JK aaga Watanzania ughaibuni


RAIS Jakaya Kikwete ameendelea kuaga Watanzania kila anapopata fursa ya kukutana nao, huku mafanikio ya miaka kumi ya uongozi wake yakijidhihirisha katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambako Bajeti ya Serikali kupitia wizara mbalimbali imekuwa ikijadiliwa na kupitishwa.
 
Mwishoni mwa wiki hii akiwa jijini Stockholm nchini Sweden alikokwenda kwa ziara ya siku tatu, ambayo pia ni ya kwanza ya kuaga nchi wahisani, Rais Kikwete alikutana na Watanzania waishio nchini humo, ambako kabla ya kuwaaga, alielezea changamoto anazoziacha.
 
Rais Kikwete katika mazungumzo hayo, amesema Rais ajaye anakabiliwa na changamoto ya kuhakikisha Tanzania inayoundwa na Muungano wa nchi mbili, inaendelea kuwa moja kwa kudumisha umoja wa Watanzania na amani.
 
“Hapa tulipofikia lazima tuhakikishe Taifa linakuwa moja, kuna vyama na makabila mbalimbali, lakini lazima tuhakikishe nchi inabaki moja,” amesisitiza Rais Kikwete.
 
Rais Kikwete pia alielezea matumaini yake kuwa Tanzania itapata kiongozi mzuri na kuelezea mafanikio ambayo Serikali yake imeyapata na kutumaini kuwa yatadumishwa na kuendelezwa na Rais ajaye.
 
Uchumi Awali akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika uchumi alipokutana na Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven, Rais Kikwete alisema uchumi wa Tanzania umekua kwa wastani wa asilimia 7, katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.
 
Mbali na kukua kwa uchumi wastani, pato la Taifa limekua kwa zaidi ya mara tatu, kutoka Dola za Kimarekani bilioni 14.4 hadi kufikia Dola bilioni 49.2 za Marekani.
 
Aidha, pato la mtu mmoja mmoja kwa mwaka 2005, wakati Rais Kikwete alipokuwa akiingia madarakani lilikuwa Dola za Marekani 375, lakini mwaka jana lilifikia Dola za Marekani 1,038.
 
Mafanikio hayo kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, zilisababisha Waziri Mkuu wa Sweden, Lofven, kuona umuhimu wa kuanzisha awamu nyingine ya uhusiano katika maendeleo, utakaoleta maana zaidi.
 
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo Sweden (SIDA), Torbjorn Pettersson, ambaye pia alikutana na Rais Kikwete, alieleza kuwa Sweden imeridhishwa na kiwango cha maendeleo na juhudi za kupunguza umaskini nchini Tanzania.
 
Hata hivyo, Rais Kikwete alipokuwa akizungumzia kasi ya kuondoa umasikini, alisema bado juhudi za kuondosha umaskini zinahitajika na zitafanikiwa kwa kuelekeza nguvu kwenye kilimo, ambacho ndicho kinachoajiri na kutegemewa na Watanzania wengi zaidi hasa wanaoishi vijijini.
 
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Sweden, Urban Ahlin, pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini humo na kushukuru kwa misaada ya maendeleo kwa takribani miaka 50 sasa.
 
Viongozi hao wamempongeza Rais kwa kufanya ziara ya shukrani na kuwaaga, kwani ni mara chache kwa viongozi wengi wa Kiafrika kuaga na kuondoka madarakani.
 
Mbali mazungumzo hayo ya Sweden, mafanikio mengine ya Serikali kwa miaka 10 iliyopita, kwa wiki ya tatu sasa yamegeuka nguzo mbuhimu ya kutetea bajeti za wizara mbalimbali bungeni na katika warsha mbalimbali.
 
Afya Kwa mfano katika wiki hii katika sekta ya afya, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alipokuwa akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, aliwataka kusoma takwimu za mafanikio ya Tanzania ikilinganishwa na nchi zingine badala ya kuishia kusoma bajeti ya sekta hiyo pekee.
 
Kwa mujibu wa Dk Rashid, pamoja na Tanzania kuwekeza asilimia 2.8 tu ya pato la Taifa katika sekta ya afya, vifo vya watoto chini ya miaka mitano vimepungua na mafanikio hayo ni makubwa kuliko katika nchi zinazoonekana kupiga hatua zaidi katika uwekezaji huo.
 
Alitaja nchi ya Botswana yenye uwekezaji wa asilimia 3 ya pato la Taifa katika afya na Zambia yenye asilimia 4.2 ya pato la Taifa katika sekta hiyo, kwamba mataifa hayo katika kila vizazi hai 1,000 wamekuwa wakipoteza watoto wengi zaidi.
 
