NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini
Posted by Bigie siasa 5:37 AMTume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja na Mara.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo ofisini kwake Dr. Sisti
Kariah amesema kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha
uandikishaji kwa BVR katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na
Mara zoezi ambalo lilitarajiwa kuanza leo na badala yake zoezi hilo
litafanyika kuanzia tarehe 16/06/2015.
Uamuzi wa kusogeza mbele unafuatia mabadiliko ambayo yanaendelea
kufanywa na Mipaka ya kiutawala ya kata, Vijiji, Vitongoji na Mitaa.
Uandikishaji kwa kutumia mfumo wa BVR unatoa fulsa kwa wananchi wote
wenye sifa za kuwa wapiga kura na wale walio na kadi za Mpiga watatakiwa
kujiandikisha upya.
Zoezi la Uboeshaji wa Daftari la Kudumu la wapiga
hivisasa limefikia asilimia 50 kwa maana ya mikoa iliyofikiwa na zoezi
hilo nchini Tanzania.
Membe: Nikiwa Rais Wasanii Wataenda Kujifunza Nje
Posted by Bigie siasa 8:43 PM
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe,
amesema kama atachaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, atahakikisha anasimamia haki za wasanii ipasavyo.
Membe alitoa kauli hiyo mkoani Lindi wakati akitangaza nia ya kuwania
urais kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
“Nitahakikisha naweka mipango imara katika kusimamia kazi za wasanii wote kunufaika na hakimiliki zao,” alisema.
Pia alisema atahakikisha wasanii wanakwenda kujifunza nje ya nchi
masuala ya sanaa ili sekta hiyo ipate mabadiliko ya kimaendeleo kwa
wasanii na Serikali kwa ujumla.
“Nikichaguliwa kuwa rais, nimejiwekea mikakati mingi kuhakikisha sekta
ya sanaa inapiga hatua kutoka hapa tulipo sasa,” alisema Membe.
Katika mkutano huo, waliohudhuria ni baadhi ya wasanii akiwemo
mchekeshaji, Adam Melele ‘Swebe’, Hemed Malyaga ‘Mkwere Orijino’ na
Kulwa Kikumba ‘Dude’.
Gazeti la Mtanzania
JK aaga Watanzania ughaibuni
Posted by Bigie siasa 1:46 AM
RAIS Jakaya Kikwete ameendelea kuaga Watanzania kila anapopata fursa
ya kukutana nao, huku mafanikio ya miaka kumi ya uongozi wake
yakijidhihirisha katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambako Bajeti ya Serikali kupitia
wizara mbalimbali imekuwa ikijadiliwa na kupitishwa.
Mwishoni mwa wiki hii akiwa jijini Stockholm nchini Sweden
alikokwenda kwa ziara ya siku tatu, ambayo pia ni ya kwanza ya kuaga
nchi wahisani, Rais Kikwete alikutana na Watanzania waishio nchini humo,
ambako kabla ya kuwaaga, alielezea changamoto anazoziacha.
Rais Kikwete katika mazungumzo hayo, amesema Rais ajaye anakabiliwa
na changamoto ya kuhakikisha Tanzania inayoundwa na Muungano wa nchi
mbili, inaendelea kuwa moja kwa kudumisha umoja wa Watanzania na amani.
“Hapa tulipofikia lazima tuhakikishe Taifa linakuwa moja, kuna vyama
na makabila mbalimbali, lakini lazima tuhakikishe nchi inabaki moja,”
amesisitiza Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia alielezea matumaini yake kuwa Tanzania itapata
kiongozi mzuri na kuelezea mafanikio ambayo Serikali yake imeyapata na
kutumaini kuwa yatadumishwa na kuendelezwa na Rais ajaye.
Uchumi Awali akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika uchumi
alipokutana na Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven, Rais Kikwete
alisema uchumi wa Tanzania umekua kwa wastani wa asilimia 7, katika
kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Mbali na kukua kwa uchumi wastani, pato la Taifa limekua kwa zaidi ya
mara tatu, kutoka Dola za Kimarekani bilioni 14.4 hadi kufikia Dola
bilioni 49.2 za Marekani.
Aidha, pato la mtu mmoja mmoja kwa mwaka 2005, wakati Rais Kikwete
alipokuwa akiingia madarakani lilikuwa Dola za Marekani 375, lakini
mwaka jana lilifikia Dola za Marekani 1,038.
Mafanikio hayo kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, zilisababisha Waziri
Mkuu wa Sweden, Lofven, kuona umuhimu wa kuanzisha awamu nyingine ya
uhusiano katika maendeleo, utakaoleta maana zaidi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo Sweden (SIDA),
Torbjorn Pettersson, ambaye pia alikutana na Rais Kikwete, alieleza kuwa
Sweden imeridhishwa na kiwango cha maendeleo na juhudi za kupunguza
umaskini nchini Tanzania.
Hata hivyo, Rais Kikwete alipokuwa akizungumzia kasi ya kuondoa
umasikini, alisema bado juhudi za kuondosha umaskini zinahitajika na
zitafanikiwa kwa kuelekeza nguvu kwenye kilimo, ambacho ndicho
kinachoajiri na kutegemewa na Watanzania wengi zaidi hasa wanaoishi
vijijini.
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Sweden,
Urban Ahlin, pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini
humo na kushukuru kwa misaada ya maendeleo kwa takribani miaka 50 sasa.
Viongozi hao wamempongeza Rais kwa kufanya ziara ya shukrani na
kuwaaga, kwani ni mara chache kwa viongozi wengi wa Kiafrika kuaga na
kuondoka madarakani.
Mbali mazungumzo hayo ya Sweden, mafanikio mengine ya Serikali kwa
miaka 10 iliyopita, kwa wiki ya tatu sasa yamegeuka nguzo mbuhimu ya
kutetea bajeti za wizara mbalimbali bungeni na katika warsha mbalimbali.
Afya Kwa mfano katika wiki hii katika sekta ya afya, Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alipokuwa akizungumza na wahariri wa
vyombo vya habari, aliwataka kusoma takwimu za mafanikio ya Tanzania
ikilinganishwa na nchi zingine badala ya kuishia kusoma bajeti ya sekta
hiyo pekee.
Kwa mujibu wa Dk Rashid, pamoja na Tanzania kuwekeza asilimia 2.8 tu
ya pato la Taifa katika sekta ya afya, vifo vya watoto chini ya miaka
mitano vimepungua na mafanikio hayo ni makubwa kuliko katika nchi
zinazoonekana kupiga hatua zaidi katika uwekezaji huo.
Alitaja nchi ya Botswana yenye uwekezaji wa asilimia 3 ya pato la
Taifa katika afya na Zambia yenye asilimia 4.2 ya pato la Taifa katika
sekta hiyo, kwamba mataifa hayo katika kila vizazi hai 1,000 wamekuwa
wakipoteza watoto wengi zaidi.
Wakati Tanzania ikipoteza watoto 52 katika kila watoto hai 1,000
wanaozaliwa, Kenya wao wanapoteza watoto 71, Zambia watoto 87 na
Cameroon ni watoto 95 katika kila vizazi haivyo 1,000.
Umeme Katika upatikanaji wa huduma za nishati na umeme, mpaka mwaka
jana, Serikali ilikuwa imefikisha umeme kwa zaidi ya asilimia 35 ya
Watanzania, kutoka asilimia wastani wa chini ya asilimia 15 iliyokuwepo
mwaka 2005.
Akizungumza bungeni jana, Waziri wa Nishati na Madini, George
Simbachawene alisema idadi ya wateja waliounganishiwa umeme vijijini
imefikia asilimia 68. Idadi hiyo imeongezeka kutoka 143,113 mwaka 2013
hadi kufikia wateja 241,401 Aprili mwaka huu.
