OFISA UBALOZI ATAKA KESI YA PROFESA MAHALU IFUTWE

ALIYEKUWA Ofisa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini Italia, Grace Martin ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu hakuisababishia Serikali hasara ya Euro2 milioni, bali alileta faida kwa taifa kwa kuwa na jengo zuri na kwamba anahitaji kupewa shukrani.
 
Profesa Mahalu na Grace wanakabiliwa na mashtaka sita likiwemo la uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya Euro 2,065,827.60.

Akiongozwa na Wakili Mabere Marando kujitetea dhidi ya tuhuma zinazomkabili jana mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu, Grace alidai kuwa kwa ufahamu wake, Balozi Mahalu hakuisababishia Serikali hasara kwa kuwa manunuzi yalileta faida na nchi kupata jengo zuri na hakuna fedha hazikupotea na anastahili shukrani.

“Mheshimiwa kwa ufahamu wangu, mashtaka yote sita yanayomkabili Balozi Mahalu hakuyatenda, aliwasilisha  mikataba miwili kama taarifa iliyofanyika kihalali,” alidai Grace.

Aliendelea kuiomba mahakama itupilie mbali tuhuma hizo  na kwamba madai ya kuwa Balozi Mahalu alitumia risiti ya ununuzi wa jengo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia kuidanganya Serikali kuwa mwenye nyumba amelipwa fedha siyo ya kweli.

Hata hivyo, akiongozwa na Wakili Marando, Grace alihoji ni kwanini upande wa Jamhuri haukumleta mmiliki wa jengo hilo la ubalozi wa Tanzania nchini Italia kukana risiti hiyo au Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hossea na Fungo  kuulizwa juu ya ununuzi wa jengo hilo kwa sababu walikwenda nchini humo kufanya uchunguzi.

Wakili Marando aliiomba mahakama wawasilishe hoja zao kama washtakiwa wana hatia au la kwa njia ya mdomo ndipo wakili wa Serikali, Ponziano Lukosi alipendekeza ziwasilishwe kwa njia ya maandishi.

Hakimu aliwaeleza hadi Mei 16, mwaka huu atakuwa amekwisha wapa pande zote mbili mwenendo wa Kesi ili waweze kuandaa hoja hizo.

Utetezi huo wa mtuhumiwa huyo umekuja siku moja baada ya Rais mstaafu, Benjamin Mkapa kupanda kizimbani hapo na kutoa ushahidi wake huku akimtetea Mahalu kwamba ni mtu mwadilifu.
Pia Mkapa alisema yeye ndiye aliyeagiza kununuliwa kwa jengo hilo la ubalozi na ilikuwa ni muhimu lipatikane na kuongeza kwamba, alishangaa Mahalu kushitakiwa.

Chanzo: Mwananchi

Posted by Bigie on 11:25 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.