MAHAKAMA YAWAONYA WABUNGE WA CHADEMA WALIOMPIGA NA KUMDHALILISHA MKUU WA WILAYA YA IGUNGA


MAHAKAMA ya Mkoa wa Tabora, imewaonya wabunge wawili wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kwa kitendo cha kushindwa kuhudhuria mahakamani kusikiliza kesi inayowakabili ya kumdhalilisha Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Fatuma Kimario.
Akitoa onyo hilo jana, Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, alisema mahakama inalazimika kuwaonya washtakiwa hao, kutokana na kutoridhika na sababu zilizowasilishwa mahakamani hapo na upande wa utetezi.

Alisema kitendo hicho kinaonyesha kuwa washtakiwa hao wanajali kazi zao na kutotoa kipaumbele kwa mahakama, hivyo kama hawatafika mahakamani watafutiwa dhamana ili wakakae rumande.
Hakimu Simba alienda mbali zaidi na kusema hata kama ni wabunge wanatakiwa kuheshimu sheria za mahakama, hivyo chochote kinachotokea kinatakiwa kutolewa kwa maelezo na sababu zinazopelekea kutokuhudhuria mahakamani na kuomba ruhusa vinginevyo kesi hiyo haitaisha mapema.

Awali kabla ya uamuzi huo, Wakili Mwandamizi, Mussa Kwikima, aliyewawakilisha washtakiwa hao, aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa wa kwanza na wa pili ambao ni wabunge: Sylivester Kasulumbai (Maswa Mashariki) na Suzan Kiwanga (Viti Maalum), wameshindwa kuhudhuria mahakamani kwa sababu wako kwenye vikao vya kamati za Bunge.

Wakili Kwikima alisema kwamba mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Anwar Kashaga, ameshindwa kuhudhuria mahakamani kwa vile yuko hospitalini Bugando jijini Mwanza akipatiwa matibabu, madai ambayo pia yalielezwa na mdhamini wa mshtakiwa huyo.
Hata hivyo, hoja hizo zilipingwa na mawakili wa upande wa mashtaka, Juma Masanja na Mugisha Mboneko, ambao waliieleza mahakama kwamba hoja hizo hazitoshi kuifanya mahakama ikubaliane nao kwa sababu hazina vielelezo vyovyote kama inavyotakiwa kisheria.
Mshtakiwa wa nne katika kesi hiyo aliyeongezwa katika mashtaka hayo Oktoba 4, mwaka huu, Robert William, amerudishwa rumande baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana ya sh milioni 5, mali isiyohamishika na wadhamini wawili.

Washtakiwa hao wanashtakiwa kwa mashtaka matatu kila mmoja ikiwa ni pamoja na shambulizi la kudhuru mwili, kuiba simu ya mkononi yenye thamani ya sh 400,000 na kumuweka chini ya ulinzi Mkuu wa Wilaya, Kimario, kinyume cha sheria.
Mshtakiwa Kasulumbai, ndiye anayekabiliwa na mashtaka manne yakiwemo hayo matatu na mashtaka mengine ya kutumia lugha ya kashfa dhidi ya mkuu huyo wa wilaya.

Posted by Bigie on 8:46 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.