Alisema wateja hao wameunganishiwa umeme kupitia miradi ya Wakala wa
Umeme Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Bomba la gesi Akizungumzia jitihada za kuanza kutumia hazina ya gesi
asilia kwa ajili ya kuzalisha umeme badala ya mafuta mazito
yanayosababisha umeme uwe bei ghali nchini, Simbachawene alisema mitambo
ya kusafisha gesi asilia na bomba la gesi asilia, vitaanza kazi rasmi
Septemba mwaka huu.
Alisema ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara kupitia Lindi
hadi Dar es Salaam umekamilika, ujenzi wa mitambo ya kusafirisha gesi
asilia katika eneo la Madimba, Mtwara umefikia asilimia 99 na mitambo ya
Songo Songo, Lindi nao umefikia asilimia 99. “Mitambo na bomba hilo
vitaanza kufanya kazi (Commercial Operational Date) Septemba 2015.
“Haya ni matokeo ya utekelezaji wa miongoni mwa miradi iliyoanishwa
kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16),” alisema
Simbachawene.
Alisema matumizi ya gesi asilia yatachochea ukuaji wa viwanda,
utunzaji wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kuongeza
ajira na hatimaye kuleta maendeleo ya uchumi na kijamii kwa ujumla.
Elimu Katika elimu, mwaka 2005 wakati Rais Kikwete akiingia
madarakani, Bajeti ya Serikali katika sekta hiyo ilikuwa Sh bilioni 600,
lakini mwaka jana ilifikia Sh trilioni 3.4.
Sababu ya uwekezaji huo mkubwa, Rais Kikwete aliwahi kusema
alipoingia madarakani, alikuta Tanzania yenye watu wengi zaidi katika
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iko nyuma ikilinganishwa
na Kenya na Uganda, kwa idadi ya wanafunzi waliokuwa wakisoma shule za
sekondari na vyuo.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mwaka 2005 wanafunzi waliokuwa wakisoma
sekondari ni zaidi ya 500,000, wakati nchini Uganda waliokuwa wakisoma
sekondari walikuwa zaidi ya 700,000 na Kenya zaidi ya 900,000.
Kwa upande wa vyuo vikuu, Tanzania ilikuwa na wanafunzi 40,000 tu wakati Uganda ilikuwa na wanafunzi 124,000 na Kenya 180,000.
Hatua zilizochukuliwa, Rais Kikwete alisema Serikali kwa kushirikiana
na wananchi, waliamua kujenga shule za sekondari za kata, ambapo
wananchi walihamasishwa, wakahamasika wakajenga shule mpaka Mkurugenzi
mmoja wa elimu, akahofia kukosa walimu wa kupeleka katika shule hizo.
Kwa sasa Tanzania ina wanafunzi 1,800,000 wanaosoma sekondari na
imeshaipita Uganda yenye wanafunzi 1,700,000 wanaosoma elimu ya
sekondari, lakini imezidiwa na Kenya ambayo ina wanafunzi 2,100,000.
Hata hivyo alisema ni rahisi kuipita Kenya kwa hilo pengo la
wanafunzi 300,000, kwa kuwa shule za sekondari zilizopo zina nafasi ya
kuongeza wanafunzi milioni mbili zaidi.
Kwa upande wa elimu ya juu, Rais Kikwete alisema vyuo vikuu
vimeongezeka kutoka 26 mwaka 2005 hadi kufikia 52 na idadi ya wanafunzi
walio katika vyuo vikuu ilitoka 40,719 hadi kufikia 200,956.
Hata bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh bilioni 56.1 hadi Sh bilioni 345 mwaka 2014.
Hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza na Wazee wa Dodoma 4 Novemba 2014
Posted by Bigie siasa 9:17 PMNdugu Wananchi;
Nakushukuru sana Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Dodoma, Mheshimiwa Balozi Job Lusinde kwa kuandaa mkutano huu. Wakati nilipofanya ziara ya Mkoa wa Dodoma tulipanga tukutane lakini kwa vile ratiba yangu iliingiliwa na mambo mengi, hivyo haikuwezekana, lakini leo imewezekana.
Pengine hii ndiyo siku ambayo Mwenyezi Mungu alipanga tukutane. Tumshukuru Muumba wetu kwa rehema zake, na tumuombe ajaalie mkutano wetu uanze salama na uishe salama. Nawashukuru kwa Risala yenu na maudhui yake. Nawaahidi nitayafuatilia na majibu mtapata. Pamoja na yaliyomo kwenye risala yenu mimi nina mambo manne ambayo ni yatokanayo na ziara yangu nchini China na Vietnam, maradhi ya Ebola, uchaguzi wa Serikali za Mitaa na hatua zinazofuata kwenye Mchakato wa Katiba.
ZIARA YA CHINA NA VIETNAM
Ndugu Wananchi;
Kuanzia tarehe 21 Oktoba, 2014 hadi tarehe 28 Oktoba, 2014 nilikuwa katika ziara rasmi ya kutembelea nchi za China na Vietnam. Nilitembelea China tarehe 21 hadi 26 Oktoba, 2014 na Vietnam tarehe 26 hadi 28 Oktoba, 2014. Ziara hizo nilizifanya kufuatia mwaliko wa Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping na mwaliko wa Rais wa Vietnam Mhe. Truong Tan Sang. Ziara katika nchi hizo zilikuwa za mafanikio makubwa sana hata kuliko nilivyotarajia. Nchini China tulipokelewa kwa namna hawajafanya kwa miaka mingi.
Ziara ya China
Ndugu Wananchi;
Nchini China, kwa makubaliano na wenyeji wetu tulifanya hafla maalum ya kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China. Katika hafla hii upande wa China uliwakilishwa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Li Yuanchao. Pande zetu mbili ziliitumia fursa hiyo kuzungumzia tulipotoka, tulipo sasa na mbele tuendako.
Kwa jumla wote tumeridhika kuwa tumekuwa na nusu karne ya uhusiano wenye mafanikio makubwa. Katika kipindi hiki nchi zetu zimekuwa marafiki wa kweli, wa kuaminiana na kusaidiana kwa mambo mengi. Katika medani za kimataifa nchi zetu zimekuwa zikielewana kwa mambo mengi na kusaidiana. China ilikuwa ngome kuu katika kusaidia kwa hali na mali harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika.
Wakati ule Tanzania ilikuwa ikiongoza nchi za mstari wa mbele. Wenzetu bado wanakumbuka sana jinsi nchi yetu ilivyokuwa mstari wa mbele kuipigania nchi ya China kurejeshewa haki yao hususan ya kuketi kiti chao katika Umoja wa Mataifa, baada ya Chama cha Kikomunisti chini ya uongozi wa Mwenyekiti Mao Tse Tung kufanikiwa kukishinda Chama cha Kuomintang na kiongozi wake Chian Kai Sheki na kulazimika kukimbilia Taiwan.
Mataifa makubwa ya Magharibi yalikataa kuitambua China mpya na kuitenga. Katika kufanya hivyo, waliitambua Taiwan na kuifanya kuwa ndiyo wawakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa.
Baada ya hapo Jamhuri ya Watu wa China ilipinga uamuzi ule na kuanzisha kampeni ya kudai haki yake stahiki. Madai yao hayo yalipata nguvu pale Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipoamua kuwa Tanzania ishiriki katika kampeni hiyo kwa nguvu zake zote. Kwa kushirikiana na nchi nyingine rafiki, jitihada hizo za pamoja zilizaa matunda na mwaka 1971, China ilipokubaliwa kuchukua nafasi yake stahiki katika Umoja wa Mataifa na Taiwan kuondolewa.
