Bohari ya Madawa Tanzania, MSD lawamani Korogwe, Tanga


BAADHI ya waganga na wauguzi kwenye zahanati na vituo vya afya wilayani Korogwe mkoani Tanga wamelalamikikia Bohari ya Dawa nchini (MSD) kuwa inawatafutia 'kesi' kwa wananchi, kwani madereva wa idara hiyo waliopewa kazi ya kusambaza 'huwatupia' dawa hizo waganga na wauguzi bila wajumbe wa Kamati ya Usimamizi wa zahanati husika.

Walitoa lalamiko hilo juzi jana kwa nyakati tofauti kwa wajumbe wa Bodi ya Afya ya Wilaya ambao wanafanya ziara ya siku saba kutembelea zahanati, hospitali na vituo vya afya vyote vilivyopo kwenye wilaya hiyo ili kuona changamoto na utekelezaji wa utoaji huduma kwa wananchi.

Mganga wa Zahanati ya Kerenge iliyopo Tarafa ya Magoma Dkt. Saleh Hussein alisema magari ya MSD tena yakiwa na madereva tu, wamekuwa wanawaletea, wanapoambiwa ngoja tuwatafute wajumbe wa Kamati ya Usimamizi ya Zahanati ama Kituo cha Afya wanasema wanaharaka.

"Zamani walikuwa wanakubali tunamuita mjumbe angalau mmoja wa kamati, lakini sasa hivi wanasema wana haraka. Tena sasa hivi ambapo gari linakuja na dereva tu, wanafungua kabisa boksi la dawa na kunipa listi ya dawa, lakini kwenye jamii hilo
hawawezi kulikubali" alisema Bw. Hussein.

Mganga wa  Zahanati ya Kwemazandu iliyopo kata ya Magoma Bi. Zuhura Akida alisema picha kwa ajili ya kitambullisho cha Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) zinakwamisha zoezi hilo, kwani wananchi wengi wapo tayari kuchangia sh. 5,000 kwa ajili ya tiba ya familia ya watu sita, lakini gharama za picha ni kikwazo.

"Kama mpango wa kuwapiga picha wanawake wajawazito kwa ajili ya kulipiwa bure matibabu na Mfuko wa Taifa wa Bima ya afya (NHIF) pia utawapiga picha bure wanaojiunga na CHF, wanachama wangeongezeka kwani wanaona kupiga picha ni gharama kuliko kulipia matibabu" alisema Bi. Akida.

Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi ya Zahanati ya Kerenge aliwataka Bima ya Afya ambao wamejitwisha 'msalaba' wa CHFkufanya kampeni za kijiji hadi kijiji kuwawezesha wananchi kujiunga na mfuko huo, kwani bado hawaamini kama kwa sh. 5,000 wanaweza kutibiwa bure, wakati wenye fedha zao wakienda kwenye zahanati wakati mwingine wanakosa dawa.

Mjumbe wa Bodi ya Afya ambaye pia ni Mratibu wa mifuko ya NHIF na CHF Wilaya ya Korogwe Bi. Judith Malya aliwatahadharisha waganga na wauguzi kuacha kupokea dawa bila ushahidi wa wajumbe wa kamati, huku akidai hao madereva wa MSD wanalipwa posho na mishahara  kwa kazi hiyo.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Korogwe Dkt. Rashid Said aliwaasa wajumbe hao kwenda kuangalia changamoto wanazokutana nazo wagonjwa na watumishi wa afya kwenye maeneo husika ili yaweze kupatiwa ufumbuzi, ikiwa ni pamoja na kuangalia hali ya chanjo, mifuko ya CHF, mradi wa mama wajawazito na miundombinu ya zahanati na vituo cha afya.

---
via blogu ya Nyakasagani

Posted by Bigie on 9:10 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.