MKUU WA MKOA WA KILIMANJARO AWAPONGEZA TPC KWA KUJENGA UKUMBI WA KISASA
JAMII 11:07 PM
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Leonidas Gama akizindua ukumbi mpya wa kisasa katika kiwanda cha sukari cha TPC mjini Moshi hivi karibuni.
Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Leonidas Gama akiwa ameambatana na mkuu wa wilaya ya Moshi ,Musa Samizi (mwenye suti nyeusi) wakipata maelezo kutoka kwa Afisa mtendaji mkuu wa kiwanda cha sukari cha TPC,Robert Baisaac kati yao.
Afisa mtendaji wa utawala wa TPC,Jafary Ally akizungumza wakati wa ufunguzi wa ukumbi huo.
Baisaac akionesha ngao na cheti vilivyokabidhiwa kwake kutoka PPF kwa kuwa washindi wa kwanza.
Afisa mtendaji mkuu wa TPC ,Baisaac akiteta jambo la mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro,Leonidas Gama.
Baadhi ya Wastaafu wa kiwanda cha sukari cha Tpc mwaka 2011wakiwa katika ukumbi huo ambapo pia walifanyiwa sherehe ya kuagwa.
Ukumbi uliofunguliwa katika kiwanda cha sukari cha TPC unavyoonekana kwa ndani.
SERIKALI mkoani Kilimanjaro imesema itahamishia mikutano yake yote mikubwa katika ukumbi mpya wa kisasa uliojengwa katika kiwanda cha sukari cha TPC kutokana na hali ya utulivu iliyopo katika eneo hilo.
Kauli hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama wakati wa ufunguzi wa ukumbi wa TPC ,ulioenda sanjari na sherehe ya kuwaaga wastaafu wa kiwanda hicho wa mwaka 2011.
Gama alisema kukamilika kwa ujenzi wa ukumbi huo wenye uwezo wa kuchukua watu 1200 utasaidia watu binafsi ,makampuni na taasisi mbalimbali kufanyia mikutano yao mikubwa kutokana na ukumbi huo kujitoshereza kwa kila kitu.
“Niwapongeze waliobuni wazo la kuwa na ukumbi wa kisasa kama huu…hatukujua mapema majuzi waziri mkuu amekuja kututembelea tukalazimika kwenda kubanana katika ukumbi mdogo ,lakini tungejua mapema tungemleta waziri mkuu kufanyia mkutano wake hapa”alisema Gama.
Alisema mbali na mikutano ukumbi huo pia utaweza kutumika kwa ajili ya burudani kwa viongozi ambao wangependa kucheza dansi wakati mwingine lakini wamekuwa wakishindwa kufanya hivyo kutokana na kwamba kulikuwa hakuna ukumbi ambao ungewawezesha na wao kupata burudani.
“Wakati mwingine viongozi pia wanataka kujitikisa kidogo lakini walifikiri wapi waende,ukienda kujichanganya kwenye kumbi zetu za mjini,wataulizana hee na huyu nae vipi ?sasa tutaweza kuja hapa mara moja moja”alisema Gama
Kwa upande wake afisa mtendaji mkuu wa TPC ,Robert Baisaac alisema uwepo wa jengo hilo utaongeza ubora wa maisha ya wakazi wa TPC,vijiji jirani na mji wa Moshi kwa kutumia ukumbi huo kwa matukio tofauti yatakayofanyika katika ukubi huo.
“Tutapenda kuona jengo hili likitumika kwa burudani kila wiki,tutapenda kuona matamasha,sanaa za maonesho ,muziki,ngoma za utamaduni,maonesho ya sinema yakifanyika hapa”alisema Baisaac.
Alisema ukumbi huo ni mfano hai wa kuwa wanahisa na bodi ya wakurugenzi wanathamini ustawi wa wafanyakazi wao ikiwa ni pamoja na kuboresha mazingira ya TPC kwa manufaa ya wafanyakazi.
Ujenzi wa ukumbi huo uliogharimu zaidi ya shilingi milioni 500 ulianza Februari 21 mwaka huu chini ya mkandarasi Kalsi & Jutley Enterprises na kukamilika Novemba 19 mwaka huu.