ana haki hiyo. Na haitakuwa mara ya kwanza kwake kututangazia Watanzania nia yake hiyo.

Lakini, inasikitisha, kuwa hoja ya pili ya Shibuda imechangia kuua hoja yake ya kwanza; ni hoja ya ukabila.
Shibuda anaonekana kututaka Watanzania tujadili ukabila na hususan chama chake cha Chadema na ukabila ulio ndani ya chama hicho.

Shibuda ni mmoja wa viongozi ninaowaheshimu sana kwa mchango wao kwa taifa letu. Naamini, kuwa Shibuda anaheshimika na wengi wengine hapa nchini. Lakini, kwa kutuletea Watanzania hoja ya Chadema na ukabila,  nahofia Shibuda amepotea.  


Maana, hoja yake haina msingi. Imejengeka katika hisia kuliko uhalisia. Yumkini, Shibuda amekuja na hoja hii sasa, ama , kwa bahati mbaya, au kukusudia. Hilo la mwisho halina kusudi la kujenga, bali kubomoa. Inasikitisha.

Maana, hoja ya ukabila haina umaarufu katika nchi yetu kwa sasa. Watanzania wa sasa hatuendekezi ukabila. Kauli ya

Shibuda kuwa anabaguliwa katika chama chake cha Chadema  kwa vile ni Msukuma haikupaswa kutamkwa kwa  mtu kama Shibuda na haikupaswa kutamkwa na yeye na bado akaendelea kubaki katika chama anachoamini kina ubaguzi wa kikabila na huku mwenyewe akiwa mwathirika wa ubaguzi huo.

Na kwa vile hana ushahidi wowote wa kuthibitisha anachosema, Shibuda anachochea moto ambao Watanzania hatuutaki. Ukabila ni moto wa hatari, kama ilivyo kwa moto wa udini.

Kama Shibuda analalamika kuwa anabaguliwa kwa vile ni Msukuma, ingekuwaje basi, John Shibuda angeitwa Ramadhan Shibuda? Je, angeongeza dai la pili; kuwa anabaguliwa Chadema kwa vile ni Muislamu. Si Mkatoliki?

Kama Shibuda anadhani kauli zake za ukabila zinakisaidia chama chake cha zamani cha CCM, basi, napo anakosea; maana, kwa CCM kuhusishwa sasa na kauli za Shibuda za ukabila, kunakiharibia zaidi kuliko kukijenga kwa Watanzania walio wengi.  Lililo bora kwa CCM sasa ni kujitenga na kauli za Shibuda juu ya ukabila .


Maana, Watanzania wa leo si wa jana.  Ni wepesi sasa wa kubaini hila na ghilba za wanasiasa. Wengi wanaonekana kusikitishwa na hoja ya Shibuda juu ya kubaguliwa kwa vile ni Msukuma.  Wanasikitika kwa vile wanadhani hoja imejengeka katika hila na ghilba kwa wananchi.


Shibuda afahamu ukweli huu; Watanzania walio wengi  kwa sasa wanataka mabadiliko. Wanaiona sasa mishale ya saa ya mabadiliko ikisonga mbele. Wanamwona hata Rais wao, Jakaya Kikwete akisaidia kusukuma mabadiliko hayo.Ni mabadiliko ya kimfumo.


Hivi, ni Watanzania wangapi walifahamu kuhusu uwepo wa CAG miaka mitatu iliyopita?  Hakika, upinzani bungeni, ndani ya chama tawala, na uwepo wa ofisi ya CAG iliyopewa nguvu umeanza kurudisha matumaini ya Watanzania. Uwepo wa uwajibikaji wa viongozi.


Naam, Watanzania hawataki tena kurudi katika mfumo wa chama kimoja  kilichoshika hatamu. Majaribio yote ya kuua upinzani, kufuta fikra huru, yatazidi kulaaniwa na walio wengi katika nchi hii.

Hivyo, Shibuda hawezi tena leo kurudisha nyuma mshale wa saa ya mabadiliko; hata kwa ajenda ya ukabila. Nahitimisha.

Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765

Posted by Bigie on 10:54 PM. Filed under , . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.