MAANDAMANO YA CHADEMA YAMTIKISA RC
JAMII 11:28 PM
SIKU moja baada ya wakazi wa manispaa ya Songea kufanya maandamano yaliyoongozwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuhusiana na tatizo la umeme, mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Saidi Mwambungu, ametembelea mitambo ya kufua umeme na kujionea kazi ya kutengeneza mitambo hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, alisema lengo la kutembelea mitambo hiyo ni kuondoa uvumi unaoenezwa na baadhi ya watu kuwa hakuna mashine iliyoletwa na Rais Jakaya Kikwete ndiyo maana kuna tatizo la umeme.
Mkuu huyo wa mkoa (RC), alisema mashine inayofanya kazi kwa sasa ni ile iliyoletwa na Rais ambayo ni mpya na inazalisha umeme wa megawati 1.9 na inasaidia kupunguza makali ya mgawo wa umeme.
Alisema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa Juni tatizo hilo litakuwa limekwisha, kwani mashine iliyotoka mkoani Mtwara na zile za zamani zitakuwa zimepona kutokana na kasi ya mafundi waliopo.
“Niwaombe wananchi wasiendelee kupewa taarifa zisizo sahihi kuwa Rais hajatekeleza ahadi yake ya kuleta jenereta mpya; si kweli, kwani umeme tunaoupata sasa ni wa jenereta hilo ambalo limeletwa kusaidia kupunguza makali ya mgawo,” alisema.
Pamoja na hayo, alilitaka Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kuweka utaratibu mzuri wa utoaji wa taarifa kwa wananchi badala ya kusubiri makao makuu watoe taarifa, kwani tatizo la Songea ni vema wananchi wakaelewa kupitia ofisi zilizoko mkoani hapa.
Kwa upande wake, mkurugenzi uzalishaji TANESCO, Boniface Njombe, alisema tatizo lililojitokeza wiki mbili zilizopita na kusababisha watu kuandamana lilitokana na kuishiwa mafuta kwa kuwa shirika hilo liliishiwa fedha za kumlipa mzabuni.
Alisema mahitaji ya mji wa Songea ni megawati 4.5, lakini kutokana na ubovu wa mashine umeme unaozalishwa kwa sasa ni megawati 2.6, jambo linalosababisha kuwepo kwa mgao mkali wa umeme.





