WAZANZIBAR WACHARUKA, WAIGOMEA TUME YA KATIBA


WANANCHI wa Visiwa vya Zanzibar wamekuja juu na kudai kuwa hawatatoa tena maoni yao mbele ya Tume ya Kukusanya Maoni ya Jaji Joseph Warioba wakipinga kile walichodai kuzuiwa na hatimaye kukamatwa kwa wananchi 12 wa kisiwa cha Pemba, waliotaka kujadili masuala ya Muungano.

Kwa pamoja Baraza la Katiba la Zanzibar pamoja na Jukwaa la Katiba wamesema kamati teule ya kukusanya maoni kwa ajili ya uundwaji wa Katiba mpya inayoongozwa na Jaji mstaafu Joseph Warioba imevunja Katiba ya nchi kwa kuwatisha wananchi hao ambao wanataka kutoa maoni yao kuhusiana na jambo hilo.

Wakizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Deus Kibamba na wa Baraza la Katiba Profesa Abdul Sheriff walisema kitendo cha kuwazuia baadhi ya wananchi wa Pemba kuingia kwenye mkutano wa kutoa maoni ni ukiukwaji wa Katiba ya nchi.

Profesa Sheriff alisema Tume ya Jaji Warioba ikitumia vyombo vya dola imewatia mbaroni wananchi 12 waliofurahia haki yao ya uhuru wa maoni kwa mujibu wa ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar ya mwaka 1984.

“Tumefedheheshwa na kitendo cha vitisho cha vyombo vya dola dhidi ya wote wenye mawazo tofauti kuhusu uwepo wa Muungano au aina ya muungano unaohitajika,” alisema profesa huyo.

Akifafanua vitisho vilivyotolewa na viongozi mbalimbali wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mwenyekiti wa Baraza hilo alinukuu kauli ya Rais wa visiwa hivyo Dk. Ali Mohamed Shein akiwataka wananchi walioichoka amani waondoke Zanzibar.

Alisema kauli zenye vitisho vya aina hiyo zimewahi kutolewa pia na Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Dadi Faki Dadi aliyepiga marufuku mihadhara ya wananchi kuhusu Katiba na wakazi wa Machomanne kuzuiwa na jeshi la polisi kukutana ili wajadili katiba.

“Kwa sababu hizo Wazanzibari hatuna haja ya kuzungumzia katiba ambayo haituhusu. Zanzibar na Tanganyika ziliungana sasa tusipozungumzia Muungano tutakua tunachezeshwa ngoma isiyotuhusu,” alisisitiza Profesa Sheriff.

Pamoja na tishio la kutochangia maoni, wamemtaka Mwenyekiti wa Tume ya kukusanya maoni ya Katiba mpya Jaji mstaafu Joseph Warioba kufafanua kauli yake ya kukataa shinikizo kwenye utendaji wa kamati hiyo.

Kwa upande wake Kibamba alisema tume ya Jaji Warioba haiwezi kuendelea na kazi kwa sasa hadi baadhi ya vipengele kwenye sheria ya mabadiliko ya katiba mpya viwekwe sawa.

Kibamba alivitaja vipengele vinavyominya uhuru wa wananchi ni kile cha 18(6) kinachoitaka tume hiyo kutoruhusu asasi, taasisi au makundi ya watu kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wake kutoa maoni na 21(1)-(4) kinachotamka makosa mbalimbali na adhabu zake kifutwe chote kwa sababu hakina nia nzuri na kwamba kukitokea wahalifu wakati wa mchakato huo sheria nyingine za nchi zitatumika.

“Kwa hali hiyo kifungu hiki kinatishia wananchi na kitawafanya wengi wao wasishiriki katika kutoa elimu, maoni au mawazo kwa kuogopa kifungo cha kati ya mwaka mmoja na mitatu jela au faini kati ya sh milioni mbili na milioni tano au vyote pamoja,” alisisistiza Kibamba.

Awali aliwaomba wabunge na wawakilishi kuvifanyia marekebisho na kukiondoa kabisa kifungu cha 21 (1)-(4) kabla ya kuanza kujadili bajeti ya mwaka 2012/2013 ili kuiruhusu kamati ya kukusanya maoni ianze upya kazi zake bila kuvunja Katiba ya nchi.

Posted by Bigie on 5:56 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.