Ndugu zetu wa China hawasahau msaada wetu huo na hawaoni haya kulisemea waziwazi jambo hilo na vizazi vyote vya China vinafundishwa kuhusu wema ambao Tanzania imewafanyia. Kwa sababu hiyo, Tanzania ina nafasi maalum nchini China. Wao wenyewe wana msemo maalumu kuhusu Tanzania kwamba ni “all weather friends”. Yaani marafiki wa majira yote.
Katika ziara yangu nilifuatana na kaka yangu Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye ndiye alikuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa wakati ule. Rafiki zetu wa China walifurahi sana kumwona Dkt. Salim kwani yeye hasa ndiye aliyefanya kazi ya kushawishi nchi nyingine kuiunga mkono Jamhuri ya Watu wa China.
Pia nilifuatana na Mheshimiwa Balozi Mstaafu Jenerali Mrisho Sarakikya aliyekuwa Mkuu wa Majeshi wa kwanza wa Tanzania. Yeye ndiye alihusika sana kujenga uhusiano wa mambo ya kijeshi baina ya nchi yetu na China. Pia, nilikwenda na Balozi Mstaafu, Mzee Waziri Juma aliyewahi kuwa Balozi wa Pili wa Tanzania nchini China.
Kama mjuavyo nchi ya China imetusaidia mambo mengi kwa maendeleo yetu. Misaada mingine ilihusu vitu vikubwa ambavyo katika hali ya kawaida isingewezekana kusaidiwa na nchi nyingine zinazotoa misaada ya maendeleo na mikopo.
Miongoni mwa hayo ni ujenzi wa Reli ya Uhuru (TAZARA), misaada ya zana, vifaa na mafunzo vilivyosaidia kujenga Jeshi letu jipya yaani JWTZ baada ya kuvunjwa kwa lile tulilorithi kutoka kwa Wakoloni kuaasi Januari 20, 1964. Msaada wao mkubwa ndiyo uliotuwezesha mpaka kuweza kulinda na kukomboa nchi yetu dhidi ya uvamizi na kutekwa eneo la Misenyi, Kagera na majeshi ya dikteta Iddi Amin wa Uganda.
Hata sasa China imeendelea kuwa mshirika wetu mkubwa kuliko wote katika kuimarisha na kuendeleza Jeshi letu. Msaada mwingine mkubwa ni ule mkopo wa dola za Marekani bilioni 1.2 wa kujenga bomba jipya la gesi kutoka Mtwara na Songosongo hadi Dar es Salaam. Isingekuwa rahisi kupata mkopo mkubwa kiasi kile kutoka nchi nyingine au Shirika lolote la fedha duniani.
Mkopo ule unalimaliza tatizo la upungufu wa umeme kutokea sasa mpaka mwaka 2020 inapokadiriwa kuwa nchi yetu itahitaji megawati 10,000. Hata wakati huo bomba hili ni muundombinu wa msingi utakaorahisisha upanuzi wa miundombinu ya kuzalisha umeme kutosheleza mahitaji hayo kama itaamuliwa gesi iendelee kuwa chanzo kikuu cha nishati ya umeme nchini.
Katika mazungumzo yangu na Waziri Mkuu Li Keqiang na Rais Xi Jinping wote wawili wameelezea kuridhika kwao na uhusiano baina ya nchi zetu tangu siku za nyuma mpaka hapa tulipo sasa. Hali kadhalika walielezea kuwa wangependa kuona uhusiano wetu na ushirikiano wetu unaimarika na kukua mpaka kufikia hatua bora na ya juu kabisa.
Niliwahakikishia kuwa hiyo ndiyo fikra yangu na Watanzania kuhusu uhusiano baina ya nchi zetu mbili rafiki.
Kwa nyakati tofauti viongozi wote wakuu wa China walinihakikishia utayari wao wa kuendelea kuchangia maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiusalama ya Tanzania. Jambo lililonipa faraja kubwa mimi na wenzangu ni kuwa mambo yote tuliyoomba ndugu zetu wa China watusaidie wamekubali. Hakika Wachina wameendelea kuwa marafiki wa kweli wa nchi yetu na watu wake.
Tuliwaomba waendelee kushirikiana nasi na wabia wenzetu wa Zambia kulijenga upya Shirika la Reli ya TAZARA na wamekubali. Tuliwaomba pia tuendelee kushirikiana kukuza uwekezaji na biashara baina ya nchi zetu mbili rafiki.
Walilipokea jambo hilo kwa furaha. Ni ukweli ulio wazi kwamba biashara na uwekezaji umekua sana kiasi cha kuifanya China kuwa nchi inayoongoza kwa mambo yote mawili. Hata hivyo, sote tumekubaliana kuwa biashara ya dola za Marekani bilioni 3.7 na uwekezaji wa dola za Marekani bilioni 2.5 ni kidogo mno hivyo tuongeze juhudi tufanye vizuri zaidi katika kipindi kifupi kijacho.
Ndugu Wananchi;
Kulikuwa na mkutano mkubwa wa uwekezaji uliohudhuriwa na makampuni ya kichina yapatayo 500 yaliyokuwa tayari kuwekeza na kufanya biashara na Watanzania. Kwa upande wetu miradi kadhaa tuliyopeleka imepata wabia. Miongoni mwa waliofaninikiwa sana ni Shirika la Nyumba la Taifa waliopata wabia watakaowekeza dola za Marekani bilioni 1.7 kwenye ujenzi wa nyumba.
Aidha, kuhusu ujenzi wa Ukanda wa Kiuchumi wa Mbegani ambao tuliwaomba watusaidie kusukuma utekelezaji wake, viongozi wa China walielezea utayari wao kusaidia mradi huo ufanikiwe. Tulipokuwa Shenzhen, tulipata nafasi ya kutembelea Makao Makuu ya Kampuni ya China Merchants Ltd., na kuzungumza na viongozi wake.
Walitembezwa kuangalia shughuli za kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na jinsi Kampuni hiyo ilivyoshiriki katika ujenzi wa mji wa Shenzhen kutoka kijiji cha uvuvi na kuwa jiji kubwa la kisasa, lenye maendeleo ya kiuchumi, teknolojia na biashara. Waliahidi kutumia ujuzi wao, maarifa yao na uwezo wao wa kifedha kujenga Mbegani kama ilivyotokea Shenzhen.
Siku ile pia tulishuhudia Mfuko wa Akiba wa Oman wakitiliana saini na China Merchants na Mamlaka yetu ya Uendeshaji wa Maeneo Huru ya Uwekezaji (EPZA) hati ya makubaliano kujiunga rasmi katika kuwekeza na kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo. Kilichonifurahisha sana siku ile ni kule kuwepo kwa mpango kazi unaotarajia ujenzi wa bandari na ukanda wa maendeleo ya kiuchumi wa Mbegani kuanza tarehe 1 Julai, 2015.
Hali kadhalika, nilipokuwa Shenzhen nilipata nafasi ya kutembelea kampuni za teknolojia ya habari na mawasiliano za Huawei na ZTE. Nilifika mjini Jinan, Jimbo la Shandong na kutembelea kampuni nyingine kubwa ya aina hiyo iitwayo INSPUR. Bahati nzuri kampuni zote zimewekeza Tanzania na wanataka kupanua uwekezaji wao.
Nilipokuwa Jinan nilitembelea Hospitali Kuu ya Jimbo la Shandgon, Mjini Jinan, ambayo imetoa madakatari wengi na kupata nafasi ya kuwashakuru viongozi wa Jinan na Jimbo la Shandong kwa kutuletea madakatari na wataalamu wengine wa afya kuja kufanya kazi nchini Tanzania. Vile vile, nimewashukuru kwa mchango wao muhimu uliotuwezesha kupata hospitali ya moyo katika Hospitali ya Muhimbili.
