RAIS Jakaya Kikwete ameendelea kuaga Watanzania kila anapopata fursa
ya kukutana nao, huku mafanikio ya miaka kumi ya uongozi wake
yakijidhihirisha katika maeneo mbalimbali, ikiwemo katika Bunge la
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambako Bajeti ya Serikali kupitia
wizara mbalimbali imekuwa ikijadiliwa na kupitishwa.
Mwishoni mwa wiki hii akiwa jijini Stockholm nchini Sweden
alikokwenda kwa ziara ya siku tatu, ambayo pia ni ya kwanza ya kuaga
nchi wahisani, Rais Kikwete alikutana na Watanzania waishio nchini humo,
ambako kabla ya kuwaaga, alielezea changamoto anazoziacha.
Rais Kikwete katika mazungumzo hayo, amesema Rais ajaye anakabiliwa
na changamoto ya kuhakikisha Tanzania inayoundwa na Muungano wa nchi
mbili, inaendelea kuwa moja kwa kudumisha umoja wa Watanzania na amani.
“Hapa tulipofikia lazima tuhakikishe Taifa linakuwa moja, kuna vyama
na makabila mbalimbali, lakini lazima tuhakikishe nchi inabaki moja,”
amesisitiza Rais Kikwete.
Rais Kikwete pia alielezea matumaini yake kuwa Tanzania itapata
kiongozi mzuri na kuelezea mafanikio ambayo Serikali yake imeyapata na
kutumaini kuwa yatadumishwa na kuendelezwa na Rais ajaye.
Uchumi Awali akizungumzia mafanikio yaliyopatikana katika uchumi
alipokutana na Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Lofven, Rais Kikwete
alisema uchumi wa Tanzania umekua kwa wastani wa asilimia 7, katika
kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Mbali na kukua kwa uchumi wastani, pato la Taifa limekua kwa zaidi ya
mara tatu, kutoka Dola za Kimarekani bilioni 14.4 hadi kufikia Dola
bilioni 49.2 za Marekani.
Aidha, pato la mtu mmoja mmoja kwa mwaka 2005, wakati Rais Kikwete
alipokuwa akiingia madarakani lilikuwa Dola za Marekani 375, lakini
mwaka jana lilifikia Dola za Marekani 1,038.
Mafanikio hayo kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, zilisababisha Waziri
Mkuu wa Sweden, Lofven, kuona umuhimu wa kuanzisha awamu nyingine ya
uhusiano katika maendeleo, utakaoleta maana zaidi.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo Sweden (SIDA),
Torbjorn Pettersson, ambaye pia alikutana na Rais Kikwete, alieleza kuwa
Sweden imeridhishwa na kiwango cha maendeleo na juhudi za kupunguza
umaskini nchini Tanzania.
Hata hivyo, Rais Kikwete alipokuwa akizungumzia kasi ya kuondoa
umasikini, alisema bado juhudi za kuondosha umaskini zinahitajika na
zitafanikiwa kwa kuelekeza nguvu kwenye kilimo, ambacho ndicho
kinachoajiri na kutegemewa na Watanzania wengi zaidi hasa wanaoishi
vijijini.
Rais Kikwete pia amefanya mazungumzo na Spika wa Bunge la Sweden,
Urban Ahlin, pamoja na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa nchini
humo na kushukuru kwa misaada ya maendeleo kwa takribani miaka 50 sasa.
Viongozi hao wamempongeza Rais kwa kufanya ziara ya shukrani na
kuwaaga, kwani ni mara chache kwa viongozi wengi wa Kiafrika kuaga na
kuondoka madarakani.
Mbali mazungumzo hayo ya Sweden, mafanikio mengine ya Serikali kwa
miaka 10 iliyopita, kwa wiki ya tatu sasa yamegeuka nguzo mbuhimu ya
kutetea bajeti za wizara mbalimbali bungeni na katika warsha mbalimbali.
Afya Kwa mfano katika wiki hii katika sekta ya afya, Waziri wa Afya
na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alipokuwa akizungumza na wahariri wa
vyombo vya habari, aliwataka kusoma takwimu za mafanikio ya Tanzania
ikilinganishwa na nchi zingine badala ya kuishia kusoma bajeti ya sekta
hiyo pekee.
Kwa mujibu wa Dk Rashid, pamoja na Tanzania kuwekeza asilimia 2.8 tu
ya pato la Taifa katika sekta ya afya, vifo vya watoto chini ya miaka
mitano vimepungua na mafanikio hayo ni makubwa kuliko katika nchi
zinazoonekana kupiga hatua zaidi katika uwekezaji huo.
Alitaja nchi ya Botswana yenye uwekezaji wa asilimia 3 ya pato la
Taifa katika afya na Zambia yenye asilimia 4.2 ya pato la Taifa katika
sekta hiyo, kwamba mataifa hayo katika kila vizazi hai 1,000 wamekuwa
wakipoteza watoto wengi zaidi.
