BARAZA a Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Singida Vijijini, limemshutumu mbunge wao, Lazaro Nyalandu kwa kusababisha chama hicho kukosa ushindi mnono kwenye baadhi ya maeneo katika jimbo la Singida Kaskazini wakati wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa hivi karibuni.
Katika Kikao cha Baraza hilo kilichoketi mjini hapa juzi kutathmini Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, wajumbe hao walisema kuwa sababu kuu ya baadhi ya maeneo kuchukuliwa na upinzani ni mbunge huyo, ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii, kushindwa kutimiza ahadi zake kwa wakati.
Walisema kuwa kati ya vijiji 84 vilivyopo kwenye jimbo hilo, vijiji vinane vimechukuliwa na upinzani wakati kati ya vitongoji 436, vitongoji 49 vimechukuliwa na upinzani.
“Hii ni kutokana na mbunge wetu kuwa na ahadi hewa na kukataa baadhi ya ahadi alizowahi kutoa mwenyewe,” walisema wajumbe.
Akisoma maazimio ya kikao hicho, Mwenyekiti wa UVCCM Singida Vijijini, Shaban Mang’ola alisema kuwa kutokana na hali hiyo wamempa mbunge huyo muda wa siku 14 tu kuweza kufika Singida mara moja kuonana na jumuiya hiyo na kutoa maelezo ya kuridhisha juu ya mustakabali wa ahadi zake.
Aidha, maazimio hayo yanasema kuwa iwapo mbunge huyo atashindwa kufanya hivyo katika muda uliopangwa, UVCCM itaitisha mkutano mkuu wa vijana wa jimbo na kutoa maamuzi watakayaona yanafaa.
Waziri Nyalandu anadaiwa kuhamasisha na kuahidi kuwapatia mikopo vijana zaidi ya 9,000 wa jimbo hilo, ahadi ambayo hajatimiza hadi hivi sasa. Wajumbe walidai kuwa kila kijana aliyetaka kuchukua mkopo aliingia gharama ya Sh 8,000. Pia anadaiwa kuitisha ligi ya mpira wa miguu na kuahidi kuwapatia zawadi washindi lakini baadaye akaikana ligi hiyo.
Aidha, mbunge huyo anadaiwa kuwatukana hadharani baadhi ya wapiga kura wake jambo, ambalo baraza hilo limekiita kuwa ni dharau kwa jumuiya ya umoja huo.
Hata hivyo, Nyalandu akizungumza kwa simu na gazeti hili alisema taarifa hizo hazina ukweli wowote na kwamba kuna watu walilipwa fedha kwa ajili ya kumchafua na kukichafua chama.
“Habari hizi ni za kuchafua tu na uongo. Kuna watu walilipwa na Mwenyekiti huyo wa UVCCM anajua, kisha wakaitisha mkutano kinyume na utaratibu pamoja na waandishi wa habari, wakachaguliwa vijana watano ili kusema hayo waliyosemwa. Kwenye Jimbo langu, CCM imefanya vizuri sana na huo ndio ukweli,” alisema.
Nyalandu ambaye pia ni Waziri wa Maliasili na Utalii alisema katika jimbo lake hilo la Singida Kaskazini, CCM imeshinda vijiji 179 na kushindwa katika vijiji vinane na kuongeza kuwa huo ndio ukweli halisi na kuhoji kuwa kwa idadi hiyo ya ushindi kweli CCM imeshindwa?
Kwa mujibu wa Nyalandu, leo Kamati ya Siasa ya Wilaya inakutana katika mkutano wa dharura ambapo watajadiliana kuhusu mwenyekiti huyo anayedaiwa kuhongwa fedha na kufanya mkutano huo wa vijana usiokuwa rasmi na kwamba moja ya hatua zinazotarajiwa kuchukuliwa dhidi ya Mang’ola ni kusimamishwa na chama.
“Ni watu wenye nia mbaya tu wameamua kuitisha mkutano kinyume cha Sheria. Lakini Kamati ya siasa ya wilaya inaitisha mkutano wa dharura na kuna tamko litatolewa kuhusiana na mwenyekiti huyo, kwa sababu inajulikana kabisa kwamba walipewa hongo kutoa taarifa hizo za uongo,”