Pamoja na kuwashukuru niliomba idadi iongezwe kwani mahitaji yapo na watu wanawapenda Madaktari wa China. Yapo mambo mengi mazuri yaliyofanyika katika ziara yangu nchini China ambayo tutakesha kama tutahitaji kuyafafanua moja baada ya jingine. Hata hivyo, napenda kuyazungumzia mambo mawili.
Kwanza ni taarifa aliyonipa Rais Xi Jinping kwamba wanaongeza ufadhili wa masomo kwa kutupa nafasi 100 zaidi kwa vijana wa Tanzania kusoma China kwa kipindi cha miaka mitano. Pia wamekubali kutusaidia ujenzi wa chuo cha ufundi (VETA) cha Mkoa wa Kagera. Aidha, wamekubali ombi langu la kuongeza idadi ya madaktari na wataalamu wa afya kutoka China kuja kufanya kazi nchini.
Ziara Vietnam
Ndugu Wananchi;
Baada ya kumaliza ziara yangu China nilitembelea Vietnam kwa siku mbili. Huko nako nilikwenda kuimarisha na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi zetu, na kujifunza zaidi kutoka kwa wenzetu ambao wamepata mafanikio makubwa kiuchumi katika kilimo na viwanda kwa kipindi kifupi. Hii ni nchi ambayo tulianza nayo mageuzi ya kiuchumi wakati mmoja mwaka 1986.
Wenzetu wameweza kupata mafanikio makubwa katika kilimo, viwanda, ufugaji wa samaki na mengine mengi. Kwa upande wa teknolojia ya mawasiliano ya simu, wanayo kampuni ya Viettel ambayo imekuwa kubwa duniani na inakusudia kuwekeza nchini.
Kwa kweli mafanikio ambayo Vietnam imepata tangu mwaka 1986 yanatupa matumaini kwamba na sisi Tanzania tunaweza kufanikiwa kama wao. Hatuna budi kujipanga vizuri. Tumekubaliana kushirikiana zaidi hasa kubadilishana uzoefu na maarifa katika kilimo na viwanda.
UGONJWA WA EBOLA.
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia, si mara yangu ya kwanza kufanya hivyo. Hili si jingine bali ni tahadhari juu ya maradhi ya Ebola yaliyoanzia huko Afrika Magharibi katika nchi za Liberia, Sierra Leone na Guinea. Baadae yalifika Nigeria, Senegal, Mali, Marekani, Spain na Uingereza.
Inakadiriwa kuwa ugonjwa huu hatari umekwishaua watu 4,960 na wengine 13,567 wameambukizwa toka ulipoanza hadi sasa. Ugonjwa huu umeendelea kuwa tishio la dunia kutokana na kasi kubwa ya kuenea kwake. Lakini hasa kwamba asilimia 70 mpaka 90 wanaoupata ugonjwa huu hupoteza maisha. Bahati mbaya hauna dawa wala kinga. Bado wataalamu wa dawa wanachuna bongo.
Taarifa njema ni kuwa ugonjwa huu haujaingia nchini Tanzania. Hata hivyo, hii haiondoi ukweli kuwa unaweza kufika kwani watu wanatembea kutoka nchi zenye maradhi haya na kuja nchini kwetu. Hapa jirani na sisi upo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Sitashangaa pia kwamba wapo Watanzania wanaokwenda nchi zenye maambukizi makubwa hata wakati huu. Watu hao wana hatari kubwa ya kupata maambukizi.
Narudia kukumbusha umuhimu wa kuchukua tahadhari kitaifa na kila mtu anayeishi hapa nchini. Sisi Serikalini tunaendelea kuchukua hatua stahiki na kuimarisha jitihada na hatua za kuwachunguza wageni katika mipaka yetu ya usafiri wa nchi kavu na usafiri wa anga.
Tumejiandaa vya kutosha kutambua watu wenye joto kubwa zaidi ya joto la kawaida la mwili wa mwanadamu. Hali kadhalika, tumewataka watu wanaoingia nchini kueleza kama katika wiki tatu zilizopita wametembelea nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia. Nia ya kutaka waseme siyo kuwazuia wasiingie nchini bali kuwapa ushauri juu ya dalili za ugonjwa wa Ebola na nini wafanye iwapo dalili hizo zitawatokea. Pia tunapenda kujua mahala watakapofikia ili tuweze kuwafuatilia.
Ndugu Wananchi;
Ninawaomba ushirikiano wa kila mmoja wenu kutoa taarifa kwa wakati mara mtakapoona mtu mwenye dalili za ugonjwa huo ambazo ni homa kali ya ghafla, kutokwa na damu mwilini, kutapika na kuharisha kwa wakati mmoja. Toeni taarifa ili wataalamu wenye ujuzi na vifaa stahili vya kujikinga waweze kuja kuwahudumia ipasavyo wagonjwa wenye dalili hizo. Jiepusheni na kumsogelea au kugusana na mtu wa aina hiyo.
Na, maiti aliyekufa kutokana na ugonjwa wenye dalili hizo pia asiguswe. Kufanya hivyo ni kujiweka kwenye hatari ya moja kwa moja ya kuambukizwa kwani huenda mtu huyo ni muathirika wa Ebola. Toa taarifa upate maelekezo ya kitaalamu.
UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA
Ndugu Wananchi;
Kama mnavyofahamu tarehe 14 Desemba, 2014 tutafanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ngazi ya vitongoji, mitaa na vijiji. Tumelazimika kufanya Uchaguzi huo mwezi Desemba, 2014 badala ya mwezi Oktoba kama ilivyostahili kutokana na shughuli za Bunge Maalum la Katiba kuendelea hadi tarehe 4 Oktoba, 2014 kwa kupitisha Katiba Inayopendekezwa. Kutokana na Taifa kuwa katika jambo lile kubwa ilionekana ni busara kuacha kwanza mchakato ule ukamilike kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Nimeambiwa na TAMISEMI kwamba maandalizi ya uchaguzi huo yanakwenda vizuri na kwamba ratiba imekwishatolewa, na majina ya mitaa, vijiji na vitongoji vipya nayo yamekwishatolewa. Kazi ya kuandikisha wapiga kura itafanyika kuanzia tarehe 23 Novemba, 2014 na itamalizika kwa orodha ya wapiga kura kubandikwa mahali pa wazi hasa kwenye mbao za matangazo katika vitongoji, mitaa, na vijiji husika ifikapo tarehe 30 Novemba, 2014.
Kufanya hivyo kutawezesha wananchi kukagua orodha hiyo kuona kama majina yao yapo, na kujiridhisha kuwa majina ya wale walioandikishwa kwenye daftari hilo ni wapiga kura wenye sifa stahiki za kupiga kura katika uchaguzi huo katika eneo husika. Nawasihi wananchi wote mjitokeze kwa wingi kujiandikisha na kukagua orodha ya wapiga kura itakapobandikwa ili kufanikisha zoezi hilo.
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi vyama vya siasa vinapaswa kuwasilisha fomu za wagombea wao kwa Msimamizi wa Uchaguzi kuanzia tarehe 20 hadi 22 Novemba, 2014. Kwa maana hiyo, wale wenye shauku, nia na sifa za kugombea uongozi katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa, wanapaswa kutega sikio ili kujua ratiba za uchaguzi na uteuzi ndani ya vyama vyao ili wapate fursa ya kuteuliwa kugombea.
Napenda kuchukua fursa hii kuwahimiza wananchi wote wakiwa pia vijana na wanawake wasibakie nyuma, wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi hizo na nyingine katika Uchaguzi Mkuu ujao. Ratiba ya uchaguzi huo iliyotolewa na TAMISEMI inaonyesha kwamba mikutano ya kampeni ya kuwanadi wagombea itafanyika kwa siku 14 kuanzia tarehe 30 Novemba, 2014 hadi tarehe 13 Desemba, 2014 siku moja kabla ya siku ya kufanyika kwa uchaguzi huo.
