Polisi Achomwa Mkuki Ubavuni
news 5:56 PM
POLISI wa kituo cha Kinesi wilayani Rorya mkoani Mara, Konstebo Deogratius amejeruhiwa kwa kuchomwa mkuki ubavuni.
Alichomwa
mkuki wakati akiwa na wenzake walipokuwa wakipambana kujaribu kuwaondoa
zaidi ya watu 2,000 waliovamia mgodi wa dhahabu wa kampuni ya Acacia wa
North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime.
Askari huyo mwenye namba G 7606 amelazwa katika Hospitali ya Shirati akitibiwa jeraha hilo.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa alisema
kuwa kutokana na uvamizi huo, polisi inawashikilia watu sita
wanaotuhumiwa kuingia ndani ya mgodi na kujeruhi baadhi ya askari
akiwamo huyo aliyechomwa mkuki kwa lengo la kuiba mawe ya dhahabu.
Kamanda
huyo alibainisha kuwa watu hao zaidi ya 2,000 waliingia ndani ya mgodi
huo, saa 7:00 mchana wakiwa na silaha za jadi kama vile mapanga,
mishale, mikuki na marungu.
“Waliingia
ndani ya mgodi na kuanza kufanya vurugu kwa kuwashambulia askari na
walinzi waliokuwa wakilinda mgodi huo kwa nia ya kutaka kupora mawe ya
dhahabu,” alisema na kuongeza:
“Askari wetu wa Jeshi la Polisi wakishirikiana na walinzi wa mgodi huo waliwazuia wavamizi hao kwa kurusha mabomu ili wasiingie kupora mali.
“Askari wetu wa Jeshi la Polisi wakishirikiana na walinzi wa mgodi huo waliwazuia wavamizi hao kwa kurusha mabomu ili wasiingie kupora mali.
“Walijitahidi
kupambana na kundi hilo la wavamizi hao na kufanikiwa kuwaondoa ndani
ya mgodi huo, lakini askari wetu PC Deogratius aliyekuwa katika
operesheni hiyo alijeruhiwa na mkuki ubavuni”.
Alisema
alikimbizwa kupatiwa matibabu ya awali katika Hospitali ya Wilaya
Tarime na kwa sasa amehamishiwa kupata vipimo vya x-ray katika Hospitali
ya Shirati wilayani Rorya ambapo anaendelea na matibabu.
Alisema
watu sita wanaoshikiliwa na polisi wanatarajiwa kufikishwa mahakamani
wakati wowote kujibu tuhuma za kuvamia na kuingia ndani ya mgodi bila
idhini wakiwa na lengo la kufanya uhalifu na kujeruhi askari.