TWANGA PEPETA WATANGAZA TAREHE YA UZINDUZI WA ALBUM YAO YA 11


Kampuni ya African Stars Entertainment imeandaa tamasha kubwa la burudani kwa jili ya kusherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania Bara na Uzinduzi rasmi wa Albamu ya 11 ya Bendi yake ya African Stars "Twanga Pepeta".

Tamasha hilo linataraji kuwahusisha wasanii wa fani mbalimbali za Muziki wa hapa nchini na kutoka nje ya nchi. Fani zitakazohusishwa ni pamoja na Taarab, Muziki wa Kizazi kipya na Muziki wa Dansi na msanii mmoja kutoka Nchini Kenya ambaye bado uongozi wa ASET unaendelea kufanya naye mazungumzo.

Tamasha hilo la uzinduzi linataraji kufanyika katika viwanja vya Leaders Club vilivyopo maeneo ya Kinondoni Jijini Dar es salaam siku ya Jumapili ya tarehe 09-11-2011 kuanzia saa sita za mchana.

Albamu itakayozinduliwa bado haijapatiwa jina ila nyimbo zilizopo kwenye albamu hiyo ni pamoja na "Mapenzi hayana Kiapo" utunzi wake Saleh Kupaza, "Penzi la Shemeji" utunzi wake Mwinjuma Muumini au Kocha wa Dunia, "Umenivika umasikini" utunzi wake Luizer Mbutu, "Dunia Daraja" utunzi wake Charlz Baba, "Mtoto wa Mwisho" utunzi wake Dogo Rama na nyimbo ya mwisho ni "Kauli" iliyotungwa na Rogart Hegga.

Nyimbo zote zimesharekodiwa katika CD kwenye studio ya Metro chini ya Mtengenezaji Allen Mapigo na nyimbo tatu zinatamba redioni na kwenye stesheni za redio mbalimbali hapa Nchini na nje ya nchi.

Maandalizi ya Tamasha yanaendelea vizuri na katika kufanikisha Tamasha hili, ASET imeandaa ligi ndogo itakayoshirikisha timu 12 ikiwemo Timu ya Twanga Pepeta FC iliyoundwa na wanamuziki na wadau wa karibu wa Bendi.

Uzinduzi wa mwaka huu tumeamua kuuweka tofauti kama zinduzi zilizopita ili kuenda sambamba na maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru wa Tanzania Bara. Bendi inataraji kuingia kambini wiki moja kabla ya tarehe ya uzinduzi ili kujitayarisha vizuri kwa ajili ya shoo kali.

HASSAN REHANI.
MENEJA ASET.




Posted by Bigie on 10:27 PM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.