RAIS KIKWETE AOMBOLEZA MAAFA YA MAFURIKO DAR ES SALAAM
JAMII 10:42 PM
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mheshimiwa
Said Meck Sadiq kuomboleza vifo vya watu 13 ambao wamepoteza maisha katika mafuriko makubwa yaliyotokana na mvua ambazo zimekuwa zinanyesha tokea jana, Jumanne, Desemba 20, 2011.
Aidha, Rais Kikwete amempa pole Mkuu huyo wa Mkoa kutokana na uharibifu mkubwa wa nyumba, makazi na mali nyingine za wananchi uliosababishwa na mvua hizo ambazo pia zimesababisha uharibifu wa miundombinu.
Rais Kikwete pia ameuelekeza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kusaidiana na taasisi na vyombo vyenye uzoefu wa maafa kushirikiana katika kuendelea kuokoa maisha ya watu, kusaidia waliozingirwa na mafuriko na kuwahifadhi na kuwasaidia wale wote waliopoteza nyumba na makazi kutokana na mafuriko hayo.
Katika salamu zake, Rais Kikwete amemwambia Mheshimiwa Sadiq: “Nimepokea kwa masikitiko habari za vifo vya wenzetu 13 ilivyotokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa ambayo sote tumeishuhudia katika Mkoa wa Dar es Salaam tokea jana.
Amesema: “Nakutumia wewe rambirambi zangu kutokana na vifo hivyo, na kupitia kwako kwa familia, ndugu na jamaa waliopoteza wapendwa wao katika balaa hili la mafuriko. Wajulishe kuwa msiba wao ni msiba wangu, naelewa machungu yao na niko nao katika hali ya sasa ya maombolezo. Mungu aziweke pema peponi roho za marehemu wote.”
Ameongeza Rais Kikwete: “Napenda pia kupitia kwako kutoa pole zangu nyingi kwa wote walioumia ama kupoteza mali zao katika mafuriko haya. Wajulishe kuwa moyo wangu uko nao wakati huu wa mazingira magumu.
“Chini ya usimamizi wako, ningependa kuona uongozi wa Mkoa kwa kushirikiana na taasisi na vyombo vyenye ujuzi na uzoefu wa kupambana na majanga na dharura za namna hii, kuhakikisha kuwa tunaendelea kuokoa watu ambao badowamezingirwa na mafuriko, tunawapa matibabu wale walioumia katika mafurikohayo, na tunawahifadhi na kuwapa huduma za kibinadamu wote waliopoteza nyumba na makazi yao katika mafurikio hayo.”
IMETOLEWA NA:
KURUGENZI YA MAWASILIANO YA RAIS IKULU
DESEMBA 21, 2011
DAR ES SALAAM