BABU WA LOLIONDO HUENDA AKAKABILIWA NA KIFUNGO CHA MIAKA 7 JELA....
JAMII 10:59 PM
Mchungaji Ambilikile Masapile ‘Babu Ambi’ wa Samunge, Loliondo, Arusha, atapanda kizimbani kukabili kesi za madai na jinai, hii ni kwa mujibu wa wakili maarufu, Mabere Nyaucho Marando.
Wakili huyo alisema, endapo mahakama itamkuta na hatia ya kutenda jinai, Babu Ambi, anaweza kuhukumiwa kifungo kisichopungua miaka saba jela.
Marando alisema, kesi ya jinai ambayo Babu Ambi anafunguliwa ni ile ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kwamba aliwahadaa watu kuwa dawa yake inatibu, wakati hakuna mtumiaji aliyepona.
Aliongeza kuwa kesi ya madai, inafunguliwa kwa sababu anatakiwa alipe fidia za watu waliopoteza maisha na wote waliosafiri kutokana sehemu mbalimbali wakitumia gharama kubwa kwa dawa isiyotibu.
Marando alifafanua, Babu Ambi, anaweza kukumbana na kifungo hicho endapo atakutwa na hatia kutokana na sheria ya jinai namba 302.
“Nipo makini na suala hili, hawezi kupona, nitasimamia kesi na tutamfunga,” alisema Marando na kuongeza:
“Nina taarifa nyingi kuhusu watu waliokufa, hakuna aliyepona.
Mazingira ya kisheria, yanatoa picha rahisi kuwa Babu atakutwa na hatia.”
Kutokana na msimamo huo, Marando aliwataka wale wote waliotibiwa na Babu Ambi lakini hawakupona, waende kwake kwa sababu amedhamiria kuisimamia kesi hiyo.
“Kiukweli babu aliwadanganya watu kuwa anatibu magonjwa sugu, lakini watu walipokwenda na kupata kikombe, hawakupona, na hawezi kuthibitisha mahakamani kuwa dawa yake imethibitishwa na serikali kuwa inatibu magonjwa aliyoyasema,” alisema Marando.
Aliongeza kuwa yupo tayari kuandaa kesi hizo na ndugu wote waliokunywa dawa na hawakupona, wanaweza kwenda kwake ili wakusanye ushahidi wa kutosha.
“Ni jambo linaloumiza, nitasimamia kesi hiyo na nitahakikisha anafungwa si chini ya miaka saba kama sheria inavyosema...ama zake ama zetu, alisababisha wagonjwa wa Ukimwi kuacha kutumia ARV, wengine wakatoroka hospitalini kwenda kwake na wengi wamepoteza maisha,” alisema Marando.
Wakili huyo aliigeukia serikali na kuilaumu kwa kumruhusu Babu kuwapa dawa watu wakati ikijua kuwa ilikuwa haijafanyiwa majaribio ya kitaalamu kujua kuwa kama inatibu au la.
Alisema anaweza kumfungulia kesi ya madai mchungaji huyo kwa kuwa wagonjwa wengi waliuza mali au kuchukua akiba zao na kusafiri hadi Samunge wakijua kuwa watapona baada ya kunywa dawa yake.
“Badala ya kupona wengi walifariki dunia huku wengine wakibaki masikini na hawajapona kutokana na udanganyifu mkubwa uliofanywa na Babu huyo na sasa hawawezi tena kupata mali nyingine,” alisema Marando.
Mwanasheria mwingine, Dk. Ngali Maita alipohojiwa kwa simu alisema atakuwa tayari kumsaidia mawazo ya kisheria Marando ikiwa atahitajika kwa kile alichodai, Babu alidanganya watu kuhusu tiba ya kikombe.
“Ni kitu kibaya sana alifanya Babu wa Loliondo, amesababisha maafa makubwa kwa jamii na mbaya zaidi hadi sasa uchunguzi wa dawa yake upo gizani, serikali haisemi chochote licha ya kuahidi wananchi kuwa watataarifiwa… hii ni mbaya na ni hatari,” alisema Dk. Ngali.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Waganga wa Tiba Asilia jijini Dar es Salaam, Maneno Tamba alisema alishangazwa sana na serikali kumruhusu Babu kufanya tiba bila kufuata sheria ya tiba asili ya mwaka 2002.
“Sifa za kutibu kiasili zimebainishwa na sheria, kwamba pamoja na sheria nyingine mtoa dawa ni lazima awe chini ya mganga wa jadi kwa miaka mitatu ndipo anaweza kusajiliwa.
Je, Babu alisajiliwa? Inafaa ashitakiwe,” alisema Tamba.
Babu wa Loliondo alijipatia umaarufu mapema mwaka huu baada ya kutangaza kwamba amezungumza na Mungu kwenye ndoto na kumuonesha dawa inayoitwa Mugariga inayotibu Ukimwi, Kisukari, Moyo, Kifafa na magonjwa mengine sugu.
Mchungaji Masapila alisema dawa yake ambayo ni dozi ya kikombe kimoja ilikuwa na gharama ya shilingi 500, hali iliyofanya maelfu ya watu wakiwemo mawaziri, wabunge na wafanyabiashara kwenda kwake huku wakitumia magari na wengine kukodi helikopta.
Hivi sasa idadi ya wagonjwa wanaokwenda kutibiwa huko ni ndogo sana na Babu anadai hali hiyo imetokana na kupigwa vita na baadhi ya viongozi wa dini na waganga wa jadi.