WAZIRI MKUU AWATAKA MADAKTARI KUTOENDELEA NA MGOMO HUKU AKIOMBA VIONGOZI WA CHAMA CHAO WAONANE NAYE MUDA WOWOTE
JAMII 12:14 AM
Waziri Mkuu Mheshimiwa MIZENGO PINDA amezungumzia mgogoro unaoendelea kati ya Chama Cha Madaktari na serikali huku akiwataka Madaktari kurejea kazini ili kuokoa maisha ya binadamu wakati madai yao yakiendelea kutafutiwa ufumbuzi.
Katika mkutano wake na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari uliofanyika leo ofisini kwake jijini Dar es salaam Waziri Mkuu, amewaomba Madaktari kurejea kazini na kuachana na mgomo huku akiwataka viongozi wa Chama hicho kuonana naye muda wowote kuanzia sasa.
Kimsingi amesisitiza kuwa hakuna jambo zuri kama kukaa meza moja lengo likiwa ni kuyatafutia ufumbuzi madai yao hivyo hakuna sababu ya kuendelea na mgomo huo kwani anayepata tabu ni mgonjwa.
Pamoja na mambo mengine katika mkutano huo pia Mheshimiwa PINDA amezungumzia masuala ya Uchumi, Elimu, Miundombinu, Mchakato wa Katiba Mpya, Mifugo, Uvuvi, Mafuriko yaliyojitokeza nchini, Umeme, Chakula na Maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru yaliyofanyika Disemba 9 mwaka jana.
Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya Waziri Mkuu amesema serikali tayari imeunda kamati ya kutafiti ni wapi yatakuwa Makao Makuu ya Tume itakayoundwa kwa ajili ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katika Mpya pamoja na kuandaa vitendea kazi vya Tume hiyo.
Pia kuhusu zoezi la kuwahamisha waathirika wa mafuriko katika makazi mapya ya Mabwepande amesema linaendelea vizuri huku akisisitiza kuwa serikali itawachukulia hatua kali watu watakoendelea kukaa sehemu hatarishi za Mabondeni.
Akizungumzia suala la baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi kufutiwa matokeo yao kutokana na udanganyifu amesema serikali ipo katika mchakato wa kuangalia mfumo wa ufundishaji unaotumika nchini na kama utaonekana una kasoro basi utabadilishwa mara moja.
Kuhusu uteuzi wa Wakuu wa Mikoa Mipya pamoja na Wakuu wa Wilaya Mheshimiwa PINDA amesisitiza kuwa watajulikana mapema mwezi ujao.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema hatagombea nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kama ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya wanasiasa kuwa yeye ni miongoni mwa wagombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao.