Ndugu Wananchi;
Mfumo wa utawala wa nchi yetu huanzia katika ngazi ya kitongoji na mtaa kisha kijiji, kata na hatimaye taifa. Kwa hiyo uchaguzi wa vitongoji, mitaa na vijiji ndiyo msingi wa uongozi na utawala wa nchi yetu. Tukipata viongozi wazuri katika ngazi hii ya msingi, tutakuwa tumefanikiwa sana katika kuimarisha utawala bora na kuongeza kasi ya maendeleo yetu.
Rai yangu kwenu, wananchi wenzangu ni kuwa mjitokeze kwa wingi wakati wa kampeni kuwasikiliza wagombea wetu wakijieleza, kisha tuwachague wale watu ambao sisi tunaona wanatufaa. Lazima tutambue kuwa ngazi ya vitongoji, mitaa na vijiji ndiyo msingi wa uongozi wa nchi yetu. Tukipata watu wazuri tutakuwa tumejenga msingi imara wa uongozi katika taifa letu.
Watu wote watakaojitokeza kugombea katika ngazi ya vitongoji, mitaa na vijiji vyetu ni watu tunaoishi nao na kwamba tunawafahamu vizuri sana. Hatuna budi kuvitendea haki vijiji, mitaa na vitongoji vyetu kwa kuwachagua viongozi wazuri watakaokuwa chachu ya maendeleo katika maeneo yetu. Tukifanya makosa ya kuchagua watu wasiofaa tuelewe kwamba tutakuwa tumejinyima fursa ya kuwa na viongozi bora kwa kipindi cha miaka 5 ijayo. Pia tunaweza kuzua migogoro na kupunguza kasi ya maendeleo katika maeneo yetu. Tusione haya kuwashawishi watu wazuri wajitokeze kugombea.
MACHAKATO WA KATIBA NA KURA YA MAONI
Ndugu wananchi,
Bunge la Katiba lilikamilisha kazi yake ya kutunga Katiba mpya ilipofika tarehe 2 Oktoba, 2014 ambayo ilikuwa siku mbili kabla ya muda uliopangwa wa tarehe 4 Oktoba, 2014. Tarehe 8 Oktoba, 2014, Mwenyekiti wa Tume ya Katiba aliikabidhi Katiba hiyo kwangu na kwa Rais wa Zanzibar kama yalivyo matakwa ya Kifungu cha 28A(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mara nyingine tena nawapongeza kwa dhati aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel John Sitta, Makamu wake Mhe. Samia Suluhu na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa kazi kubwa na nzuri. Wametupatia Katiba Inayopendekezwa inayojitosheleza kwa kila hali. Nawapongeza pia Makatibu wa Bunge, Sekretarieti yao na wafanya kazi wote.
Bunge Maalum la Katiba linastahili pongezi nyingi kwa kazi nzuri waliyofanya na hasa kwa kuikamilisha ndani ya muda wa uliopangwa wa siku 130 tu. Baadhi ya nchi duniani jukumu hili limechukua muda mrefu zaidi ya uliokusudiwa au hata kushindikana.
Tutakuwa wachoyo wa fadhila tusipoipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mwenyekiti Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu wake Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani pamoja na Wajumbe wote wa Tume hiyo. Tunawapongeza kwa kutayarisha Rasimu nzuri ya Katiba ambayo ndiyo iliyoliongoza Bunge Maalum la Katiba kupata Katiba Inayopendekezwa iliyo bora.
Kilichobakia ni kuwaachia wananchi kuamua kama wanaitaka Katiba Inayopendekezwa au hapana. Watafanya hivyo kwenye kura ya maoni itakayofanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni iliyotungwa kutekeleza matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Ndugu wananchi,
Miaka ya nyuma kulikuwa na tangazo la sabuni ya Omo lililokuwa likisema “Uzuri wa Ngoma Sharti Uicheze”. Uzuri wa Katiba Inayopendekezwa siyo wa kuambiwa. Unahitaji uione, uisome na uielewe. Imeandikwa kwa Kiswahili rahisi na fasaha. Inasomeka na kueleweka kwa urahisi sana.
Ni rai yangu kwamba wananchi wote muipate nakala ya Katiba Inayopendekezwa na mjisomee.
Sheria imeniagiza kuichapisha Katiba hiyo kwenye gazeti la Serikali ndani ya siku saba baada ya kukabidhiwa. Nimekwisha kufanya hivyo. Aidha, Sheria inaeleza kwamba Katiba Inayopendekezwa isambazwe kwenye magazeti ya kawaida ndani ya siku 14.
Zoezi hili ni endelevu. Usambazaji wa Katiba Inayopendekezwa unaendelea na utaendelea mpaka Kura ya Maoni itakapopigwa.
Wito wangu kwenu Watanzania wenzangu ni kwamba msikubali kulaghaiwa na maneno ya wale wachache wanaotaka kuturudisha nyuma na kutunyima fursa ya kupata Katiba iliyo bora zaidi. Maana hapajawahi kutokea ushiriki mpana kama huu katika kutengeneza Katiba katika nchi yetu. Pengine, hata kwingineko duniani si wengi wametoa fursa kama tulivyofanya sisi.
Kura ya Maoni
Ndugu wananchi,
Sheria ya Kura ya Maoni iliniagiza kutangaza tarehe ya Kura ya Maoni katika Gazeti la Serikali ndani ya siku 14 baada ya kupokea Katiba Inayopendekezwa. Nimefanya hivyo. Awali Sheria hiyo iliagiza Kura ya Maoni ifanyike na matokeo yake yajulikane ndani ya siku 70. Waziri mwenye dhamana ya Uchaguzi alipowauliza viongozi wa Tume ya Uchaguzi kuhusu utekelezaji wa matakwa hayo ya Sheria, Tume ilisema isingweza kuendesha Kura ya Maoni ndani ya muda huo. Mambo yanayojitajika ni mengi mno ambayo hayawezi kukamilika katika muda huo.
Wakaomba wapewe muda zaidi. Bahati nzuri Kifungu 51 cha Sheria ya Kura ya Maoni kimetoa mamlaka kwa Waziri mwenye dhamana ya Uchaguzi baada ya kushauriana na Waziri anayehusika na Uchaguzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kubadilisha masharti haya kama kutakuwa na umuhimu wa kufanya hivyo.
Baada ya mashauriano hayo, Mawaziri wenye dhamana ya uchaguzi wa pande zetu mbili za Muungano waliridhika kuwa upo umuhimu wa kusogeza mbele muda ili kutoa fursa kwa Tume kukamilisha taratibu inazowajibika kufanya. Hayo ni pamoja na kuboresha Daftari la Kudumu la Mpiga Kura, matayarisho ya upigaji wa Kura ya Maoni na mambo mengine kadhaa.
Hivyo basi, tarehe 03 Oktoba, 2014, Waziri mwenye dhamana ambaye ni Waziri Mkuu kwa kutumia mamlaka aliyopewa ya Kifungu cha 51 cha Sheria ya Kura ya Maoni, alitangaza kupitia gazeti la Serikali kubadilisha sharti la siku 70 na kuacha Rais aamue siku ya kupiga kura.
Kwa sababu ya mabadilikio hayo, tarehe 10 Oktoba, 2014 nilitangaza kupitia Gazeti la Serikali kuwa Kura ya Maoni itakuwa tarehe 30 Aprili, 2015 ili kutoa fursa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kukamilisha taratibu zake. Katika tangazo hilo pia, nilielekeza kuwa kampeni zitaanza tarehe 30 Machi na kuisha tarehe 29 Aprili, 2014 siku moja kabla ya siku ya kupiga kura, kama ilivyo desturi yetu katika upigaji kura hapa nchini.
