GARI LA KIGOGO MKWEPA KODI LADAKWA NA POLISI
JAMII 10:42 PM
Gari lenye namba T 637 ADA aina ya Toyota Land Cruiser, la Coleman Mushi, linalodaiwa kukwepa kulipa kodi tangu Juni 2010, likiwa kituo cha polisi makao makuu Dar es Salaam jana (Ijumaa) mchana kabla ya kurejeshwa kwa mmiliki wake jioni.
GARI la kigogo mmoja anayefanya kazi Mamlaka ya Bandari Tanzania (THA), Coleman Mushi, linalodaiwa kukwepa kulipa kodi, limetiwa mbaroni na polisi.
Gari hilo lilikamatwa kutokana na mtego wa polisi wa usalama barabarani kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) waliodokezwa hila la kigogo huyo kwa barua ambayo nakala yake ilipelekwa kwa Kamishna Mkuu wa TRA, Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohamed Mpinga na Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Said Mwema.
Kwa mujibu wa barua ya Oktoba 4 mwaka huu, iliyoandikwa na mkazi wa Dar es Salaam, George Joseph kwenda kwa Kamishna Upelelezi wa Kodi - TRA, gari hilo lenye namba T 637 ADA aina ya Toyota Land Cruiser, linadaiwa kukwepa kulipiwa kodi tangu Juni 2010.
Barua hiyo ilieleza kuwa mmiliki wake hajawahi kulipa kodi ya leseni ya kuliruhusu kutembea barabarani na amekuwa akiliendesha kila siku huku kutoka Gongo la Mboto akapoishi kwenda maeneo mbalimbali Dar es Salaam, akidai yeye ni Ofisa wa Usalama wa Taifa.
Kwa mantiki hiyo, amekuwa akiikosesha mapato Serikali kwa vile gari hilo licha ya kutokuwa na kibali cha kutembea barabarani, pia halina bima na hata mmiliki hana leseni ya kuendesha gari.
SOURCE: KWANZA JAMII