Wakati Tanzania ikipoteza watoto 52 katika kila watoto hai 1,000
wanaozaliwa, Kenya wao wanapoteza watoto 71, Zambia watoto 87 na
Cameroon ni watoto 95 katika kila vizazi haivyo 1,000.
Umeme Katika upatikanaji wa huduma za nishati na umeme, mpaka mwaka
jana, Serikali ilikuwa imefikisha umeme kwa zaidi ya asilimia 35 ya
Watanzania, kutoka asilimia wastani wa chini ya asilimia 15 iliyokuwepo
mwaka 2005.
Akizungumza bungeni jana, Waziri wa Nishati na Madini, George
Simbachawene alisema idadi ya wateja waliounganishiwa umeme vijijini
imefikia asilimia 68. Idadi hiyo imeongezeka kutoka 143,113 mwaka 2013
hadi kufikia wateja 241,401 Aprili mwaka huu.
Alisema wateja hao wameunganishiwa umeme kupitia miradi ya Wakala wa
Umeme Vijijini (REA) na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
Bomba la gesi Akizungumzia jitihada za kuanza kutumia hazina ya gesi
asilia kwa ajili ya kuzalisha umeme badala ya mafuta mazito
yanayosababisha umeme uwe bei ghali nchini, Simbachawene alisema mitambo
ya kusafisha gesi asilia na bomba la gesi asilia, vitaanza kazi rasmi
Septemba mwaka huu.
Alisema ujenzi wa bomba la gesi asilia kutoka Mtwara kupitia Lindi
hadi Dar es Salaam umekamilika, ujenzi wa mitambo ya kusafirisha gesi
asilia katika eneo la Madimba, Mtwara umefikia asilimia 99 na mitambo ya
Songo Songo, Lindi nao umefikia asilimia 99. “Mitambo na bomba hilo
vitaanza kufanya kazi (Commercial Operational Date) Septemba 2015.
“Haya ni matokeo ya utekelezaji wa miongoni mwa miradi iliyoanishwa
kwenye Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2011/12 - 2015/16),” alisema
Simbachawene.
Alisema matumizi ya gesi asilia yatachochea ukuaji wa viwanda,
utunzaji wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya kuni na mkaa, kuongeza
ajira na hatimaye kuleta maendeleo ya uchumi na kijamii kwa ujumla.
Elimu Katika elimu, mwaka 2005 wakati Rais Kikwete akiingia
madarakani, Bajeti ya Serikali katika sekta hiyo ilikuwa Sh bilioni 600,
lakini mwaka jana ilifikia Sh trilioni 3.4.
Sababu ya uwekezaji huo mkubwa, Rais Kikwete aliwahi kusema
alipoingia madarakani, alikuta Tanzania yenye watu wengi zaidi katika
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, iko nyuma ikilinganishwa
na Kenya na Uganda, kwa idadi ya wanafunzi waliokuwa wakisoma shule za
sekondari na vyuo.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mwaka 2005 wanafunzi waliokuwa wakisoma
sekondari ni zaidi ya 500,000, wakati nchini Uganda waliokuwa wakisoma
sekondari walikuwa zaidi ya 700,000 na Kenya zaidi ya 900,000.
Kwa upande wa vyuo vikuu, Tanzania ilikuwa na wanafunzi 40,000 tu wakati Uganda ilikuwa na wanafunzi 124,000 na Kenya 180,000.
Hatua zilizochukuliwa, Rais Kikwete alisema Serikali kwa kushirikiana
na wananchi, waliamua kujenga shule za sekondari za kata, ambapo
wananchi walihamasishwa, wakahamasika wakajenga shule mpaka Mkurugenzi
mmoja wa elimu, akahofia kukosa walimu wa kupeleka katika shule hizo.
Kwa sasa Tanzania ina wanafunzi 1,800,000 wanaosoma sekondari na
imeshaipita Uganda yenye wanafunzi 1,700,000 wanaosoma elimu ya
sekondari, lakini imezidiwa na Kenya ambayo ina wanafunzi 2,100,000.
Hata hivyo alisema ni rahisi kuipita Kenya kwa hilo pengo la
wanafunzi 300,000, kwa kuwa shule za sekondari zilizopo zina nafasi ya
kuongeza wanafunzi milioni mbili zaidi.
Kwa upande wa elimu ya juu, Rais Kikwete alisema vyuo vikuu
vimeongezeka kutoka 26 mwaka 2005 hadi kufikia 52 na idadi ya wanafunzi
walio katika vyuo vikuu ilitoka 40,719 hadi kufikia 200,956.
Hata bajeti ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu imeongezeka kutoka Sh bilioni 56.1 hadi Sh bilioni 345 mwaka 2014.