Ndugu Wananchi;
Natambua kuwepo dhana kuwa siku za kampeni ni 60. La hasha! Siku za Kampeni zinaamuliwa na Rais, kufuatia Kifungu cha 4 (2) b kisemacho: “Amri kwa ajili ya kura ya maoni itakuwa kama ilivyo kwenye fomu iliyotajwa kwenye jedwali la Sheria hii, na itaainisha:
(a) Katiba Inayopendekezwa kuandikwa;
(b) Kipindi ambacho kampeni kwa ajili ya Kura ya Maoni itafanyika;
(c) Kipindi ambacho Kura ya Maoni itafanyika”
Tume ya Uchaguzi ina mamlaka ya kuruhusu vyama vya kijamii na vya kiraia kutoa elimu ya umma ndani ya siku 60 kabla ya siku ya Kura ya Maoni. Tume imepewa mamlaka hayo na Kifungu cha 5 (4) cha Sheria ya Kura ya Maoni. Kwa sababu hiyo, nawaomba Watanzania wenzangu tuzingatie matakwa ya Sheria ya Maoni ambayo imeelekeza vizuri kuhusu lini Kura ya Maoni itafanyika na lini wadau watoe elimu kwa umma. Naomba tuwe na subira mpaka hapo Tume ya Uchaguzi itakapotoa maelekezo ya utekelezaji wa fursa husika kwa wadau.
Ndugu wananchi,
Ni matarajio yangu kwamba wananchi wote mtajitokeza kwa wingi kwenda kuboresha taarifa zenu kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura kama itakavyoelekezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, na hatimaye itakapofika tarehe 30 Aprili, 2015 mtakwenda kwa wingi kupiga kura ya kuamua kuhusu hatma ya Katiba Inayopendekezwa. Naomba mfanye uamuzi mzuri. Fursa hii ni adhimu na ya kihistoria ambayo tukiipoteza huenda itachukua miaka mingi kuipata tena.
Mtakapokuwa mnakwenda kupiga kura zingatieni maslahi yenu pamoja na ya watoto na wajukuu zenu, maana Katiba ndiyo inayoweka misingi na mstakabali wa taifa letu sasa na karne nyingine zijazo.
Hitimisho
Ndugu Watanzania wenzangu,
Naomba nimalizie kwa kuwasihi mjitokeze kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 14 Desemba, 2014. Endeleeni kusoma Katiba Inayopendekezwa ili muda utakapofika kila mtu atoe uamuzi stahiki na wenye maslahi kwa nchi yetu. Nimezitaka Wizara na Taasisi zinazohusika na utekelezaji wa makubaliano yetu na Serikali ya China na Vietnam kuchukua hatua za ufuataliaji na wanipe taarifa. Narudia kutoa wito tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola. Nawaomba muendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika jitihada zake za kuiletea maendeleo nchi yetu na watu wake.
Mwisho, ingawa siyo kwa umuhimu, vijana wetu 297,488 wameanza mtihani wa taifa wa kidato cha nne jana tarehe 3 Novemba, 2014. Tuna imani wamejiandaa vya kutosha na wameandaliwa vyema na walimu, wazazi na walezi wao kwa ajili ya mtihani huo. Naungana na walimu, wazazi, walezi na Watanzania wote kuwatakia kila la heri katika mtihani wao huo.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza!
"UNAYAJUA YALIYOMKUTA AMINA CHIFUPA?.....SASA TUKUONE UMEKUWA MWANASIASA".......HIVI NI VITISHO KWA LOVENESS WA CLOUDS FM
Posted by Bigie DIVA, habari za kitaifa, picha za utupu, siasa 11:23 PM
Unakumbuka kuna muda mtangazaji wa Clouds FM Loveness aka Diva alitangaza kuwa mwaka 2015 atagombea ubunge?
Well, hakuwa anatania kwani hivi karibuni alianza kwa kuchukua kadi ya uanachama wa CHADEMA......

Diva akionesha kadi yake ya uanachama wa CHADEMA

Lakini pamoja na kuchukua uamuzi huo, jana Diva amesema amepewa vitisho kutoka baadhi ya watu kuwa hatofika popote na huenda yakamtokea kama ya marehemu Amina Chifupa.
“Kuna watu walinikalisha chini 4hours, wananiambia umemuona Amina Chifupa, kaishia wapi?! Basi niliogopa sana,” alitweet kumweleza mbunge wa jimbo la Kawe mheshimiwa Halima Mdee.
“Don’t tell me u give in so easily…..I thought i knew you…..kumbe mwoga?umenidisappoint!,” alisema Halima.
Mazungumzo na mheshimiwa Mdee yalimpa nguvu kidogo mtangazaji huyo ambaye aliandika,
“Really?Basi Umerudisha imani yangu, Its official am in , Joining the movement , sitagive up tena,tatizo my friends hate politics.”
NAPE AKIWA SONGEA JANA
Posted by Bigie habari za kitaifa, siasa 1:52 AM
Kiana mama wakigara gara chini mbele ya Nape (jukwaani) baada ya kuingiwa na hotuba yake


Nape akisalimia wazee baada ya kuwasili Kata ya Tanga, wilanai Songea ambako yalifanywa mapokezi yake
Na Bashir Nkoromo NAPE AZOA WANACHAMA WAPYA VIJANA ELIMU YA JUU IRINGA, WAFAGILIA MAGEUZI NDANI YA CHAMA
Posted by Bigie habari za kitaifa, siasa 4:40 PM
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye akizungumza na vijana katika mahafali ya Makada wa CCM kutoka katika vyuo vikuu mkoa wa Iringa, ambapo alikabidhi vyeti kwa wahitimu 230 na kadi za CCM kwa wanachama wapya 148.
Wabunge wa Chadema Waangwa rasmi kwa kuangalia mechi ya kimataifa
Posted by Bigie habari za kitaifa, siasa 12:56 AMWabunge wa chama cha Chadema wakipata flash ya pamoja na warembo wa Kibrazil ndaniya uwanja wa FedexField, uliopo Landover Maryland Nchini marekani.
Picha ya pamoja na viongozi wa juu wa Chadema kwenye mpambano wa US na Brazil Usiku wa kuamkia leo Alhamis Mei 31,2012 ndani ya ndani ya uwanja wa Fedex, uliopo Landover Maryland Nchini marekani
Nabendera ya Taifa wakishangilia Bao la kwanza la Brazil lilifungwa kwa Penalti na mchezaji Neymar
Wachezaji wa Brazil wakilinda ngome yao kwa kuwadhibiti timu ya US kwenye mechi hiyo ya kirafiki ambapo timu ya Brazil waliweza kuwabamiza US bao 4-1 nyumbani kwao.
US. hoi kwa Brazil baada ya kubamizwa bao nne bao la kwanza lilifungwa na Neymar, na lapili na Thiago mnamo wa dakika ya 11, kipindi cha kwanza. bao la US lilifungwa na Hercules Gomes dakika ya 44 kipindi chakwanza hadi mapumziko Brazil 2 US 1 kwenye mchezo wa kirafiki.

Forward wa United States Landon Donovan, akipandisha majeshi juu huku alidhibitiwa na Brazil defender Marcelo wa Brazi katika mpambano wa kirafiki.
