SERIKALI YASISITIZA,MADAKTARI WALIO KWENYE MGOMO WAREJEE KATIKA VITUO VYAO VYA KAZI.

 Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuhusu mgomo wa madaktari unaoendelea na kutoa wito kwa madaktari hao kurejea kazini  na kuendelea kutoa huduma za utabibu wakati serikali ikiendelea na juhudi za kuboresha maslahi ya watumishi wa sekta ya afya nchini.
 Naibu waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Lucya Nkya (kulia) akimweleza jambo waziri wa Afya na Ustawi wa jamii mara baada kumaliza mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wakitekeleza majukumu yao ya kuihabarisha jamii wakati wa mkutano kati yao na viongozi wa Wizara ya afya uliojadili hatma ya mgomo wa madaktari unaoendelea nchini.
**HABARI KAMILI**

Serikali imewataka madaktari wote nchini walio kwenye mgomo kurejea katika vituo vyao vya kazi na kufanya kazi za utabibu ili kuokoa maisha ya wagonjwa.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dkt. Hadji Mponda amesema  serikali inatambua mchango walio nao wataalam wa afya katika utoaji wa huduma za afya nchini na inaendelea kuboresha maslahi yao.
Amesema serikali kwa kutambua mchango huo imekuwa ikiboresha maslahi yao na kuongeza nafasi za ajira kila mwaka kwa wataalam wenye sifa kutoka  nafasi 1,677 za mwaka 2005/2006 hadi kufikia 9,391 katika  mwaka huu wa fedha 2011/2012.
“Serikali inatambua mchango wa watumishi wa kada za afya nchini na ndio maana nafasi za ajira zimekuwa zikiongezeka kila mwaka hasa katika mwaka huu wa fedha 2011/2012”
Amefafanu kuwa madaktari kupitia Chama chao (MAT) wamewasilisha madai mbalimbali serikalini yakiwemo nyongeza ya posho ya kuitwa kazini baada ya kazi na madaktari kupewa nyumba za kuishi karibu na hospitali amesema kuwa serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuboresha maslahi hayo ili kuwawezesha wataalam hao kutekeleza majukumu yao ikiwemo ujenzi wa nyumba 8 za madaktari kwa wilaya 18 pamoja na kufanya maboresho ya posho.
“Serikali imepata fedha kutoka Mfuko wa Dunia(Global Fund) kwa ajili ya kujenga nyumba za madaktari na kwa kuanzia wilaya 18 zilizo pembezoni zimechaguliwa kujengewa nyumba 8 kila wilaya kama hatua ya kuboresha upatikanaji wa nyumba”
Kuhusu malipo ya udhamini kwa madaktari wanaochukua mafunzo ya uzamili,Kuhamisha madaktari bingwa wenye mikataba ya Ajira na Hospitali ya Taifa Muhimbili, Posho ya mazingira hatarishi na ajira za madaktari amesema kuwa baada ya serikali kupandisha hadhi ya hospitali za mikoa kuwa hospitali za Rufaa za mikoa kumekuwa na umuhimu wa madaktari hao kwenda kufanya kazi katika hospitali hizo na kuongeza kuwa idadi ya udhamini wa madaktari katika mafunzo ya uzamili imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Aidha kuhusu madai  ya kutaka nyongeza za mishahara ya shilingi milioni 3.5 kwa mwezi Dkt. Mponda ameeleza kuwa mishahara ya watumishi serikalini hufuata miundo ya utumishi (Scheme of Service)iliyopo huku akibainisha kuwa muundo wa malipo ya watumishi wa umma katika sekta ya afya umeboreshwa.
“Lazima tukubali kuwa baada ya kuboreshwa kwa miundo ya utumishi wa umma wafanyakazi wa sekta ya afya hivi sasa wanapata mishahara mikubwa kuliko watumishi wengine serikalini” amesisitiza.

Posted by Bigie on 8:52 AM. Filed under . You can follow any responses to this entry through the RSS 2.0
.

Featured Post

NEC ya ahirisha uandikishaji kwa BVR mikoa 4 nchini

Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeahirisha zoezi la uandikishaji kwa BVR katika mikoa minne  ambayo ni  Arusha, Kilimanjaro, Manyara pamoja ...

2010 BlogNews Magazine. All Rights Reserved. - Provided by Free Blogger template.