MAHAKAMA KUU YAAMURU "DAVID KAFULIA" AENDELEE KUWA MBUNGE MPAKA HAPO KESI YA MSINGI ITAKAPOSIKILIZWA


Mahakama Kuu Dar es Salaam, imeamuru Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, kuendelea na wadhifa wake wa ubunge hadi hapo kesi yake ya msingi itakaposikilizwa.

Hivi karibuni, Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi, ilimfukuza Kafulila uanachama, uamuzi ambao unamuondolea sifa ya kuwa mbunge.

Hata hivyo, kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu jana, Kafulila ataendelea kushikilia nafasi yake ya ubunge mpaka hapo kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa hukumu.

Uamuzi huo wa mahakama, umefuatia kesi iliyofunguliwa na Kafulila, kupinga uamuzi wa Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi wa kumvua uanachama na kumuondolea sifa ya kuendelea kuwa mbunge.

Kafulila alipozungumza na mwandishi wetu alisema kuwa Mahakama Kuu itakaa Februari mwakani na kupanga kuanza kusikiliza kesi hiyo.

“Namshukuru Mungu, siku zote Mungu yupo pamoja na wanyonge. Bado nasimamia ukweli kwamba kikao cha Halmashauri Kuu ya NCCR-Mageuzi kilichoamua, kilikiuka sheria na taratibu. Hata hivyo, suala hili lipo mahakamani, tuache mahakama itaamua,” alisema Kafulila.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, amepongeza uamuzi wa mahakama na kueleza kwamba ni mpango wa Mungu kumtetea mnyonge.

Zitto, aliandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Kijamii, Facebook jana saa 9:40 alasiri: “Kafulila kuendelea na ubunge. Mahakama Kuu imetoa amri muda mfupi uliopita. Ataendelea kuwa mbunge mpaka hapo kesi ya msingi itakapokwisha. Mungu yupo pamoja na wanyonge siku zote.”

Posted by Bigie on 9:56 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.