Hivyo ndivyo ilivyo katika uwanja wa FedexFeild, uliopo Landover Maryland Nchini Marekani
(Picha na SWAHILIVILLA BLOG)
JOHN SHIBUDA NA HOJA YAKE YA UKABILA (MAKALA, MWANANCHI JUMAPILI)
Posted by Bigie habari za kitaifa, siasa 10:54 PM
Kuna wakati nilitua uwanja wa ndege wa Nairobi na kupanda teksi. Nilishangaa sana pale dereva wa teksi alipojitambulisha kwangu kwa kutamka; “ I am Peter, and a Kikuyu”
Kwamba anaitwa Peter na kabila lake ni Mkikuyu. Kwa mimi Mtanzania hilo lilikuwa jambo la ajabu sana. Sijapata kujitambulisha kwa jina na kabila langu katika maisha yangu yote. Si kawaida yetu Watanzania.
Katika nchi za wenzetu kuna tatizo la ukabila. Watanzania tuna bahati kubwa; hatuna ukabila. Labda ukabila wetu upo kwenye lugha ya Kiswahili. Udugu wetu Watanzania umejenga sana kwenye lugha ya Kiswahili. Anayezungumza lugha ya Kiswahili ni mwenzako huyo, huulizi tena kabila lake.
Ndio, Watanzania hatuna ukabila wala udini. Wenye kutaka kupandikiza mbegu za chuki za ukabila na udini miongoni mwetu ni wachache sana, na hususan wanasiasa kwa malengo ya kisiasa. Tuwe makini sana.
Ona majuzi hapa, Mtanzania mwenzetu John Shibuda ameibua hoja ya ukabila. Nakubaliana na Shibuda kwenye hoja ya kutaka haki yake ya kutangaza nia ya kuwania Urais wa nchi hii iheshimiwe.
Shibuda ana haki hiyo. Na haitakuwa mara ya kwanza kwake kututangazia Watanzania nia yake hiyo.
Lakini, inasikitisha, kuwa hoja ya pili ya Shibuda imechangia kuua hoja yake ya kwanza; ni hoja ya ukabila.
Shibuda anaonekana kututaka Watanzania tujadili ukabila na hususan chama chake cha Chadema na ukabila ulio ndani ya chama hicho.
Shibuda ni mmoja wa viongozi ninaowaheshimu sana kwa mchango wao kwa taifa letu. Naamini, kuwa Shibuda anaheshimika na wengi wengine hapa nchini. Lakini, kwa kutuletea Watanzania hoja ya Chadema na ukabila, nahofia Shibuda amepotea.
Maana, hoja yake haina msingi. Imejengeka katika hisia kuliko uhalisia. Yumkini, Shibuda amekuja na hoja hii sasa, ama , kwa bahati mbaya, au kukusudia. Hilo la mwisho halina kusudi la kujenga, bali kubomoa. Inasikitisha.
Maana, hoja ya ukabila haina umaarufu katika nchi yetu kwa sasa. Watanzania wa sasa hatuendekezi ukabila. Kauli ya
Shibuda kuwa anabaguliwa katika chama chake cha Chadema kwa vile ni Msukuma haikupaswa kutamkwa kwa mtu kama Shibuda na haikupaswa kutamkwa na yeye na bado akaendelea kubaki katika chama anachoamini kina ubaguzi wa kikabila na huku mwenyewe akiwa mwathirika wa ubaguzi huo.
Na kwa vile hana ushahidi wowote wa kuthibitisha anachosema, Shibuda anachochea moto ambao Watanzania hatuutaki. Ukabila ni moto wa hatari, kama ilivyo kwa moto wa udini.
Kama Shibuda analalamika kuwa anabaguliwa kwa vile ni Msukuma, ingekuwaje basi, John Shibuda angeitwa Ramadhan Shibuda? Je, angeongeza dai la pili; kuwa anabaguliwa Chadema kwa vile ni Muislamu. Si Mkatoliki?
Kama Shibuda anadhani kauli zake za ukabila zinakisaidia chama chake cha zamani cha CCM, basi, napo anakosea; maana, kwa CCM kuhusishwa sasa na kauli za Shibuda za ukabila, kunakiharibia zaidi kuliko kukijenga kwa Watanzania walio wengi. Lililo bora kwa CCM sasa ni kujitenga na kauli za Shibuda juu ya ukabila .
Maana, Watanzania wa leo si wa jana. Ni wepesi sasa wa kubaini hila na ghilba za wanasiasa. Wengi wanaonekana kusikitishwa na hoja ya Shibuda juu ya kubaguliwa kwa vile ni Msukuma. Wanasikitika kwa vile wanadhani hoja imejengeka katika hila na ghilba kwa wananchi.
Shibuda afahamu ukweli huu; Watanzania walio wengi kwa sasa wanataka mabadiliko. Wanaiona sasa mishale ya saa ya mabadiliko ikisonga mbele. Wanamwona hata Rais wao, Jakaya Kikwete akisaidia kusukuma mabadiliko hayo.Ni mabadiliko ya kimfumo.
Hivi, ni Watanzania wangapi walifahamu kuhusu uwepo wa CAG miaka mitatu iliyopita? Hakika, upinzani bungeni, ndani ya chama tawala, na uwepo wa ofisi ya CAG iliyopewa nguvu umeanza kurudisha matumaini ya Watanzania. Uwepo wa uwajibikaji wa viongozi.
Naam, Watanzania hawataki tena kurudi katika mfumo wa chama kimoja kilichoshika hatamu. Majaribio yote ya kuua upinzani, kufuta fikra huru, yatazidi kulaaniwa na walio wengi katika nchi hii.
Hivyo, Shibuda hawezi tena leo kurudisha nyuma mshale wa saa ya mabadiliko; hata kwa ajenda ya ukabila. Nahitimisha.
Maggid Mjengwa,
Iringa
0788 111 765
CHADEMA Wafunga Barabara Kwa Saa 2 Baada Ya Mkutano uliofanyika jana jijini Dar
Posted by Bigie habari za kitaifa, siasa 8:33 PM







Kutoka Facebook: Nape Asema; " Inatosha!"
Posted by Bigie habari za kitaifa, siasa 8:29 PM
"INATOSHA!! Mmewadanganya sana watu, utadhani wakivaa magwanda matatizo yao na ya nchi yanakwisha!! Mnatafuta biashara ya magwanda yenu!! Karibuni nazindua operation ya VUA GWANDA NA GAMBA VAA UZALENDO!!
kinachopungua kwetu, Afrika na Dunia nzima ni UZALENDO, sasa tunakwenda kuwavua magwanda na magamba na KUWAVISHA UZALENDO na ndo DAWA INAYOHITAJIKA DUNIANI LEO. Stay tuned!!!! Soon operation hii itaanza tufute uongo!"- Nape Nnauye
WATEULE WA TANZANIA KATIKA BUNGE LA AFRIKA MASHARIKI
Posted by Bigie habari za kitaifa, siasa 8:08 PMSpika wa Bunge Mhe. Anne Makinda amefunga rasmi semina elekezi ya siku mbili kwa wabunge wapya wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki na kuwataka wabunge hao wakazingatie maslahi ya Taifa katika Bunge hilo. Pichani Mhe. makinda akisisitiza jambo wakati wa hotuba yake ya kufunga semina hiyo jana jijini Dar es Salaam.
Spika wa Bunge Mhe. Anne Makinda akimkabidhi hadidu za rejea Mwenyekiti wa wabunge wapya wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki Mhe. Adam Kimbisa mara baada ya kufunga rasmi semina hiyo jana jijini Dar es salaam. Picha na Owen Mwandumbya.
RIPOTI KAMILI YA HUKUMU YA KESI ILIYOKUWA IKIMKABILI JOHN MNYIKA
Posted by Bigie habari za kitaifa, siasa 9:47 AMMahakama Kuu Kanda ya dar es Salaam leo imemtangaza mbunge wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (Chadema) kuwa ni mbunge halali wa jimbo hilo.
Hayo yamesemwa LEO Katika Mahakama Kuu na Jaji Upendo Msuya katika hukumu ya kesi ya uchaguzi dhidi ya Mnyika iliyokuwa imefunguliwa na Hawa Ng'humbi ambaye alikuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika jimbo hilo.