Wakati Tanzania ikipoteza watoto 52 katika kila watoto hai 1,000 wanaozaliwa, Kenya wao wanapoteza watoto 71, Zambia watoto 87 na Cameroon ni watoto 95 katika kila vizazi haivyo 1,000.
 
Umeme Katika upatikanaji wa huduma za nishati na umeme, mpaka mwaka jana, Serikali ilikuwa imefikisha umeme kwa zaidi ya asilimia 35 ya Watanzania, kutoka asilimia wastani wa chini ya asilimia 15 iliyokuwepo mwaka 2005.
 
Akizungumza bungeni jana, Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene alisema idadi ya wateja waliounganishiwa umeme vijijini imefikia asilimia 68. Idadi hiyo imeongezeka kutoka 143,113 mwaka 2013 hadi kufikia wateja 241,401 Aprili mwaka huu.
 
Alisema wateja hao wameunganishiwa umeme kupitia miradi ya Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
 
Bomba la gesi Akizungumzia jitihada za kuanza kutumia hazina ya gesi asilia kwa ajili ya kuzalisha umeme badala ya mafuta mazito yanayosababisha umeme uwe bei ghali nchini, Simbachawene alisema mitambo ya kusafisha gesi asilia na bomba la gesi asilia, vitaanza kazi rasmi Septemba mwaka huu.
 
Alisema ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara kupitia Lindi hadi Dar es Salaam umekamilika, ujenzi wa mitambo ya kusafirisha gesi asilia katika eneo la Madimba, Mtwara umefikia asilimia 99 na mitambo ya Songo Songo, Lindi nao umefikia asilimia 99. “Mitambo na bomba hilo vitaanza kufanya kazi (Commercial Operational Date) Septemba 2015.
 
“Haya ni matokeo ya utekelezaji wa miongoni mwa miradi iliyoanishwa kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16),” alisema Simbachawene.
 
Alisema matumizi ya gesi asilia yatachochea ukuaji wa viwanda, utunzaji wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kuongeza ajira na hatimaye kuleta maendeleo ya uchumi na kijamii kwa ujumla.
Elimu Katika elimu, mwaka 2005 wakati Rais Kikwete akiingia madarakani, Bajeti ya Serikali katika sekta hiyo ilikuwa Sh bilioni 600, lakini mwaka jana ilifikia Sh trilioni 3.4.
 
Sababu ya uwekezaji huo mkubwa, Rais Kikwete aliwahi kusema alipoingia madarakani, alikuta Tanzania yenye watu wengi zaidi katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iko nyuma ikilinganishwa na Kenya na Uganda, kwa idadi ya wanafunzi waliokuwa wakisoma shule za sekondari na vyuo.
 
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mwaka 2005 wanafunzi waliokuwa wakisoma sekondari ni zaidi ya 500,000, wakati nchini Uganda waliokuwa wakisoma sekondari walikuwa zaidi ya 700,000 na Kenya zaidi ya 900,000.
 
Kwa upande wa vyuo vikuu, Tanzania ilikuwa na wanafunzi 40,000 tu wakati Uganda ilikuwa na wanafunzi 124,000 na Kenya 180,000.
 
Hatua zilizochukuliwa, Rais Kikwete alisema Serikali kwa kushirikiana na wananchi, waliamua kujenga shule za sekondari za kata, ambapo wananchi walihamasishwa, wakahamasika wakajenga shule mpaka Mkurugenzi mmoja wa elimu, akahofia kukosa walimu wa kupeleka katika shule hizo.
 
Kwa sasa Tanzania ina wanafunzi 1,800,000 wanaosoma sekondari na imeshaipita Uganda yenye wanafunzi 1,700,000 wanaosoma elimu ya sekondari, lakini imezidiwa na Kenya ambayo ina wanafunzi 2,100,000.
 
Hata hivyo alisema ni rahisi kuipita Kenya kwa hilo pengo la wanafunzi 300,000, kwa kuwa shule za sekondari zilizopo zina nafasi ya kuongeza wanafunzi milioni mbili zaidi.
 
Kwa upande wa elimu ya juu, Rais Kikwete alisema vyuo vikuu vimeongezeka kutoka 26 mwaka 2005 hadi kufikia 52 na idadi ya wanafunzi walio katika vyuo vikuu ilitoka 40,719 hadi kufikia 200,956.
 
Hata bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh bilioni 56.1 hadi Sh bilioni 345 mwaka 2014.

Posted by Bigie on 1:46 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.