Jaji huyo amesema kuwa mdai ambaye ni Nghumbi alishindwa kuthibitishia Mahakama kuhusu kesi dhidi ya Mnyika katika madai yake matano aliyokuwa aliyawasilisha mahakamani hapo na hivyo mahakama hiyo imeamuru gharama za kesi hiyo zitalipwa na Ngh'umbi.
Hata hivyo baada ya hukumu hiyo Ng'humbi alisema kuwa hawezi kusema kama ameridhika au laa kwa wakati huo.
Kwa upande wa chadema ilikuwa ni Sherehe ya ushindi,huku Mnyika akiondolewa kwa kubebwa na wana Chadema waliokuwa wamejaa mahakamani hapo ambapo Mwenyekiti wa Chama hicho,Freeman Mbowe alisema kuwa ameridhika na hukumu hiyo na kukiri kuwa mahakama imetenda haki.
Aidha mahakama hiyo imetamka kuwa uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa wa halali na kura alizopata Mnyika ni halali, Mnyika ndiye mbunge halali wa jimbo la Ubungo. Maombi ya Ng’humbi kuwa mahakama hiyo ibatilishe matokeo yaliyompa ushindi Mnyika yametupwa mbali na Jaji Msuya.
Mahakama hiyo ilijaa wanachama wa vyama hivyo viwili ingawa wanachama wa Chadema walikuwa ni wengi zaidi hata hivyo askari walikuwa wametanda kila mahali katika mahakama hiyo pamoja na barabara ya Kivukoni kuanzia Mahakama ya Rufaa wakiwa na magari.
Baada ya Hukumu Mnyika alikumbatiana na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe ambaye alikuwepo mahakamani hapo na kutoka nje huku Mnyika akiwa amebebwa na wafuasi wa Chadema huku wakiimba kwa ushindi huo, hata hivyo hakukuwa na vurugu kubwa zilizokuwa na madhara zaidi ya maandamano yaliyoondoka mahakamani hapo wakiimba.
Mbowe aliwaeleza waandishi wa habari kuwa kesi hiyo imetumia zaidi ya Sh bilioni mmoja hivyo kesi kabla ya kusikilizwa ichunguzwe zaidi ikionekana haina hoja za msingi ni vizuri kutupwa mapema. Hata hivyo alisema “ mahakama imetenda haki na hii inaonyesha namna ambavyo inaweza kutenda haki hata katika vyama vya upinzani.”
Kwa upande wake Hawa Ng’humbi alisema kuwa amepokea maamuzi yaliyotolewa na Mahakama lakini hawezi kusema lolote kwa wakati huo na kwamba wana CCM wawe na utulivu kwasababu anaamini ni watulivu kama kuna jambo tofauti atazungumza baadaye.
Hukumu hiyo imesomwa leo katika Mahakama Kuu kanda ya Dar es Salaam kwa takribani saa moja na nusu kuanzia saa 4 asubuhi na Jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, Jaji Upendo Msuya ambaye aliamuru kuwa gharama za kesi hiyo zitabebwa na mdai (Hawa Ng’umbi).
Jaji Msuya katika hukumu hiyo alisema kuwa Ng’humbi katika madai yake yote matano hakuna hata moja alilolithibitisha kama ambavyo sheria inamtaka mdai katika kesi ya uchaguzi, kuthibitisha dai lake bila kuacha shaka yoyote na pia kutoa ushahidi kuonyesha ni namna gani iliathiri matokeo ya uchaguzi.
Katika hukumu hiyo, jaji huyo alisema kuwa Ng’humbi na mashahidi wake aliowawasilisha mahakamani hapo hawakuonyesha wala kuthibitisha madai yaliyowasilishwa mahakamani kwamba yalitendeka, na pia iliathiri matokeo ya uchaguzi uliofanyika Octoba 31,2010.
“Nilipata nafasi ya kupitia ushahidi wa kila shahidi pamoja na vielelezo vilivyotolewa mahakamani katika kesi hii lakini nimeshangaa ni kwanini mdai hakuleta mahakamani mashahidi ambao walikuwepo katika chumba cha majumuisho ya kura ambako ndiko madai hayo yalikotokea,” alisema jaji Msuya.
Alisema hata hivyo hakuelewa ni kwanini watu zaidi hawakuletwa kuunganisha ushahidi wao kuthibitisha madai ya mdai na pia kama kweli madai hayo yalitokea ni kwanini wagombea wengine au watu waliokuwa katika chumba cha majumuisho hawakulalamika.
Fomu namba 24 b ilikuwa na dosari na ndiyo ilikuwa inabishaniwa na Ng’humbi ilikosewa kuandika. Kura halali ni Mnyika aliyetangazwa kuwa ni mshindi alipata kura 66,742 wakati Ng’humbi kura 50,544. Wagombea wote kura 132496.
Alisema kuwa katika ushahidi wa mdai hakuonyesha ni vipi ongezeko hilo la kura liliathiri matokeo ya uchaguzi na pia mdaiwa Mnyika anahusika vipi na ongezeko hilo.
Hata hivyo jaji huyo kabla hajaanza kuchambua hoja za Ng’humbi aliwapongeza mawakili katika kesi hiyo ambao walijitahidi kuwasilisha mashahidi na kuhoji maswali ya msingi bila kupoteza muda kwa kuuliza maswali yasiyo na msingi na pia kuwasilisha pingamizi zinazopelekea shauri kuwa na mlolongo mrefu.
Dai la udhalilishwaji na kuitwa fisadi na Mnyika katika mkutano alioufanya kwenye kampeni ambapo alidai kuwa Ng’humbi aliuza nyumba ya Umoja wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi Tanzania (UWT), na kwamba watu wasichague CCM inakumbatia mafisadi.
Jaji Msuya alisema madai hayo kwa mujibu wa ushahidi wa mdai maneno hayo yaliongewa na Mnyika kwenye mkutano ambao ulikuwa na watu zaidi ya 500 lakini yeye hakuwepo hivyo mahakama haichukui maneno ya kuambiwa bali mtu aliyesikia mwenyewe au kushuhudia.
“hata hivyo katika watu wote hao 500 waliokuwa kwenye mkutano hakuja hata mtu mmoja kutoa ushahidi, na pia haikuthibitishwa ni namna gani iliathiri uchaguzi na hivyo hoja hiyo imeondolewa,” alisema Jaji Msuya.
Dai la Mnyika aliingia na wafuasi wengine wa CHADEMA kwenye kujumlisha matokeo, jaji huyo alisema kuwa ushahidi pekee ni wa mdai na kwamba hadhani kuwa ni jambo linalowezekana mtu asiyehusika kuingia katika chumba cha majumuisho ya kura wakati kulikuwa na ulinzi na kwamba wagombea wengine wangelalamikia jambo hilo hata hivyo mdai hakuleta mashahidi waliokuwa katika chumba hicho kutoa ushahidi kuwa kuna watu wasiohusika waliingia.
Aidha dai la msimamizi wa uchaguzi alitumia kompyuta ndogo (laptop) za Mnyika badala ya rasmi za tume ya uchaguzi na pia hazikukaguliwa na kwamba pengine kulikuwa na taarifa zisizo rasmi kwenye kompyuta hizo ikiwa ni pamoja na ongezeko lile la kura 14,000.
Jaji Msuya alisema kuwa kwa mujibu wa ushahidi hazikutumika kompyuta za mnyika na kwamba zilikuwa za mawakala na kwamba katika hili Mdai angeweza kuleta mashahidi zaidi kuthibitisha ikiwa ni pamoja na mkurugenzi wa uchaguzi.
.
Featured Post
NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...
